Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd akiangalia waya wa umeme aina ya shaba ambao amezuia mauzo yake hadi
uongozi wa kiwanda cha sukari utapokaa pamoja na Wizara ya fedha kufikia
maamuzi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiuagiza
Uongozi wa Kiwanda cha sukari Mahonda kukaa pamoja na Wizara inayosimamia Fedha
Zanzibar ili kufikia mwafaka wa matumizi ya waya wa umeme wa aina ya shaba ambao
tayari ulikuwa umeshauzwa.
Baadhi ya Maafisa wa Kiwanda cha Sukari Mahonda
wakibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati
alipokitembelea kiwanda hicho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi akitembelea kiwanda cha sukari Mahonda akiwa pamoja na Uongozi wa
Kiwanda hicho. Picha na
Hassan Issa –Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
--
Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imezuia mauzo ya waya wa umeme aina ya Shaba uliokuwa
ukitumiwa na Kiwanda cha Sukari Mahonda ambao tayari ulikuwa umeshauzwa kwa
shilingi Milioni Mbili na Nusu (2,500,000/-).
Waya huo
unakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni
300,000,000/-.
Zuio hilo
limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati
akizungumza na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari pamoja na Uongozi wa Wizara ya Nchi
Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar katika ofisi za
Kiwanda cha Sukari Mahonda.
Balozi Seif
amesema zipo hitilafu zinazotumiwa na baadhi ya maafisa wa Serikali katika mauzo
ya mali za Serikali na matokeo yake kusababisha kuitia hasara kubwa Serikali
Kuu.Amesema Mali za Serikali zimekuwa zikinunuliwa kwa gharama kubwa lakini
uuzwaji wake baada ya matumizi hakulingani na thamani ya mali zenyewe jambo
ambalo hutoa mwanya kwa mali hizo kuuzwa kwa bei ya chini
kabisa.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi
na Mipango ya Maendeleo kukaa pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari kuangalia
namna ya matumizi ya waya huo ambao ulikuwa ukitumiwa na Kiwanda
hicho.
Waya huo
ulilazimika kufukuliwa na Uongozi wa Kiwanda hicho baada ya kubainika kuanza
kuhujumiwa kwa kukatwa katwa na baadhi ya wezi kufuatia kutambulikana thamani
yake katika masoko ya Kimataifa.
Mapema Mshauri wa
Kiwanda cha Sukari Mahonda Dkt. Hamza Hussein Sabri alisema Zanzibar inatarajiwa
kujitosheleza kwa Sukari ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, kufuatia
uongozi wa Kiwanda cha sukari Mahonda kufanikiwa kupata washirika zaidi katika
kuongeza nguvu ya kuanza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya
Jamii.
Dkt. Hamza
alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Kiwanda hicho umeongeza nguvu za
Wataalam kutoka Kampuni ya Biashara za Nje (Export Trade Group) ambazo matunda
yake yataonekana ndani ya mwaka huu.
“ Tunaimani
thabiti kwamba Zanzibar itaweza kujitosheleza kwa Sukari kufuatia uzalishaji
wetu wa Sukari kuwa mkubwa utakaowezesha Tani 50,000 za miwa kuzalisha Tani 400
za Sukari safi, ikiwa ni sawa na Tani 40 kwa siku kiwango ambacho tunauhakika
kitatosheleza kabisa”. Alisema Dkt. Hamza.
Mshauri huyo wa
Kiwanda cha Sukari Mahonda alifahamisha kwamba wananchi wa maeneo
yanayokizunguka kiwanda na mashamba ya miwa tayari wameshaonyesha moyo wa
kusaidia kuendeleza mradi huo ambao utatoa fursa ya ajira miongoni mwa wananchi
hao.
Naye Mkurugenzi
wa Mashamba wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bw. Narayani amesema taratibu za
uimarishaji wa mashamba ya miwa uko katika hatua nzuri na uoteshaji miwa
unatarajiwa kuanza rasmi kabla ya mwezi wa Aprili Mwaka huu.
Bwana Narayani
amesema hatua za awali zitaanza kwa kujumuisha ekari 1800 zilizopo katika maeneo
ya Mahonda na Upenja ambapo zaidi ya familia 5000 zinatarajiwa kufaidia kiajira
kutokana na mradi huo wa uzalishaji Sukari.
Hata hivyo Bwana
Narayani alieleza kwamba zipo baadhi ya changamoto ikiwemo suala la umeme wa
uhakika ambalo linatafutiwa ufumbuzi kupitia washirika wa maendeleo pamoja na
baadhi ya mashamba ya miwa ambayo yatahitaji kufanyiwa marekebisho kwa vile
yalikuwa yakitumiwa kwa kilimo kingine.
Mkurugenzi huyo
wa mashamba wa Kiwanda cha Sukari amesema kwamba mradi huo wa Sukari Mahonda
umetengewa Dola za Kimarekani kati ya 35 hadi 40 Milioni kuendeshea
mradi.
Amesema kati ya
fedha hizo shilingi za Kitanzania Milioni 65,000,000/- zitaelekezwa katika
uimarishaji wa mashamba ya miwa Mahonda na Upenja ili kuwa na uhakika wa mali
ghafi kabla ya kuanza kwa uzalishaji.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kukagua baadhi ya maeneo ya Kiwanda hicho
ambayo tayari yameanza kufanyiwa marekebisho makubwa na kuridhika na hatua
iliyofikiwa.
Post a Comment