Mkaguzi wa dawa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati, Dkt.Engelbert Mbekenga, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya msako unaoendelea wa kukamata bidhaa zilizokwisha muda wake wa kutumika na zile zilizopigwa marufuku kutumiwa. Hivi karibuni mamlaka hiyo iliteketeza bidhaa zilizoisha muda wake na zile zenye sumu za thamani ya zaidi ya silingi milioni 7.1 zilizokamatwa wilaya ya Iramba na Singida vijijini. (Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati, imeteketeza bidhaa mbalimbali ikiwemo vipodozi vyenye viambato vya sumu, zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 7.1.
Bidhaa zingine zilizoteketezwa ni pamoja na vyakula na vinywaji vilivyokwisha muda wake wa kutumika na zile zenye ubora hafifu.
Hayo yamesemwa na Mkaguzi wa TFDA Kanda ya Kati Dkt. Englibert Mbekenga, muda mfupi baada ya kuteketeza bidhaa hizo katika mji wa Old Kiomboi, wilaya ya Iramba mkoa wa Singida.
Amesema bidhaa hizo wamezikamata wakati wa ukaguzi ulioanzia wilaya ya Singida vijijini Machi 4 hadi 10 na katika wilaya ya Iramba, ulioanza Machi 11 na kumalizika 16 mwaka huu.
Amesema lengo la ukaguzi huo ni kuangalia hali ya majengo, usafi, hali ya usajili na vibali kutoka mamlaka ya chakula na dawa, pamoja na hali ya ubora wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.
Kuhusu bidhaa hizo, Dkt. Mbekenga amesema kuwa vipodozi vyenye viambato vya sumu vyenye uzito wa tani 0.16 vimekamatwa kwenye msako huo endelevu, na thamani yake ni zaidi ya Sh.3.2 milioni.
Amesema pia tani 0.15 za vyakula ambavyo muda wake wa kutumika umeisha, vimekamatwa na kuviteketeza na thamani yake ni zaidi Sh. laki sita na vile vile vinywaji vyenye uzito wa lita 701 vimeteketezwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mbekenga ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha wananchi kuwa makini wakati wanafanya manunuzi ya bidhaaa mbali mbali.
Amesisitiza kuwa mwananchi asipokuwa makini, kuna uwezekano mkubwa akanunua sumu ambayo itaenda kumuuawa taratibu, kwa hiyo ni lazima kuwe na umakini, soma maelezo ya bidhaa, angalia muda wake wa kutumika na ubora wake.
Mkaguzi huyo pia amewaonya wafanyabiashara wanaowakimbia wakaguzi wa TFDA, kuwa arobaini yao ipo karibu, na kuwa dawa pekee ya wafanyabiashara ni kuwa rafiki wazuri wa TFDA, ni kuwa waadilifuna wanaoheshimu maisha ya watu.
Post a Comment