HATUA ya vyombo vya habari kulivalia njuga suala la
kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom
Kibanda haiwafurahishi watendaji wa serikali.
Vyombo kadhaa
vya habari yakiwemo magazeti, vimekuwa na habari, makala na maoni mfululizo
kuisukuma serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi iwasake na kuwafikisha
mahakamani wahusika wa tukio la Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa
Kampuni ya New Habari (2006).
Katika habari
hizo, vyombo hivyo vinaeleza kushangazwa na kitendo cha Jeshi la Polisi
kushughulikia matukio mepesi haraka na kwa kutumia nguvu nyingi, huku sakata la
Kibanda na lile la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka
uchunguzi wake ukidorora.
Msukumo huo wa
vyombo vya habari kuvisakama vyombo vya dola na baadhi ya vigogo serikali
kuhusika na matukio hayo umepokelewa kwa mtazamo hasi.
Katika mkakati
huo, tayari gazeti la Mtanzania limeandikiwa barua na Msajili wa Magazeti ambapo
Kaimu Mhariri wake anatakiwa kwenda kujieleza Idara ya Habari (Maelezo) kuhusu
habari iliyochapishwa Machi 20, mwaka huu.
Akithibitisha
kupokea wito huo, Mhariri wa Mtanzania, Kulwa Karedia, alisema barua hiyo ina
kumb. Na. IR/RN/336/57 ya Machi 21 mwaka huu, na imesainiwa na Jamal Zuberi kwa
niaba ya Msajili wa Magazeti.
Alisema kuwa
Kaimu Mhariri wao anajulishwa, “Madhumuni
ya wito huo ni kujadili habari iliyochapishwa na gazeti lako toleo Na.7262 yenye
kichwa cha Urais wa damu.”
Karedia alisema
kuwa habari husika iliyoandikwa na Mtanzania ilielezea kuwa sakata la
kushambuliwa kwa Kibanda limeanza kuibua tetesi na kutaka Waziri wa Mambo ya
Nje, Bernard Membe ahojiwe kutokana na kauli yake.
Membe alihojiwa
na kituo cha televisheni cha ITV Julai mwaka jana, katika kipindi cha Dakika 45
na kudai kuwa anao maadui 11 wakiwemo waandishi wa habari wawili ambao
atawatwanga kweupe.
Hatua ya kutaka
Membe ahojiwe ni kutokana na Kibanda kuumizwa ikiwa ni takribani miezi tisa
tangu kauli hiyo itolewe bila kufafanua maadui zake aliwakusudia akina
nani.
Hata hivyo
gazeti hili lilidokezwa kuwa baadhi ya vigogo waandamizi wa serikali, CCM na
maofisa kadhaa wa Usalama wa Taifa wamekuwa na vikao vya kujadili namna ya
kunyamazisha magazeti hayo.
Lengo la mkakati
huo ni kuhamisha mjadala ili wananchi wahangaike na mambo mengine wasahau sakata
la kuteswa kwa Kibanda.
Miongoni mwa
wanaohaha katika suala hili ni waziri mmoja machachari ambaye anatajwa kuusaka
urais kwa nguvu akishirikiana na kigogo mwingine wa CCM.
Inadaiwa kuwa
kumekuwa na vikao vya mfululizo ambapo vya mara ya mwisho vimefanyika juzi kwa
siku mbili ofisini na nyumbani kwa waziri huyo jijini Dar es Salaam kujadili
mkakati wao.
Miongoni mwa
walioshiriki vikao hivyo yumo pia kigogo mmoja wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo.
Baadhi ya mambo
waliyojadili ni kuyafungia baadhi ya magazeti, hasa Tanzania Daima na Mtanzania,
ambayo wamesema yanafuatilia na kuripoti sana habari za masaibu yaliyompata
Kibanda.
Hata hivyo,
baada ya mjadala mrefu walikubaliana kwamba ni rahisi kuanza na Mtanzania kwa
sababu za kimkakati na kisiasa.
Kwa sababu
zao za kimkakati walikubaliana kuanza na Mtanzania na kuliacha Tanzania Daima
ambalo linamilikiwa na kiongozi wa upinzani.
Hatua hiyo
ilifikiwa baada ya kujiridhisha kwamba mchakato wa kuvishitaki vyombo hivyo
unaweza kuchukua muda mrefu na kuibua masuala mengine wasiyotaka jamii
iyajue.
Vigogo hao
walienda mbali zaidi wakimhusisha Ofisa Mkuu Mtendaji wa New Habari (2006),
Hussein Bashe wakidai amekuwa akitumia magazeti ya Rai na Mtanzania kuelekeza
yaandike masuala yanayochafua serikali, waziri mmoja na kundi lake na makundi
kadhaa ndani ya CCM.
Ingawa suala
la uraia wa Bashe lilishamalizika kwa Idara ya Uhamiaji kuuthibitisha, mipango
ya kundi hili sasa imejielekeza katika kuibua upya suala hilo kisiasa ndani ya
chama kwa kumtumia kijana machachari na bingwa wa propaganda ambaye ana wadhifa
mkubwa ndani ya chama.
Taarifa
zinasema suala hilo litaibuliwa ndani ya vikao vikuu vya chama vijavyo ili CCM
iendelee kusisitiza haitambui uraia wake na iweke shinikizo afukuzwe
uanachama.
Vile vile
waliweka mkakati kuwa shinikizo hilo litapelekwa hadi kwa mwajiri wa Bashe,
Rostam Aziz ili amwondoe kwenye cheo hicho au amfukuze kazi kwa sababu magazeti
yake yamekuwa hayatimizi malengo asilia yaliyomsukuma
kuyanunua.
Bashe
ashangaa
Alipotafutwa
Bashe jana kueleza kama ana taarifa za mikakati ya kikao hicho, alijibu kwa
kifupi; “Sijazipata taarifa hizo ila
nitazifanyia kazi.”
Bashe alikiri
kupokea barua ya Msajili wa Magazeti ikiwataka wafike kujieleza Jumatatu mchana,
lakini akaongeza; “Hilo suala la uraia
wangu kama kweli wanaendelea nalo watakuwa wanajisumbua
bure.”
Nape
ang’aka
Katibu wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnuye, alipoulizwa kama
anafahamu ama ameshiriki vikao hivyo vya mikakati ya kuyanyamazisha magazeti
hayo, aling’aka na kusema CCM hawana matatizo na Tanzania Daima wala
Mtanzania.
“Hicho kikao
kinafanyikaje? Mimi ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, huyo waziri anashughulika na
wizara yake halafu huyo mtu wa Maelezo ana idara yake,” alisema.
Nape alidai
hajawahi kuonana na waziri mtajwa kwa muda mrefu na kwamba hata hajui kama
amerudi nchini tangu walipokutana nchini Afrika Kusini wiki kadhaa
zilizopita.
“CCM kama chama
hatuna matatizo na Tanzania Daima wala Mtanzania, hizo ni fitina zenu mnataka
kutengeneza, vyombo hivi tunashirikiana vizuri hata niliwahi kutembelea ofisi
zao baada ya kuteuliwa na hata kwenye ziara zetu mikoani tunavichukua,” alisema.
Waziri tajwa
na kigogo mmoja wa Maelezo hawakupokea simu zao kutoa ufafanuzi hata
walipoandikiwa ujumbe mfupi wa simu (sms) hawakujibu.
Sakata la
kutekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya kwa Kibanda linafananishwa na lile la Dk.
Ulimboka kwani hadi sasa uchunguzi wa kuwasaka waliohusika unafanyika
kimzaha.
Tangu
alipoumizwa Dk. Ulimboka Juni 26 mwaka jana, ni mtuhumiwa mmoja pekee
amefikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika na tukio hilo ingawa inaelezwa kuwa
alikuwa amerukwa na akili akajipeleka kanisani na kudai
kuhusika.
Zikiwa sasa
ni wiki tatu tangu kujeruhiwa kwa Kibanda, hakuna mtuhumiwa hata mmoja
aliyekamatwa na vyombo vya dola kuhusiana na tukio hilo, ingawa ndani ya wiki
moja Jeshi la Polisi limekamata na kumchunguza Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama
wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kisha kumfikisha mahakamani akidaiwa kujihusisha
na ugaini kwa kutumia usahidi wa video.
CHANZO:
TANZANIA DAIMA
Post a Comment