Na: Godfrey Kahango,
Mbeya
Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Mbeya imewanasa walimu wawili wa Shule ya
Sekondari ya Forest kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya kati ya Sh500
na Sh1,000 kwa wanafunzi wanaochelewa asubuhi. Imeelezwa kwamba kutokana na
mtindo huo, walimu hao wamekuwa wakijikusanyia wastani wa Sh150,000 kwa siku.
Walimu hao walikamatwa saa 8.30 mchana jana shuleni hapo baada ya baadhi ya
wanafunzi kutoa taarifa Takukuru za kuwapo kwa tabia hiyo ya kulazimishwa kutoa
fedha wanapokuwa wamechelewa kufika shuleni asubuhi. Kamanda wa Takukuru wa Mkoa
wa Mbeya, Daniel Mtuka, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kwamba
walimu hao
(majina tunayo),
walitiwa mbaroni wakati wakiwatoza wanafunzi hao fedha hizo.
Hadi wanakamatwa, walimu
hao walikutwa na kiasi cha Sh64,000 walizokuwa wamezikusanya kutoka kwa
wanafunzi hao, huku pembeni kukiwa na rundo la fimbo lililokuwa likitumika
kuwachapa.
Mtuka alisema waligundua
kuwa walimu hao walikuwa wanatengeneza kiasi cha 150,000 kwa siku kutokana na
wastani wa wanafunzi 300 waliokuwa wanawachapa. Shule hiyo ina wanafunzi
900.
“Walimu hao wamekuwa na
mradi huo wa kuwalipisha wanafunzi na wanaoshindwa kulipa walikuwa wanachapwa
viboko visivyokuwa na idadi,” alisema na kuongeza:
“Kwanza walimu hao
walikuwa wanachukua majina ya wanafunzi waliochelewa kutoka kwa walimu walioko
zamu na kuanza kuwaita kwenye chumba walichokuwa wanakiita ‘Gwantanamo’ na
kutoza fedha hizo.”
Walimu hao walichukua
jina hilo kutoka Kambi ya Guantanamo Bay iliyoko karibu na Kisiwa cha Cuba,
ambako Marekani imeweka kambi ya kijeshi.
Kambi
hiyo ilianzishwa Januari, 2002 wakati Marekani ikiwa chini ya George Bush kwa
ajili ya kuhifadhi mateka wa kivita kutoka Afghanistan na
Iraq.
Kwa nyakati
tofauti, wanafunzi walisimulia vituko vya walimu
hao.
Mwanafunzi wa kidato cha
kwanza, (jina tunalihifadhi), alisema kuwa mwanafunzi ambaye alikuwa hana fedha
za kuwapatia, alikuwa anaambiwa kuweka kichwa chini, miguu na miguu juu kisha
mwalimu huyo anamchapa kwenye makalio hadi sehemu unapopita uti wa
mgongo.
“Baada ya kuona vitendo
hivyo vinaendelea, huku uongozi wa shule ukiwa umekaa kimya, tukaamua kuwaambia
viongozi wa serikali ya wanafunzi na ndiyo waliokwenda Takukuru,”
alisema.
Post a Comment