Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu amewataka wanawake nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo zinazojitokeza katika maeneo yao ili waweze kujikwamua kiuchumi na kupambana na umaskini.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es salaam wakati akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika machi 7 mwaka huu.
Amesema maadhimisho hayo yanalenga kuwezesha upimaji wa utekelezaji wa maazimio , matamko, mikataba na itifiki mbalimbali za kimataifa na kikanda zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia kwa wanawake na kubainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kauli mbiu isemayo Uelewa wa Masuala ya Jinsia katika Jamii; Ongeza kasi“
Amesema serikali ya Tanzania imekuwa na mipango thabiti ya kuhakikisha kuwa usawa wa kijinsia nchini unazingatiwa kwa kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kuridhia na kusaini mikataba, itifaki, maazimio na matamko mbalimbali yanayohusu maendeleo, haki na ustawi wa wanawake na utungaji wa sheria ya Ardhi Na. 4 na ile ya vijiji Na.5 za mwaka 1999 ambazo zinatoa fursa sawa za umiliki wa ardhi.
Bi Ummy amefafanua kuwa kuwa Tanzania imeshasaini na kuridhia mkataba wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW 1979), Azimio la ulingo wa Beijing (1995), mkataba wa malengo ya Milenia, Azimio la kuleta Usawa wa Kijinsia katika nchi za Afrika (2004) na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu za Wanawake (2006).
Mikataba mingine iliyosainiwa na kuridhiwa na Tanzania ni ule wa Itifaki ya Maendeleo ya Jinsia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC 2008).
Ameeleza kuwa serikali imepitisha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000 ili kutoa mwongozo wa kuratibu uingizwaji wa masuala ya jinsia katika mipango, Sera, Programu, mikakati na bajeti za kisekta ili kuleta usawa baina ya wanawake na wanaume katika masuala ya maendeleo nchini.
Pia amefafanua kuwa Wizara yake imeratibu kuanzishwa kwa dawati la jinsia katika Wizara, Idara za serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini ili kuharakisha utekelezaji wa masuala ya jinsia.
Kuhusu mafanikio ya kuleta usawa wa kijinsia nchini Bi. Ummy ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi zikiwemo uwakilishi wa wanawake bungeni kutoka asilimia 30 mwaka 2005 na kufikia 36 mwaka 2010.
“Napenda kueleza kuwa mafanikio haya kwa wanawake katika ngazi za maamuzi nchini ni makubwa kwa sasa ukilinganisha na miaka iliyopita, sasa tuna mawaziri wanawake, tuna wakuu wa mikoa na wilaya , tuna wabunge wengi tu , Majaji wa mahakama kuu, makatibu wakuu na viongozi wengi wanawake” amesema.
Aidha amefafanua kuwa serikali imeendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi na tayari imeratibu na kusimamia mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) na kuongeza kuwa wanawake wamewezeshwa kiuchumi kwa kuwapatia elimu, mbinu za ujasiriamali na mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya Wanawake Tanzania ambapo mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa wanawake 5270 na wanaume 1157.
Ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana bado wanawake nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa uwepo wa wasichana wanaokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni na kuwepo kwa vtendo vya ukatili wa kijinsia katika baadhi ya jamii nchini.
Post a Comment