Na Anna Nkinda – aliyekuwa Magu
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amekipongeza kituo cha utamaduni cha Bujora kwa kutunza na kuhifadhi utamaduni wa mtanzania unaolitambulisha kabila la wasukuma jambo litakalosaidia kizazi kijacho kuweza kujifunza utamaduni huo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alitoa pongezi hizo hivi karibuni alipokitembelea kituo hicho kilichopo wilayani Magu katika mkoa wa Mwanza.
Alisema kuwa kituo hicho kimeonyesha mfano wa kuigwa kwani amejionea na kujifunza mambo mbalimbali ambayo hakuwa anayafahamu hapo awali kuhusiana na kabila hilo jambo la muhimu wahakikishe kuwa wanaendelea kutunza utamaduni wao.
“Kazi mnayoifanya ni nzuri na inatakiwa kuigwa na watu wengine, hakika kwa kufanya hivi mtarithisha utamaduni wenu kutoka kizazi kimoja hadi kingine, watoto wenu wanatakiwa kujua mila zao kwani mtu asiye na utamaduni ni mtumwa”, alisema Mama Kikwete .
Akisoma taarifa ya kituo hicho Padre Fabian Mhoja ambaye ni Mkurugezi alisema kuwa kituo kilianza mwaka 1954 kikiwa na lengo la kuhifadhi na kuendeleza tunu bora ya maisha ya watu ili waweze kumfahamu Mungu na kuishi kadiri ya mpango wake kwa kutumia utamaduni.
Alisema kuwa wanajihusisha na shughuli za kutunza na kuendeleza urithi wa utamaduni wa mtanzania kwani kupitia kituo hicho wameweza kutangaza utalii na utamaduni ndani na nje ya nchi kupitia ngoma , nyimbo na michezo mbalimbali.
Kituo hicho kimekuwa kikiandaa tamasha la Bulabo ambapo Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amekuwa akichangia ufanikishaji wa tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka na kukusanya watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi
Post a Comment