Kamishna Msaidizi wa
Polisi (ACP) Shabani Kimea (54) amefariki dunia machi 27 mwaka huu katika
Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa ajili ya
matibabu ya maradhi.
Taarifa iliyotolewa na
kuthibitishwa na Msemaji wa Polisi Advera Senso, imesema Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na Familia ya Marehemu tayari imefanikisha kuusafirisha mwili wa
marehemu kwenda Kijijini kwao Mwera mkoani Tanga, kwa ajili ya Mazishi.
Senso alisema Kufuatia
msiba huo Jeshi la Polisi nchini limepata pengo kubwa kwa kuondokewa na
kamishina huyo kwa kuwa alikuwa mtendaji hodari hali iliyopelekea kutunukiwa
nishani ya utumishi wa muda mrefu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh
Jakaya Mrisho Kikwete.
Alisema Mkuu wa Jeshi la
Polisi Nchini IGP Said Mwema amezipokea taarifa za kifo hicho kwa huzuni hasa
ukizingatia hivi sasa Askari mmoja anahudumia watu takribani 1300 hadi 1500
hivyo kufariki kwa Ofisa, Mkaguzi au Askari mmoja ni pengo kubwa kwa Jeshi la
Polisi na Watanzania hasa katika nyanja ya usalama na ameitumia familia ya
marehemu salamu za rambirambi.
ACP Kimea alijiunga na
Jeshi la Polisi Mwaka 1985 na kupandishwa vyeo mbalimbali hadi kufikia Cheo cha
Kamishna Msaidizi wa Polisi ambapo mpaka mauti yanamkuta alikuwa mkuu wa Kitengo
cha Mipango ya Raslimaliwatu (Human Resource and Planning) Makao Makuu ya Jeshi
la Polisi na nafasi nyingine alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Mkuu wa
Upelelezi wilayani Misungwi, Mkuu wa Polisi wilayani Misungwi na Geita pamoja na
Mnadhimu Mkuu wa Polisi Mkoani
Morogoro.


Post a Comment