--------------------------------
Ndugu zangu,
Usiku huu nikiwa kwenye shughuli ya shule ya
watoto wangu pale Highlands Hall Iringa nilifikiwa na habari kuwa Kijana
Ludovick amekamatwa na polisi kuhusiana na tuhuma za kuhusika na kuteswa
mwandishi Absalom Kibanda.
Namfahamu kijana Ludovik
tangu akiwa Chuo Kikuu ( DUCE). Ni mmoja wa Watanzania wengi walionifahamu
kupitia kazi zangu za magazetini.
Kwangu Ludovick ni
kijana mtaratibu na mpole sana, na hata niliposikia habari hizi kwa namna
fulani nimeshtushwa nazo.
Ludovick ambaye amekuwa
akiishi Dar ni mmoja wa vijana waliokuwa wakinisaidia kwa kujitolea kwenye kazi
zangu za mitandaoni, hususan kwenye Mjengwablog na website ya Kwanza Jamii.
Amekuwa na mchango mkubwa, na hata katika miezi ya karibuni,ndiye yeye aliyekuwa
akifanya kazi ya kuingiza magazeti kwenye Mjengwablog kila
asubuhi.
Akiwa Dar na mimi
nikiwa Iringa, Ludovick hakuwa mwajiriwa wangu kama wanavyodhani wengine, bali ,
amekuwa ni mmoja wa vijana waliokuwa tayari kunisaidia kwa kazi za hapa na pale
ikiwamo kunipelekea invoice kwa watangazaji kwenye
Mjengwablog.
Mara nyingi nimekuwa
nikimtambulisha kama ' Msaidizi wa Mwenyekiti'.
Na jana nilimwomba aje
Iringa aniletee vitabu vyangu vya invoice na risiti kwa vile nilitarajia ugeni
wa kutoka TMF- Mfuko wa Ruzuku kwa vyombo vya habari. Kwamba huenda vitabu hivyo
vingehitajika wakati wa mazungumzo na watendaji wa TMF yaliyofanyika leo
asubuhi.
Hata hivyo, katika hili
lililomtokea, siwezi hapa kumtetea wala kumtia hatiani. Maana, naye ni binadamu
kama wengine, siwezi kusema kuwa ninamfahamu sana. Kwa vile yuko mikononi
mwa vyombo vya usalama , nina imani, kuwa vyombo hivyo vitafanya kazi yake ili
kutusaidia katika kupata ukweli wa jambo zima.
Na kama ni kweli kwa
namna yoyote ile itathibitishwa kuwa ameshiriki njama za kupanga mikakati hiyo
ya kigaidi, basi, ahukumiwe kwa dhambi hiyo.
Ni mimi:
MAGID MJENGWA
Post a Comment