Na: Patricia Kimelemeta na
Fidelis Butahe, Mwananchi
Mwenyekiti wa Chama cha
NCCR-Mageuzi, James Mbatia amejitoa kwenye Tume ya serikali kuchunguza chanzo
cha kushuka kwa kiwango cha kustisha cha matokeo ya kidato cha nne, iliyoundwa
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Mbatia ambaye ametajwa kuwa mmoja wa wajumbe wa
tume hiyo yenye wajumbe 15, alisema kamwe hatoweza kufanya kazi yake kwa uhuru
kwa sababu ni Mbunge wa kuteuliwa, kamati hiyo
imeundwa na serikali
hivyo lazima kutakuwa na mgongano wa maslahi.
Hatua hiyo imekuja siku
tatu baada ya chama hicho kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete, kikimuomba
aunde tume ya kudumu ya elimu nchini.
Tume hiyo iliundwa
kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne, watahiniwa 240,903
kati ya 480,036 waliofanya mtihani walipata alama sifuri, huku 23,520 sawa na
asilimia 5.16 wakifaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wakipata
daraja la nne.
Januari 31, mwaka huu
katika kikao cha bunge, Mbatia aliwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu katika
sekta ya elimu akielezea kwa kina, sera ya elimu iliyopitwa na wakati,
kukosekana kwa mitalaa, kuwapo kwa mihtasari mibovu ya masomo na vitabu kuwa na
viwango duni.
Hata hivyo, wabunge wa
CCM wakishirikiana na Serikali walimaliza hoja hiyo bila kutolewa majibu ya
msingi.
Mbatia alisema jana kuwa
hawezi kufanya kazi yake kwa ufanisi ndani ya tume hiyo, kwa sababu ndiye
aliwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu sekta ya elimu, hoja ambayo
ilizimwa bila kutolewa majibu ya msingi.
“Kamati ya Waziri mkuu
haina jipya la kufanya kwa sababu ipo Kamati iliyoundwa mwaka 2011 kuchunguza
matokeo mabaya ya kidato cha nne, imeeleza kila kitu na ripoti ipo ofisi ya
waziri mkuu, sasa hii ya sasa inakwenda kuchunguza nini?” alihoji
Mbatia.
Post a Comment