EDWARD
LOWASSA.
Reginald
Mengi.
* AFISA IKULU AHUSISHWA NA
MKAKATI HUO, AFYA YA LWAKATARE YAZIDI KUDOROLA
WAKATI sakata la
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Wilfred Lwakatare anayetuhumiwa kupanga mikakati ya uhalifu na kurekodiwa kwa
video likizidi kuibua maswali, vigogo wengine wanadaiwa kuandaliwa mpango wa
kurekodiwa kwenye video ili kuwachafua na kuwanyamazisha, Tanzania Daima
Jumapili limebaini.
Vigogo hao ni pamoja na
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, Waziri Mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe.
Kunaswa kwa mawasiliano
hayo kunaibua hisia kwamba huenda picha za video za Lwakatare zilizosambazwa
kwenye mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi zikionesha mipango ya kufanya
uhalifu ni ya kughushi.
Kwa mujibu wa habari
hizo kuna mkakati mkubwa unaosukwa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa
vyombo vya dola, kutengeneza video nyingi kwa watu mbalimbali kuwahusisha na
ufadhili wa vitendo vya uharamia na kuwateka na kuwadhuru kama alivyofanyiwa
hivi karibuni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, Absalom
Kibanda.
“Mtu wangu wa karibu
ameniambia kuwa wana mpango wa kumtengenezea video kama hiyo, Mengi, Lowassa na
Freeman Mbowe ili kuwanyamazisha,” ilisomeka sehemu ya taarifa
hiyo.
Mbali ya kuandaliwa
video chafu kama Lwakatare, imedaiwa kuwa Lowassa, Mengi na Mbowe
wanatengenezewa fitna kuionesha jamii kwamba wanafadhili genge la kijasusi
linalosababisha mauji ya raia nchini.
Tangu kuibuliwa kwa
kashfa ya video ya Lwakatare, baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wamekuwa wakipinga propaganda za chini kwa chini kuihusisha CHADEMA na matukio
ya kijasusi ya kuuawa kwa baadhi ya raia na waandishi wa habari, likiwemo tukio
la hivi karibuni la kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda ambaye kwa sasa anatibiwa
nchini Afrika Kusini.
Duru za uchunguzi
zinaeleza kuwa mchezo mzima wa mkanda wa video ya Lwakatare na kuvamiwa na
kupigwa kwa Kibanda, unadaiwa kuchezwa na watumishi wachache wasio waaminifu
ndani ya vyombo vya dola.
Uthibitisho wa madai
hayo unatokana na mawasiliano ya ofisa mmoja wa Ikulu ambaye jana mawasilino
yake ya siri na watu mbalimbali yalinaswa akiwapongeza vijana walioandaa video
ya Lwakatare na kutaka viongozi wa CHADEMA wakamatwe na kwamba hiyo ni kete
kubwa kwa CCM.
Hata hivyo kasoro moja
ya mawasiliano hayo ni kwamba mtoa habari hakuweka kopi halisi wa hayo
mawasiliano badala yake aliweka faili ambalo liko kwenye mfumo wa
PDF.
Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alipotafutwa kwa simu kuzungumzia taarifa
hiyo na kuhusishwa kwa ofisa mmoja wa Ikulu, hakuweza
kupatikana.
Wakati huohuo,
hali ya afya ya Lwakatare ni mbaya.
Imeelezwa kuwa
hali ya kiongozi huyo imezorota kutokana na kiwango cha sukari
kupanda.
Taarifa
zilizothibitishwa na wakili wake na watu wake wa karibu, zinasema kuwa hali yake
ni mbaya na Jeshi la Polisi lilikuwa likifanya utaratibu wa kumkimbiza
hospitalini ili aweze kupatiwa matibabu.
“Hali ya Lwakatare ni
mbaya, sukari imepanda sana, kwa hali yake hii ya ugonjwa tunatafuta uwezekano
wa Jeshi la Polisi kumpeleka hospitalini, ingawa bado hawajakubali au kuonyesha
kuwa wanampeleka hospitalini,” alisema wakili wake, Nyaronyo
Kicheere.
Jana gazeti hili
liliripoti taarifa ya Kicheere akisema pamoja na polisi kumshikilia Lwakatare,
walikuwa wamemweka katika mahabusu isiyokidhi hali ya afya ya kiongozi huyo,
ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
Alisema: “Hali ya
Lwakatare ni mbaya, anaumwa kisukari, anahitaji chakula kila baada ya saa nne,
na kupata huduma ya haja ndogo mara kwa mara, lakini amewekwa katika chumba
ambacho hakina huduma ya choo ingawa vinapatikana pale
polisi.
“Ni kinyume cha sheria
kumweka mtu polisi saa zote hizo, na wanafanya vile utadhani huyu wameshamtia
hatiani. Hatuwezi kuhamishia familia yake pale ili wampatie chakula kila
mara.”
Aliongeza kuwa juzi
alipotolewa kutoka katika chumba alipohifadhiwa alikuwa na hali mbaya kiasi cha
kushindwa kuongea au kusimama kwa kuwa alikuwa hajala kwa muda mrefu kulingana
na hali ya ugonjwa wake.
“Mtu wa aina hii sio wa
kuwekwa mahabusu muda mrefu, kwanza Lwakatare sio mtu wa kutoroka, ukiachilia
mbali suala la kisheria linalowalazimisha polisi kumpeleka mahakamani ndani ya
saa 24,” alisema.
Gazeti hili lilimtafuta
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova kuhusu suala hilo na
akasema:
“Sisi hatuna haja ya
kuletewa maombi na upande wowote, mahabusu yeyote anayeumwa anapelekwa
hospitalini, sisi tunakagua chumba cha mahabusu kila baada ya nusu saa,
tunakagua afya tukikuta kuna mgonjwa basi anapelekwa hopitali, ila kwa suala
hasa la Lwakatare wasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Ilala.”
Kamanda wa Ilala,
Marietha Minangi, alipoulizwa alisema: “Tulipata taarifa tangu jana tukaenda
kumwambia tumpeleke hospitali, lakini akasema anajisikia vizuri. Suala hilo sio
lazima mpaka vyombo vya habari vitusaidie kuuliza, sisi tunajua wajibu
wetu.”
Katika hatua nyingine,
Jeshi la Polisi linamshikilia Ludovick Joseph, mfanyakazi wa blogu ya Mjengwa,
akihuhushwa na tuhuma za kuvamiwa na kupigwa kwa
Kibanda.
Hata hivyo bado kuna utata wa sababu hasa iliyomfanya
Ludovick kukamatwa na polisi.
Habari za kipolisi
zinasema kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa akihusishwa na tukio la kupigwa Kibanda
wakati taarifa zingine zikisema ameunganishwa na Lwakatare akidaiwa kuandaa
mipango ya uhalifu.
.
http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment