Kwa ufupi
Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo wakati zimeundwa kamati mpya za Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ya Ulinzi na Usalama.
Dar es Salaam. Hatimaye Bunge limetangaza mabadiliko ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge zinazotarajiwa kuanza kukutana kuanzia Jumatatu ijayo, huku baadhi ya vigogo wakiwekwa katika kamati moja na kufanya zoezi la kuchagua wenyeviti wa kamati hizo kuwa gumu.
Uteuzi wa majina ya wajumbe hao unakuja mwezi mmoja tangu kumalizika kwa Mkutano wa 10 wa Bunge ambapo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo wakati zimeundwa kamati mpya za Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ya Ulinzi na Usalama.
Majukumu ya Kamati ya Bajeti ni kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali na sera za fedha pamoja na kuainisha na kupendekeza vyanzo vya mapato ya Serikali na kufuatilia mwenendo wa uchumi.
Wajumbe waliokuwepo POAC ambao wamehamishiwa PAC ni Zitto Kabwe, Deo Filikunjombe, Ester Matiko, Zainab Kawawa na Kheri Ali Khamis.
Kamati ya PAC ni lazima iwe na mwenyekiti kutoka kambi ya upinzani, hali inayofanya uchaguzi wake kuwa mgumu kwa kuwa Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo naye ni mjumbe wa Kamati hiyo.
Cheyo anatazamiwa kupata upinzani mkali kutetea kiti chake kwani atapata upinzani mkali kutoka kwa Zitto, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya POAC.
Kuna tetesi tayari kuwa Zitto, ambaye alilalamikia kitendo cha kuvunjwa kwa kamati ya POAC, ameanza kampeni za chinichini ili kumtoa Cheyo, ambaye ameshikilia nafasi hiyo tangu mwaka 2005.
Wengine ambao walikuwa wajumbe wa POAC ambao wamehamishiwa Kamati ya Nishati na Madini ni Jerome Bwanausi na Murtaza Mangungu, pia katika kamati hiyo ya Nishati na Madini kuna wajumbe wapya ambao ni Anne Kilango na David Silinde.
Wengine waliokumbwa na mabadiliko hayo ni Grace Kiwelu ambaye amehamishwa kutoka Kamati ya Miundombinu kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira sambamba na John Mnyika na Ester Bulaya.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ametupwa katika kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, pia Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Brigedia Mstaafu Hassan Ngwilizi akibaki katika kamati hiyo, pia yuko katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo imemegwa kutoka katika Kamati ya Mambo ya Nje ambayo hivi sasa inaitwa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati hiyo kabla ya kugawanywa, Edward Lowassa pamoja na makamu wake Mussa Azzan Zungu wamekuwa wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Katika uteuzi huo Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, amekuwa mjumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge na Kamati ya Bajeti, huku Andrew Chenge, Tundu Lissu, Christopher Ole Sendeka pamoja na Zungu wakiwa katika Kamati ya Kanuni za Bunge.
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Iddi Azzan amepelekwa katika Kamati ya Masuala ya Ukimwi.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye awali alikuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi, sasa amekuwa mjumbe wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara ambayo imeunganishwa na kuwa moja.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Selemani Zedi amepelekwa LAAC, huku aliyekuwa mjumbe wa kamati hiyo, Godfrey Zambi akipelekwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Orodha hiyo inaonyesha kuwa kuna Kamati 17 ikilinganishwa na 18 za awali.
Tayari kampeni za chinichini zimeshaanza kwa baadhi ya wabunge ambao wangependa kuwa wenyeviti wa kamati hizo mpya, ambapo wabunge wa CCM jana walitarajiwa kukutana katika Ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuchagua wenyeviti wa kamati hizo.
MWANANCHI
Post a Comment