Utangulizi
Wapendwa waandishi wa habari. Tunaomba kupitia ninyi
tuweze kuongea na watanzania wenzetu kuhusu hali ya amani ilivyo nchini mwetu
kufuatia kila aina ya dalili ya watanzania kukosa uvumilivu wa kidini.
Tunatambua kuwa serikali yetu imefanya mambo mazuri mengi tu nchini, hilo hatuna
mashaka nalo; hata hivyo kama watanzania tunadhani kuna baadhi ya mambo hayaendi
sawa. Hivyo basi, tunaomba kuchukua nafasi hii kuelezea wasiwasi wetu kuhusu
migogoro hii ya kidini inayozidi kukua nchini.
Migogoro hii ilianza kuvuka kama moshi lakini sasa
inaanza kulipuka na kusambaa zaidi. Tumeshuhudia uchomaji moto wa kanisa kule
Mbagala, kumwagiwa tindikali shekhe mmoja kule Zanzibar na Shekhe mwingine
kuuawawa, kuchomwa makanisa Zanzibar, kupigwa risasi viongozi wa kikristo kule
Zanzibar na pia mgogoro wa kuchinja huko Geita ambako tumeshuhudia mchungaji
mmoja akiuawa.
Mbali na hayo, kuna matukio kadhaa kwenye shule zetu za
sekondari yakihusisha migogoro ya kidini kati ya wakristo na waislamu. Haya
tumeshahudia yakitokea sekondari za Bagamoyo, Ndanda, Kibiti, Ilboru na
kwingineko. Pia yapo malalamiko yasiyo rasmi kuhusu udini kwenye sehemu za kazi
na kwenye taasisi mbalimbali za serikali. Wapo wanaodai kuwa baadhi ya taasisi
binafsi, za kidini na hata za serikali zinazohudumia watanzania wengi zimekuwa
zikiajiri wafanyakazi kwa misingi ya kupendelea dini fulani fulani. Jambo hili
hata kama ni la kuzungumzwa tu, ni vema likafanyiwa kazi maana hisia hizi
zikipanuka hujenga chuki na kusababisha watanzania wasielewane.
Sisi wanajumuiya ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam tunaamini, kama taifa, kuna mahali tumechepuka na kuacha misingi
tuliyoachiwa na Baba wa Taifa katika ujenzi wa taifa imara na lenye umoja. Kuna
sababu kadhaa zilizotufikisha hapa tulipo, nazo ni:
- Wanasiasa na watanzania wengi tunafuata dini zetu kwa hisia zaidi pasipo kufikiri kwa kina kuhusu yale tunayoyafanya. Tumesahau kabisa kuwa dini ni kwaajili ya kutuhusianisha na ulimwengu ujao tusioujua. Tunapaswa kumheshimu na kumthamini kila binadamu aliyeko hapa duniani. Kwa bahati mbaya baadhi yetu tunadhani kuwa ulimwengu huu umeumbwa kwaajili ya dini fulani na binadamu wengine hawana haki ya kufurahia maisha yao hapa duniani. Tunataka kutumia dini zetu kumiliki utawala wa dunia hii.
Dini zetu zimekuwa mtaji kwa baadhi ya wanasiasa na
vyama vyao. Inasikitisha kuwa hakuna jitihada za kutosha zilizofanyika kuzuia
wanasiasa kutumia dini kama sera au ajenda ya katika kupata kura. Baadhi ya
wanasiasa wameingia madarakani kwa kutumia udini na ukabila na hivyo hali
inapofikia watanzania kuanza kuchukiana kwa misingi ya dini wanakosa nguvu na
ujasiri wa kukemea na kuzuia haya kwakuwa nao wamepitia njia hiyo.
- Sababu ya pili ni kwamba hivi sasa umaskini nchini umekuwa wa kiwango cha juu. Kila mtu anatafuta jawabu la umaskini wake kwa kudhani kuwa umesababishwa na mfumo ulio nje ya maisha yake na ya serikali. Katika hali hii wamejitokeza watanzania wenzetu wanaotafuta majibu mepesi kwa kusingizia kuwa wamekuwa maskini kwasababu ya dini nyingine. Hali hii imesababishwa na ukosefu wa elimu kiasi kwamba watanzania wengi wanashindwa kuwa na uwezo wa kuchambua mambo kimantiki na badala yake wanaamini bila kuchuja lolote wanaloambiwa na viongozi wa dini au mwanasiasa au mwanaharakati. Ni vema watanzania wakajua kuwa ajenda ya udini si ya dini fulani bali ni ya makundi machache ndani ya taasisi zetu za dini. Tusibebeshe lawama za udini kwa dini fulani bali tuelewe kuwa udini umekuwa ni mtazamo ya watu wachache ndani ya dini zetu.
- Tatu, watanzania tumeanza kupoteza uelewa kuhusu madui wetu wa asili ambao ni ujinga, umaskini na maradhi, na tumeongeza adui mwingine ambaye ni imani ya mwingine. Tumeacha kuelekeza nguvu zetu katika kupambana na maadui hao watatu na tunaelekeza nguvu zetu kupambana na dini nyingine ambazo kimsingi haziwezi kuwa sababu ya matatizo yetu ya kila siku.
Kwa bahati mbaya tunashindwa kuelewa kuwa dini hizi kuu
mbili za kikristo na kiislamu ni dini zilizozaliwa sehemu mmoja baadaye
zikasambaa sehemu tofauti na kuchukua utamaduni tofauti. Hatimaye tunachokiona
sasa, ndugu wa ukoo na hata kabila moja waliotokana na historia moja, utamaduni
mmoja na lugha moja wamefanywa maadui kwasababu wanafuata dini tofauti.
- Jambo la nne, nchi yetu imeruhusu uhuru wa kuanzisha taasisi za dini pasipo kuwa na usimamizi wa karibu. Taasisi nyingi za kidini zimeibuka nchini na zimekuwa chanzo kikubwa cha kuwagawa watanzania kwa misingi ya kidini. Umoja wetu unapotea kwasababu baadhi ya taasisi za kidini zilizopo zinawagawanya watanzania kwa misingi ya dini. Taasisi nyingi za dini zinafundisha mbinu na namna ya kuwakabili waumini wa dini nyingine badala ya kuhimiza upendo na mshikamano miongoni mwa watanzania.
Baadhi ya viongozi wa taasisi hizo wamewafanya
watanzania mtaji wao kwa kuwachochea wafuasi wao kuwachukia wengine kwa lengo la
kutimiza haja zao binafsi. Watanzania tunapaswa kuzinduka na kuchukua tahadhari
dhidi ya watu wanaotuchonganisha. Tukumbuke kuwa kiongozi wa dini anayekuambia
kuwa dini fulani ni ya kishenzi na wafuasi wake ni wa kishenzi basi mtu huyo si
mtumishi wa Mungu bali anatumikia maslahi yake.
Tufanyeje?
Baada ya kueleza sababu zilizotufanya tufikie hapa
tulipo sasa, sisi wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tunapendekeza
mambo yafuatayo:
- Serikali isimamie na kudhibiti vyombo vya habari vya kidini vinavyochochea chuki za kidini. Inasikitisha kuwa serikali iliyosheheni wataalamu wa kila aina inashindwa kutambua madhara ya uchochezi wa vyombo vya habari. Watanzania tunapaswa kujifunza kuwa hata mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda hayakuanza siku moja, yalichochewa na vyombo vya habari kwa muda mrefu na vyombo hivyo vilihamasisha pia mauaji hayo.
Hata hapa nchini kwetu, serikali isipokuwa tayari
kukemea na kufungia vyombo vya habari vinavyotumia udini kuleta uchochezi, ipo
siku watanzania watauana sana na nchi itapoteza heshima yake ya kuwa taifa la
amani na tutakuwa wakimbizi. Tunaishangaa serikali inaweza kuyafungia magazeti
yanayoikosoa lakini haiko tayari kuyafungia magazeti yanawachochea watanzania.
Tungependa ujasiri unaotumika na vyombo vya ulinzi na
usalama kuwakamata wanaoandika ujumbe wa vitisho kwa viongozi wa kisiasa nchini
utumike pia kuwakamata wanaochochea uvunjifu wa amani. Kama tunaweza kuwalinda
viongozi dhidi ya vitisho kwa maisha yao binafsi kwanini tushindwe kulilinda
taifa letu kwa kutumia nguvu hizo hizo za kuwatumikia
wanasiasa?
- Pia tunatoa wito kwa wanasiasa na watanzania kwa ujumla kuwakataa wale wanaotafuta vyeo mahali popote pale, iwe kwenye vyama vya siasa au taasisi, kwa kutumia udini kama kigezo cha kutaka kuchaguliwa. Ni wakati muafaka sasa kuhuisha yale yote yatakayoleta mtangamano wa kitaifa. Kama taifa tumeacha misingi mizuri ya ujenzi wa taifa tuliloachiwa na waasisi wa taifa hili.
- Jambo jingine ni kuhamasisha na kusimamia sera ya elimu sawa kwa wote. Elimu yetu ya sasa imejenga matabaka makubwa miongoni mwa watanzania na matokeo yake matabaka haya yanajitokeza zaidi katika sura ya udini. Kutokana na hali hii watanzania wengi waliokosa elimu wanadhani kuwa wenzao wa dini nyingine wanafanikiwa kwasababu ya upendeleo wa kidini. Kwa kusisitiza katika elimu, itakuwa rahisi kwa watanzania kuelimishwa kuwa chuki za kidini si msingi wa dini zetu tofauti na ilivyo sasa ambapo ukosefu wa elimu unawafanya wengi kuwa waathirika wa mafundisho potofu.
- Pia tunaisihi serikali iwachunguze viongozi wa baadhi ya taasisi za kidini zinazowahamasiha wafuasi wake kufanya vitendo vya uhalifu. Ni vigumu sana kuwadhibiti wafuasi wa taasisi ya kidini ambao wameshakuwa na nguvu ya kuungana na kufanya jambo lolote baya. Tuna wasiwasi kuwa baadhi ya viongozi wa taasisi hizo wanatumika na watu wa nje kuvuruga amani yetu. Kwa bahati mbaya viongozi hawa wanajua wazi kuwa amani ikivurugika nchini wao wanazo sehemu za kukimbilia wakati ndugu zetu wakiendelea kuuana.
Wito wetu kwa watanzania wenzetu ni kwamba wajue kuwa
viongozi wa kidini wanaowachochea kuwachukia wengine hawana nia njema na taifa
na maisha yao. Watatuacha tukiliangamiza taifa huku wao wakiwa salama. Ni vema
watanzania wakajua kuwa sababu ya umaskini na matatizo ya kimaisha
hayajasababishwa na waumini wa dini nyingine bali mfumo wetu mbovu wa utawala
unaoacha kukua kwa matabaka ya kijamii. Tukishirikiana sote kupambana na
umaskini hakutakuwa na sababu ya kuchukiana. Pia, ni muhimu sasa, kila dini
iendeshe maswala yake bila kutaka kubebwa na serikali.
Asanteni sana
Post a Comment