Na Frank John -
Maelezo
Watumishi wa umma wametakiwa kuwa
mfano wa kuigwa katika kutekeleza
majukumu yao kwa mujibu wa taaluma zao hasa katika kitengo cha manunuzi ili
sekta binafsi ziweze kujifunza kutoka kwao.
Wito huo umetolewa
jana na Kamishna
wa Idara ya Manunuzi ya Umma kutoka
wizara ya Fedha Dk. Fredrick Mwakibinga
katika kongamano la kujadili rasimu ya sera ya manunuzi lililofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa JB uliopo jijini Dar es
Salaam.
Dk Mwakibinga pia aliwataka
Maafisa ugavi, wananchi na wadau mbalimbali
kutoa maoni yao juu ya rasimu ya Sera ya
manunuzi ya Umma ili waweze kufanikisha zoezi la
mchakato wa uundwaji wa sera hiyo.
Alisema kuwa kupatikana kwa
sera nzuri na ya kisasa ya manunuzi ya umma ambayo ni muongozo wa Serikali
katika sekta hiyo, kutaisaidia Serikali kutimiza nia na malengo
ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
“Tunayo mambo mengi ya
kuangalia kama Serikali ili kuboresha sekta hii, ikiwa ni pamoja na kuangalia
miundo ya Idara za ugavi, idadi ya watumishi na kuwajengea uwezo wagavi ili
waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi”, alisema Dk.
Mwakibinga.
Alizitaja njia
zitakazotumika katika utoaji wa maoni ili kuboresha rasimu hiyo kuwa ni
baruapepe, nukushi, barua na kupitia vyombo vya habari kama magazeti ambapo
mwananchi atachangia kitu anachohitaji kiwepo
kwenye rasimu hiyo.
Alimalizia kwa kusema kuwa
baadhi ya mambo ambayo Serikali inahitaji kuyaangalia ni minundo ya Idara za
Ugavi, idadi ya watumishi na kuwajengea uwezo wagavi ili waweze kutekeleza
majukumu yake ipasavyo.
Akitoa mada katika kongamano hili
Prof. Gaspar Munishi
kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala alisema kuwa kuna umuhimu wa kuboresha
rasimu ya Sera ya manunuzi kwani inayotumika sasa
ni ya zamani na haikidhi mahitaji yaliyopo.
Prof. Munishi pia alishauri
kuwa ni lazima sera ya manunuzi iendane na sheria na taratibu za Serikali na
uhusiano wa kimataifa kati yake na washirika wa maendeleo ili kuweza kutimiza
sheria zilizopo.
Akichangia mada katika
kongamano hilo Emmanuel Maliganya
ambaye ni Afisa Ugavi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, alitoa
wito kwa wadau mbalimbali kulipa uzito jambo hilo na kuweza kutoa maoni yao ili
yawezeshe kupatikana kwa sera
bora.
Alitaka suala la rushwa
liainishwe katika sera ya manunuzi ya umma ili wale wote wanaoshiriki katika
vitendo vya rushwa ndani ya mchakato wa manunuzi ya Serikali bila afisa ugavi
kuhusika, wawajibishwe.
Kongamano hilo la siku
moja liliandaliwa na
Idara ya Sera ya manunuzi ya umma na kuhudhuliwa na wajumbe mbalimbali kutoka ofisi
za Serikali na Taasisi
binafsi
Post a Comment