TAARIFA YA KAIMU MKUU WA MKOA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO
YA WIKI YA MAJI KITAIFA TAREHE 16-22/2013 MKOANI LINDI.
Ndugu Waandishi wa Habari na Wananchi wote wa Mkoa wa
Lindi;
Napenda
kuwafahamisha kuwa Mkoa wetu umepewa heshima na Wizara ya Maji kuwa Mwenyeji wa
maadhimisho ya 25 ya Wiki ya Maji Kitaifa yatakayo anza tarehe 16 Machi, 2013 na
kufika kilele tarehe 22 Machi, 2013.
Shukrani
Napenda kuishukuru Wizara ya Maji kwa kutupa heshima ya
kuwa wenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya 25 ya Wiki ya
Maji.
Aidha, navishukuru sana Vyombo vya Habari kwa kufika
katika mkutano huu na kuwa tayari kutangaza mafanikio yaliyowekwa katika Sekta
ya Maji.
Naamini maadhimisho haya yatakuwa chachu kwa wadau
mbalimbali kuchangia kwa hali na mali katika ujenzi, uendeshaji na matengenezo
ya miradi ya maji Mkoani wa Lindi.
Utangulizi;
Kila mwaka kuanzia mwaka 1988, Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki ya
Maji kuanzia tarehe 16-22 Machi kwa kuwahusisha wananchi na wadau wote wa maji.
Kilele cha maadhimisho huwa ni tarehe 22 Machi ambayo siku hiyo
inafahamika Kimataifa kuwa ni Siku ya Maji Duniani kwa mujibu wa Azimio Na.
193/47 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Uzinduzi utafanyika tarehe 16 Machi 2013 katika Kijiji cha Mtandi
Wilaya ya Kilwa na Kilele cha Maadhimisho kitakuwa tarehe 22 Machi 2013 katika
Manispaa ya Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu. Mgeni Rasmi katika Kilele cha
Maadhimisho atakuwa ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
JAKAYA MRISHO KIKWETE.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji ya mwaka huu yataongozwa na Kauli Mbiu
isemayo “MWAKA WA USHIRIKIANO WA MAJI KITAIFA”.
Madhumuni ya Maadhimisho;
Madhumuni ya Maadhimisho ya wiki ya maji ni pamoja na:-
Kuwaelimisha wananchi kuhusu Sera ya Maji na majukumu yao katika
kuitekeleza.
Kutathmini maendeleo ya Utekelezaji wa Programu ya Maji, hali ya
huduma ya maji na usafi wa mazingira na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa
huduma na uhifadhi wa rasilimali za Maji.
Kuhamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki katika kupanga,
ujenzi, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji na usafi wa
mazingira.
Kujenga mshikamano miongoni mwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji.
Kutoa ujumbe kwa wadau kuhusu Kauli Mbiu ya Wiki ya Maji na Siku ya
Maji Duniani.
Madhumuni hayo yanalenga kuboresha utoaji wa huduma ya Maji, Usafi
na Uhifadhi wa Mazingira, pamoja na usimamizi na utunzaji wa rasilimali za Maji
nchini (vyanzo vya maji na miundombinu ya kufikisha huduma ya maji kwa
watumiaji).
Maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka 2013;
Maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanaendelea vizuri na
uzinduzi na kilele cha maadhimisho kitawahusisha viongozi wa Kitaifa.
Maadhimisho ya mwaka 2013 yanakusudia kuwashirikisha wananchi
katika:-
kupanga, kujenga, kuendesha na kufanyia matengenezo miradi ya maji na
kuimarisha usafi wa mazingira,
kutunza vyanzo vya maji na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi
endelevu ya rasilimali za maji.
Matukio haya yataenda sambamba na kutoa ujumbe (maudhui) wa Siku ya
Maji Duniani ya mwaka 2013 ambao ni “MWAKA WA USHIRIKIANO WA MAJI
KITAIFA”.
Shughuli zitakazofanyika katika Wiki ya Maji hapa Mkoani Lindi ni
pamoja na:-
Kuzindua miradi 3 ya Maji vijijini ambayo ujenzi wake
umekamilika.
Vijiji hivyo ni Mtandi (Wilaya ya Kilwa), Rondo Mnara (Halmashauri ya
Wilaya ya Lindi) na Luchelegwa (Wilaya ya Ruangwa).
Miradi hii imetekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Maji na wadau mbalimbali.
Kuzindua Mradi wa Uboreshaji Huduma ya Maji katika Mji
wa Lindi kutoka chanzo kilichopo katika eneo la Kijiji cha
Sinde.
Kutakuwa na Mikutano ya Hadhara maeneo yote ya
Uzinduzi
Miradi yote itakayozinduliwa itawanufaisha wananchi
wapatao 134,108.
Kugharamia Maadhimisho;
Ili kuweza kugharamia maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka 2013, Wadau
mbalimbali wameombwa kutoa michango ya hali na mali ili kufanikisha maadhimisho
haya.
Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Maji yanagharimiwa na Wizara ya
Maji , Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mamlaka za Maji Safi na Maji taka nchini,
Halmashauri, Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Kiserikali na yasiyo ya
Kiserikali na Watumiaji Maji.
Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wadau wote kutoa michango ya hali
na mali ili kuweza kufanikisha maadhimisho haya ya Wiki ya Maji Kitaifa
yatakayofanyika hapa Mkoani kwetu mwaka huu wa 2013.
Wito kwa Wananchi wa Lindi;
Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kuwapokea na kuwakaribusha
wageni wote ambao watakafika Mkoani kwetu kwa nyakati mbalimbali katika
Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani. Kipekee ninawaomba Wananchi/Wakazi wa
Manispaa ya Lindi kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania atakapowasili tarehe 21 Machi, 2013 na kuendelea kuwa nae mpaka siku ya
Kilele cha Maadhimisho katika Uwanja wa Ilulu tarehe 22 Machi, 2013.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
|
Post a Comment