Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MAPENDEKEZO YA CHAMA CHA NATIONAL CONVENTION FOR CONSTRUCTION AND REFORM – MAGEUZI (NCCR- MAGEUZI) KUHUSU HATUA ZA DHARURA ZA KUOKOA ELIMU YA TANZANIA

images
MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
DK. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
Kwa heshima kubwa, Chama cha NCCR-Mageuzi kinapenda kuwasilisha rasmi mapendekezo yake kwako yenye lengo la kuinusuru elimu ya Watanzania, kama ifuatavyo:
Utangulizi
Mheshimiwa Rais,
Sisi Chama cha NCCR-Mageuzi tumeguswa sana na hali isiyoridhisha ya ubora wa elimu katika Taifa letu la Tanzania. Hivyo tunaona ipo haja ya kuchukuliwa kwa hatua za dharura kuinusuru elimu, ili taifa lisiharibikiwe zaidi, badala yake kuwe na elimu yenye ubora wa hali ya juu na utimilifu wa malengo tuliyonayo kama taifa.
Mheshimiwa Rais,
Katika muktadha wa mapendekezo tunayoyaleta kwako, tunazingatia masuala ya kitaifa yafuatayo:-
(i) Tangu Taifa letu lipate uhuru wake mwaka 1961 (kwa Tanganyika) na mwaka 1964 (Mapinduzi ya Zanzibar) tulitambua umuhimu wa kufuta ujinga, kwa kuelimisha wananchi ili tujiletee maendeleo. Ingawa hadi sasa kazi kubwa imefanyika katika kukuza elimu hapa nchini, bado hatujafika katika hali ya kuwa na taifa ambalo karibu kila raia mwenye umri stahiki anajua kusoma na kuandika.
(ii) Katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, tunataja pamoja na mambo mengine kwamba, ifikapo mwaka 2025 tuwe tumejenga taifa la watu walioelimika kwa upeo wa juu katika nyanja mbalimbali.
(iii) Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambao una malengo nane ya milenia; lengo la pili likiwa ni upatikanaji wa elimu bora kwa wote (achieving universal primary education)); na
(iv) Ifikapo mwaka 2015 (takribani miaka miwili toka sasa) tutalazimika kama taifa kupima utekelezaji wa malengo hayo ya milenia ili kuendana na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Rais,
Wakati tukikabiliwa na malengo hayo ya Kitaifa, kwa muda mrefu kumekuwepo na viashiria vingi vinavyoonesha kwamba ubora wa elimu itolewayo hapa nchini katika ngazi zote hauridhishi. Viashiria hivyo ni pamoja na:-

    1. Matokeo ya hivi karibuni ya mitihani ya kidato cha nne nchini yanayoonesha kuendelea kushuka kwa viwango vya ufaulu wa wanafunzi, na wengi wao kutofaulu mitihani hiyo;
    2. Taarifa mbalimbali zimeonesha kuwa wanafunzi wengi wanaohitimu elimu ya msingi na kujiunga na elimu ya sekondari wana uwezo mdogo katika stadi za kusoma na kuandika na wengine hawawezi kabisa kusoma wala kuandika;
    3. Shule nyingi za umma zinakuwa na matokeo mabaya ya mitihani zikilinganishwa na matokeo ya shule zinazomilikiwa na watu binafsi au mashirika yasiyo ya kiserikali; na
    4. Tanzania tunashika nafasi ya ngapi kielimu katika Afrika Mashariki?
Athari za Udhaifu wa Elimu Kwa Taifa
Mheshimiwa Rais,
Athari za udhaifu katika elimu itolewayo nchini zinajidhihirisha katika sura mbalimbali, miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-
  1. Kumong’onyoka kwa mila, desturi na utamaduni wa jamii ya Watanzania;
  2. Kuporomoka kwa uadilifu miongoni mwa watumishi wa umma na kada nyinginezo na hivyo ongezeko la ufisadi na rushwa;
  3. Kuporomoka kwa uwajibikaji;
  4. Kuporomoka kwa kiwango cha utii wa Sheria na Kanuni mbalimbali;
  5. Kutokuthamini Rasilimali za taifa;
  6. Tabia ya watanzania wengi kutothamini matumizi ya muda;
  7. Kupungua kwa uzalendo kwa baadhi ya wananchi;
  8. Kutojiamini kwa baadhi Watanzania wanaohitimu elimu katika ngazi mbalimbali; na
  9. Ukosefu wa nidhamu ya matumizi ya tekinolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), mfano matumizi ya simu nururu (mobile phones) na mitandao ya kijamii wakati wa kazi bila kuzingatia umakini kwenye kazi mtu anoyafanya.
Mheshimiwa Rais,
Vile vile udhaifu ulioko katika elimu ndio hatimaye unaosababisha uwepo wa matatizo yafuatayo:-
  1. Kuporomoka kwa viwango vya huduma zitolewazo katika sekta mbalimbali;
  2. Kuporomoka kwa viwango na ubora wa bidhaa, majengo, na miundombinu;
  3. Kuporomoka kwa viwango vya uzalishaji wa bidhaa mashambani na viwandani;
  4. Uharibifu na uchafuzi wa mazingira;
  5. Udhaifu katika kukabiliana na majanga mbalimbali kama vile mafuriko na tetemeko la ardhi;
  6. Udhaifu katika kuzuia na kudhibiti ajali zinazoweza kuzuilika, kama vile ajali za vyombo vya usafiri, moto na milipuko ya silaha;
  7. Udhaifu katika kukabiliana na hatari za kiafya kwa binadamu na wanyama zitokanazo na uchimbaji migodini na usafirishaji au uhifadhi wa kemikali; na
  8. Migomo ya watumishi wa umma pamoja na makundi ya kijamii inayojitokeza katika ngazi mbalimbali, vurugu na migogoro katika jamii.
Chimbuko la Tatizo na Hatua Tulizojaribu Kuchukua
Mheshimiwa Rais,
Baada ya tafakari na utafiti wa muda mrefu sasa, NCCR – Mageuzi tumebaini kuwa, elimu ya Tanzania imedidimia zaidi kupitia mamlaka zinazoisimamia. Mifano ya matatizo yanayotokana na mamlaka husika ni kama ifuatavyo:
  1. Kukosekana kwa mitaala ya elimu nchini, ilihali ipo taasisi husika kwa ajili ya utengenezaji mitaala. Hili ni tatizo kubwa mno linalowafanya walimu wafundishe wanafunzi bila kuwa na mwongozo wa pamoja na hivyo kuifanya elimu itolewayo itegemee ufahamu wa mwalimu mmoja mmoja.
  1. Ukosefu wa umakini katika kuandaa vitabu vya kiada na ziada kwa ajili ya matumizi ya shule mbalimbali, ilihali ipo taasisi inayoidhinisha matumizi ya vitabu mashuleni. Vitabu vilivyoandaliwa na vinavyotumika kwa sasa vina upungufu mkubwa ya weledi na muongozo.
  1. Mfumo wa mitihani kukosa mwongozo wa kueleweka, japo nchi inacho chombo maalum kwa ajili ya mitihani ya kitaifa. Imefikia hatua wanafunzi wanapimwa uelewa wao kwa maswali ya kuchagua majibu na kubahatisha. Japokuwa mfumo huo ni mzuri kwa usahili na kurahisisha matokeo kutoka kwa wakati, una uwezo mdogo wa kupima uelewa wa mwanafunzi.
  1. Wingi wa masomo kwa wanafunzi wa umri mdogo; wanafunzi wa elimu ya awali wamewekewa kiwango kikubwa cha mzigo wa masomo bila kujali uwezo wao wa ufahamu na kuzingatia umri, pamoja na kwamba wapo wataalam nchini wa mitaala na mafunzo.
Kadhalika, darasa la kwanza (elimu ya msingi) wanaanza kwa kufundishwa masomo manane. Hii inashusha uwezo wa mwanafunzi kutambua mambo ya msingi na hatmaye anajikuta hatambui chochote.
  1. Kukosekana kwa waalimu wenye weledi kwenye baadhi ya masomo katika shule za umma, licha ya kwamba nchi inavyo vyuo mbalimbali vya mafunzo ya ualimu.
  1. Mazingira duni ya kazi yameshusha kwa kiwango kikubwa ari ya kufanya kazi miongoni mwa walimu; na
  1. Mfumo uliopo umeshindwa kufanya ufuatiliaji na kubaini matatizo ya elimu katika ngazi mbalimbali za elimu kwa nchi nzima, licha ya kwamba taifa linao wakaguzi wa elimu.
Mheshimiwa Rais,
Sisi NCCR-Mageuzi, kwa kutambua tatizo lililopo tumejaribu kupitia kwa wawakilishi wetu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulishirikisha Bunge katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili. Bahati mbaya jitihada zetu kupitia huko hazikufanikiwa.
Mheshimwa Rais,
Katika bunge la 10 kikao cha 4 cha tarehe 31/1/2013 Bunge lilijadili hoja
iliyotolewa na Mheshimiwa James Francis Mbatia (Mbunge wa kuteuliwa na Rais) kama hoja binafsi, kwa kuzingatia taratibu kama inavyoainishwa na Kanuni za kudumu za Bunge; Kanuni ya 62(1) (e) na Kanuni ya 62(2). Hoja hiyo ilihusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini. Katika hoja hiyo, Mbunge alifafanua kuwa udhaifu uliomo katika sekta ya Elimu, chimbuko lake hasa (kwa muhtasari) ni mambo yafuatayo;
  • Uwepo wa sera ya elimu iliyopitwa na wakati; sera hiyo japo imetungwa zamani (1995) inaendelea kutumika bila mabadiliko;
  • Kukosekana kwa andiko rasmi la mitaala nchini;
  • Hitilafu nyingi zilizomo katika mihtasari ya masomo; na
  • Vitabu vitumikavyo mashuleni kuwa na viwango duni.
Mheshimiwa Rais,
Bahati mbaya, mjadala uliofanyika Bungeni kuhusiana na hoja hiyo ulihitimishwa na Mheshimiwa Spika bila ya kuwa na muongozo unaoeleweka wa namna ya kuokoa elimu ya Tanzania.
Mheshimiwa Rais,
Baada ya juhudi hizo kutofanikiwa Bungeni, kwa heshima tunakuja kwako tukiwa na matumaini kwamba mamlaka yako yanatambua tatizo lililopo na yataona mantiki katika mapendekezo tuliyonayo.
Hivyo, Chama cha NCCR– Mageuzi kwa heshima kinakuomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulifanyie kazi tatizo lililopo kwa kuchukua hatua sahihi na za haraka ili kuinusuru elimu ya watanzania.
Mapendekezo ya NCCR–Mageuzi Kuhusu Hatua za Kuchukua
Mheshimiwa Rais,
Kwa dhati kabisa, Chama cha NCCR- Mageuzi kinapendekeza kufanyika kwa yafuatayo ili kuliondolea taifa tatizo tajwa:-
(A) Kuundwa Tume ya Kudumu ya Elimu Nchini
Mheshimiwa Rais,
Tunapendekeza kwamba, iundwe TUME ya Kudumu ya Elimu Nchini, itakayoshughulikia pamoja na mambo mengine kuhakikisha ubora wa Elimu nchini na kudhibiti mambo yote yanayoweza kusababisha kutetereka kwa ubora huo (Education Quality Assurance and Control). Tume hii iwe na mamlaka ya kuhakiki utendaji wa Taasisi mbalimbali za elimu ambazo hadi sasa zimeonekana kutotimiza vyema majukumu yake.
Tunaamini kwamba, Tume itakapoundwa inaweza vilevile kusaidia kubainisha wazi ni nini falsafa na malengo hasa ya utoaji wa elimu nchini kulingana na wakati tulionao. Hili halitakuwa suala geni sana katika nchi yetu, kwani wakati wa awamu ya kwanza ya serikali ya Tanzania huru, Uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliwahi kutunga falsafa na miongozo mbalimbali za elimu iliyowekiweka wazi malengo mahsusi ya elimu. Malengo hayo yaliweza kutekelezeka na tukapata Watanzania wenye elimu bora kwa kipindi fulani. Tatizo lilianza baada ya kuwa na mabadiliko mbalimbali katika masomo yanayofundishwa kwenye shule zetu, bila kuzingatia falsafa husika, kiasi kwamba mwelekeo wa elimu uliyumbishwa. Tunapendekeza kuwa Tume hii uiundwe kwa mamlaka uliyo nayo kikatiba, na isingojee kupatikana kwa Katiba mpya kwa kuwa jambo hili ni la haraka, na nyeti kitaifa.
Mheshimiwa Rais,
Ni matumaini yetu kwamba kwa mamlaka yako uliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, na kwa kadri utakavyoona inafaa, utaunda Tume tunayoipendekeza na kuipatia majukumu ya utendaji (Hadidu za rejea) stahiki.
Kwa uwazi zaidi, tunapendekeza Tume husika ipewe mamlaka na majukumu yafuatayo ya msingi:-
  1. Kusimamia na kuendesha shughuli za kudhibiti viwango vya elimu itolewayo hapa nchini. Hili litadhibiti pamoja na mambo mengine, kuwepo kwa utitiri wa shule nyingi ambazo hazina viwango au hazizingatii ubora wa elimu.
  1. Kuidhinisha mtaala wa elimu wa kudumu wa Tanzania, na kutoa idhini juu ya matumizi ya mitaala mingine (katika shule zitakazokubaliwa kufanya hivyo) kwa ajili ya elimu ya awali hadi vyuo vya ualimu, na kuidhinisha mabadiliko pale inapobidi.
  1. Kuhariri na kupitia vitabu vya kiada (editing and reviewing) vinavyotumiwa na shule za Tanzania.
  1. Kufanya tafiti za kisayansi kuhusiana na masuala mbalimbali ya elimu kwa lengo la kuinua ubora wa elimu nchini.
  1. Kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na/au wadau wa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya elimu nchini.
  1. Kufanya maamuzi juu ya masuala ya msingi ya elimu, kama vile suala la lugha ya kufundishia katika ngazi mbalimbali za elimu. Hapa tunarejea mjadala wa muda mrefu juu ya lugha ya kufundishia nchini, hadhi ya kiswahili chetu, na nafasi ya Tanzania katika ushirikiano wa kimataifa.
  1. Kushirikiana na vyama vya walimu, jamii na asasi za kijamii pamoja na idara za serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya kitaifa katika elimu.
  1. Kupendekeza kwa serikali, viwango vya vyeo, mishahara na marupurupu ya waalimu na watumishi wengine katika sekta ya elimu katika ngazi ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu nchini. Jukumu hili ni kama lile ambalo Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) inalo. Tume tunayoipendekeza ni kwa ajili ya Elimu ya Msingi,Sekondari na Ualimu [Tanzania Commission for Basic, Secondary and Teacher Education]
  1. Kuishauri serikali juu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu
  1. Kuwasilisha taarifa za utendaji wake kazi kila mwaka mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  1. Kuandaa na kutoa taarifa za maendeleo ya kielimu nchini. Taarifa za Tume ziwe wazi kwa wananchi ili kuweza kutumiwa kama vielelezo kwenye nyanja mbalimbali za elimu. Hii ni tofauti na Taarifa ya kirasimu ya utendaji kazi.
Kuwajibika moja kwa moja kwa Mheshimiwa Rais ili kuhakikisha ubora wa viwango vya elimu itolewayo nchini.
(B) Kuimarishwa kwa Huduma za Ukaguzi wa Elimu
Tunapendekeza kuwa huduma za wakaguzi na wasimamizi wa shule ziboreshwe na nyenzo kwa ajili ya kazi hiyo ziongezwe ili kudhibiti uwajibikaji.
(C) Serikali ikutane na Walimu
Aidha, tunapendekeza kuwa Serikali ifanye mazungumzo na walimu yenye lengo la kujadiliana nao ni nini hasa wangependa kuona kinawekwa sawa ili udhaifu uliomo katika mchakato wa ufundishaji na kujifunza kwa wanafunzi shuleni uweze kuondolewa.
(8)Hatua za dharura kwa matokeo ya kidato cha nne 2012
Mheshimiwa Rais,
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 ni janga la kitaifa. Hatuwezi kufumbia macho kuangamia kwa vijana wetu zaidi ya 240,000 ambao walipata daraja la sifuri mwaka jana. Wapo wamelinganisha tukio hili na kifo kwa vijana hawa. Tunakusihi sana Mheshimiwa Rais utumie mamlaka yako kuwaokoa vijana wetu, utoe agizo warejeshwe shuleni waanze upya kidato cha tatu au hata cha nne kama utaona inafaa. Hii ndiyo njia pekee ya kuwaokoa na matumaini yetu ni kwamba kwa busara yako utaona hilo linafaa.
TUNAOMBA KUWASILISHA.
Ndimi mtumishi mtiifu,
James Francis Mbatia (Mb)
MWENYEKITI WA TAIFA
LEO TAREHE ………… MWEZI WA ………………………… 2013
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top