WIMBI la viongozi wakuu wa
Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, kuendelea kuwindwa na watu wasiofahamika,
limeendelea kushika kasi, baada ya usiku wa kumkia jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa
kampuni hiyo, Hussein Bashe, kunusurika kutekwa.
Tukio hilo, lilitokea juzi usiku wakati Bashe alipokuwa
akitoka ofisini kwake Sinza Kijiweni, akielekea nyumbani kwake
Mbezi.
Akizungumzia tukio hilo, Bashe alisema wakati anaondoka
ofisini kwake kwa gari lake, alianza kufuatiliwa kwa nyuma na magari mawili,
likiwamo aina ya NOA ambalo hata hivyo hakufanikiwa kujua lilikuwa na watu
wangapi.
“Kama kawaida nilishinda ofisini kwa ajili ya majukumu
yangu ya kazi na muda wa kutoka ulipowadia, niliondoka kurudi
nyumbani.
“Awali wakati navuka geti la pale ofisini, sikuwa na shaka
yoyote, lakini kadri nilivyozidi kuendelea na safari yangu, niliona nyuma
nafuatiliwa na magari mawili ambayo yalikuwa yakiendeshwa kwa
tahadhari.
“Nilipofika Mwenge ile NOA ilikuwa bado iko nyuma yangu,
sasa nikaanza kupatwa na wasiwasi, nikajua hapa kuna jambo.
“Moyoni niliendelea kumuomba Mungu, huku nikijiuliza
maswali mengi hawa jamaa ni akina nani, kwa kweli sikupata jibu
zuri.
“Nilipofika Mbezi, niliona yale magari yanazidi
kunisogelea, kwa hiyo, nikaamua kuongeza kasi na wao wakazidi kuja
tu.
“Wakati niko Mbezi jirani na njia panda ya kwenda kwangu,
gari moja lilinipita kwa kasi na kuendelea mbele.
“Unajua kuelekea kwangu pale kuna barabara kama tatu ambazo
zote unaweza kuzitumia na zikakufikisha hadi nyumbani kwangu,” alisema Bashe na
kuongeza:
“Nilichokifanya nilipita barabara ya kwanza na wao wakapita
barabara ya pili na ghafla nilikutana nao uso kwa uso, wakati huo naelekea
kwangu na kibaya zaidi, gari lao walizima taa kubwa na kuacha
ndogo.
“Walivyona gari langu, walinipiga taa kuashiria wanakata
kona, lakini cha ajabu walinifuata nyuma na hapo nikaanza kujua sasa
nafuatiliwa.
“Nilichokifanya sikwenda nyumbani moja kwa moja, bali
niliamua kupaki gari kwenye grosari moja iliyoko jirani na
kwangu.
“Baadaye niliamua kuondoka ili niwazunguke kwa nyuma nisome
namba za gari lao, lakini sikufanikiwa kwa sababu taa za nyuma zilikuwa
zimezimwa,” alisema Bashe.
Kwa mujibu wa Bashe, baadaye aliingia nyumbani kwake na
kuwakuta wageni ambao alikaa nao hadi saa sita usiku baada ya kuwasimulia tukio
lilivyokuwa.
“Sasa basi, wakati jamaa zangu hao wanaondoka kurudi kwao,
walikuta lile gari pale pale njiani, wakanipigia simu, kwamba lile gari
nililowasimulia linawafuatilia.
“Nikawaambia wageuze gari lao ili wasome namba, lakini
hawakufanikiwa hata kidogo kwa sababu wale jamaa walishtuka na kuamua
kutimua.
“Kwa hiyo, nilichokifanya nilikwenda pale Polisi Kawe na
kutoa taarifa ambapo nilipewa RB yenye namba KW/RB/2899/2013,”
alisema.
Machi 6, mwaka huu, Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari
(2006) Ltd, Absalom Kibanda, alitekwa na kuteswa na watu
wasiofahamika.
Katika tukio hilo, Kibanda alitobolewa jicho la kushoto,
alipigwa kichwani na kitu chenye ncha kali na kunyofolewa kucha. Kwa sasa yuko
nchini Afrika Kusini ambako anaendelea na
matibabu.
JUMAMOSI, MACHI 30, 2013
01:07 NA MWANDISHI WETU, DAR

.jpg)

Post a Comment