
Na Emmanuel J. Shilatu
Mara baada ya kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu na nyonyaji za kikoloni na hatimaye tulifanikiwa pia kuyaunganisha Mataifa haya mawili yaani
Sio hayo tu pia tumejaliwa uwepo wa ardhi iliyojaa rutuba pamoja na madini ya kila aina ambapo ukitaka almasi utaipata
Mwenyezi Mungu bado hakuchoka kuendelea kutubariki sisi Watanzania ambapo pia ametuneemesha mbuga mbalimbali za wanyama. Baadhi ya mbuga hizo ni Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Mikumi na kadha wa kadha.
Pia tumejaliwa vivutio vya kitalii mbalimbali lakini kikubwa ni kuwa tumejaliwa uwepo wa Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mkubwa na mrefu kuliko yote barani Afrika. Mungu atupe nini tena cha zaidi?
Nchi yetu hii ya Tanzania ina ukubwa wa zaidi ya hekari 940,000 yenye mikoa 26 ambapo mikoa 21 ipo Tanzania Bara (Tanganyika) na mikoa 5 ipo Tanzania Visiwani (Zanzibar). Pia kuna wilaya zaidi ya 126 hapa nchini kwetu Tanzania.
Tanzania ina wakazi zaidi ya watu milioni 40 ambapo ndani yake kuna makabila zaidi ya 120 lakini hakuna mtu anayejaalisha kabila, rangi wala dini ya mtu ama mwenzake.
Mara baada ya kupata uhuru, Watanzania tulikuwa na kazi moja tu kubwa ya kupambana na maadui zetu. Nguvu zetu, akili zetu, umoja na mshikamano wetu ulielekezwa kwenye kupambana na maadui zetu watatu ambao ni “Ujinga”, “Maradhi”, na “Umaskini”.
Kila Mtanzania alitakiwa na anatakiwa kuwa mstari wa mbele kwenye kupigana kiume na maadui zetu hawa. Lengo kuu la kuanzishwa kwa mapambano haya ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na Taifa imara ambalo watu wake walio wengi wana elimu ya kukidhi kiwango, watu hao hao wawe na afya bora, lakini kubwa wawe na mapato ya kutosha yenye matumizi ya kuridhisha. Hiyo ndio Tanzania inayotakiwa kuwa.
Nilifurahi kuona kuwa wakati tunaanza mbio za mapambano hayo tulikuwa pamoja wenye umoja, mshikamano, upendo, ushirikiano na nia moja ya dhati. Lakini ghafla waliibuka wasaliti na kuamua kuishia njiani kutokana na sababu zao wanazozijua wao wenyewe.
Ni zaidi ya miaka 51 sasa imepita tangu tupate Uhuru wetu ambapo maendeleo yetu yanazidi kusonga mbele lakini ni kwa kusuasua zaidi. Kusuasua huku kunaweza kuwa kumesababishwa labda na mfumo wa vyama vingi; au kumesababishwa na Watanzania kuridhika mapema na kuamua kujibweteka; ama umri wetu mkubwa tangu tupate Uhuru wetu (miaka 51); au elimu kubwa ama duni tuliyonayo na mambo mengineyo kadha wa kadha.
Lakini kikubwa ambacho kinaonekana ni kujikita na hata kuota mizizi zaidi ni ile dhana nzima ya kibaguzi iliyojengeka akilini, fikrani ama kwenye tazamo za watu ama baadhi ya watu. Dhana hii ya kibaguzi imejikita ndani ya mtazamo wa neno “Serikali”.
Jamii yetu imekuwa na fikra duni, mawazo potofu ndani ya Serikali kati Viongozi na Wananchi kwenye suala zima la kimaendeleo. Jamii (sisi Raia) tumeamua kujenga dhana ya kuwa kufanya hivi na vile ni jukumu la Serikali huku wao (jamii) ambao ndio Wananchi wenyewe wakijitenga ndani ya Serikali bila hata kujua maana nzima ya Serikali na kina nani wanahusika ndani ya Serikali ama Serikali inaundwa na kina nani.
Ni kweli kabisa kwamba Serikali ni chombo cha utawala kilichoshika dola ama nchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo Wananchi. Na wanaoiwezesha Serikali kushika dola ni Wananchi (watu). Bila ya watu hakuna Serikali na hivyo Serikali haiweze kuwepo bila ya kuwepo na watu. Hivyo watu , jamii ama Raia ni sehemu ndani ya Serikali.
Sio Watu (Wananchi) wa kawaida yaani mimi, wewe, na yule pekee wanaounda Serikali. Kundi jingine ndani ya Serikali ni viongozi. Hivyo Serikali inaundwa ama ni muunganiko kati ya Viongozi na Wananchi. Ni dhambi kubwa kuwatenganisha makundi haya (watu, viongozi) katika chungu hiki (Serikali).
Inasikitisha sana, inahuzunisha sana na hata kushangaza sana kuona ni kwa namna gani sisi jamii tunapowaachia viongozi ama kundi la watu Fulani walisukume peke yao gurudumu letu la maendeleo. Kwa jinsi Watanzania tunavyoishi utadhani tunawangojea watu fulani kutoka nje ili waje kutujengea nchi yetu. Yatupasa tutambue ya kwamba ni jukumu letu kujiletea maendeleo yetu wenyewe na wala tusiwe Watumwa wa kufikiria au hata kuwangojea Wahisani waje watufanyie.
Tusiishie kuwalaumu tu Viongozi kila kukicha huku tukisahau jinsi sisi tulivyo wavivu sana wa kupindukia. Watanzania tulio wengi hatupendi kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu. Watanzania tulio wengi hatupendi njia nyoofu na sahihi badala yake tunapenda njia ya mkato ya kujipatia vipato vyetu. Watanzania wengi tunapenda sana kufanya madili, ama “michongo” kama wanavyoita watoto wa mjini.
Kwenye salaam zao ama maongezi mengi ya Watanzania ni nadra sana kukosa kusikia maneno kama vile “mambo mengine niaje, ishu vipi ama madili yakoje”. Ni dhahiri kuwa hapa inatafutwa njia ya mkato katika maisha. Hali hii huzaa matokeo endelevu mabovu ndani ya jamii kama vile utapeli; ujambazi; ongezeko la mihadarati na madawa ya kulevya; mauaji ya maalbino na vikongwe; pamoja na uchafu ama uozo mwingine kadha wa kadha unaofanana na huo.
Chanzo haswa cha uwepo wa utafutaji mambo kwa njia ya mkato halijasababishwa na Viongozi ndani ya Serikali bali msingi wake mkuu ni Watu tulio wengi kutaka matokeo chanya yenye faida na matunda kwa haraka na hata pia kukata tama ya kimaisha kwa haraka zaidi kutokana na kujinyima fursa ya uvumilivu na ustahimilifu ndani yetu.
Kuna usemi mmoja unaosema “Wanaofanikiwa zaidi ni wale walioshindwa mara nyingi” Je utashindwaje, kama hujajaribu mara nyingi? Je mafanikio katika maisha yanapatikana kwa mara moja tu? Haya ni maswali muhimu nay a msingi sana kwa Watanzania, kujiuliza.
Ifike mahali tujitambue ya kwamba kelele, tuhuma, lawama, dharau kwa viongozi wetu hazitatusaidia endapo sisi kwa sisi hatujaamua kujibidisha ipasavyo. Utakuta ndani ya jamii fulani tupo zaidi ya watu laki mbili lakini tunamtegemea kiongozi mmoja awe ni Mbunge ama Diwani ili aweze kutuletea maendeleo. Endapo sisi tulio wengi tumeshindwa kuwa kitu kimoja wenye nia moja ya umoja, mshikamano na tukaamua kwa dhati kujiletea maendeleo; Je, kiongozi mmoja pekee atawezaje?
Ndugu zangu, kwanini alaumiwe dobi kutakasa kaniki wakati tunajua rangi ya kaniki? Ni lazima tutambue ya kwamba sisi raia pia tunahusika vilivyo na huu umaskini wetu na si vyema kuwasukumizia mzigo wote wa lawama viongozi wetu pekee. Watanzania tulio wengi tunapoteza muda mwingi kwa kukaa vijiweni, kushabikia siasa tu, kupiga soga na kucheza bao muda wote. Je, tukiamua kujishughulisha kwa kuutumia muda huo ipasavyo tungekuwa wapi kimaendeleo hivi sasa?
Waswahili walisema usimuhadithie mtu ndoto yako uliyoota jana usiku lakini hapa ni kinyume kwani siri tunasema na bayana tunaambizana. Binafsi huwa Napata ukakasi pindi nionapo Serikali ina sera na majukumu lukuki lakini Watanzania tulio wengi hatushiriki vyema na hata hatutimizi wajibu wetu kwa wakati. Je, kwa uwajibikaji huu, maisha bora kwa kila Mtanzania yatapatikana kweli?
Mara nyingi sera tulizonazo zinategemea zaidi umoja, mshikamano, ushirikiano na nia ya dhati ya uwajibikaji wa pamoja ndipo ziweze kutekelezwa. Kamwe maisha bora kwa kila Mtanzania hayaji kwa kuota au kupiga soga ama kwa kungojea mpaka uone Tanzania (nchi yako) imekufanyia nini na badala yake ujiulize wewe umeifanyia nini Tanzania?
Kuna wanamapinduzi, wanaharakati na watu mashuhuri wengi tu hapa Duniani ambao hawakungoja mpaka waone nchi zao zimewafanyia nini na badala yake walijiuliza wamezifanyia nini nchi zao?
Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela, Martin Luther King Jnr, Kwame Nkurumah, Chifu Mkwawa ni baadhi tu ya Wanaharakati na wakombozi wa kweli dhidi ya Uhuru na ubaguzi wa ngozi nyeusi ambao milele na milele watabakia kuwa ni mashujaa maarufu wa ulimwengu. Jiulize mwenyewe wewe je utakumbukwa, ama tutajivunia nini kutoka kwako? Je, ni kwa huo ugoigoi wako ama kwa uwajibikaji wako?
Tuache uvivu na tujitume vilivyo kwa kuchangamkia fursa na Baraka tulizojaaliwa. Mungu ametujaalia wingi wa ardhi yenye rutuba ifaayo kwa kilimo, misitu, wanyama pori na vyanzo vingi vya kujiletea maendeleo. Ndugu zangu mmezitumia vipi fursa na Baraka tulizojaaliwa kwa manufaa yako na kwa Taifa lako?
Kila siku tunasikia ajali zikitokea ambapo huacha simanzi kubwa ya vifo vya wapendwa wetu, wengine wakisababishiwa ulemavu wa milele, ongezeko la yatima na watoto wa mitaani. Lakini athari kubwa inalikumba Taifa kwa kupoteza nguvu na rasilimali kubwa ya uzalishaji mali.
Ajali hizi husababishwa na mwendo kasi; dereva kuendesha akiwa amelewa; ukiukwaji wa taratibu za sheria na usalama barabarani; uchakavu wa gari ambapo mengine hutumia vipuri chakavu ambavyo huegeshwa kwa kufungwa na kamba ya mkonge au mgomba; na mambo mengineyo kadha wa kadha.
Pindi unapoona dalili sababishi za ajali, wewe kama ni abiria, dereva, mwana usalama barabarani au mdau wa usalama umeifanyia nini Taifa kwenye kuokoa uhai na usalama wa raia wake?
Mazingira ni vitu vyote ambavyo vimemzunguka mwanadamu vinavyohusisha ardhi, mabonde, milima, misitu, vyanzo vya maji. Mazingira ni uhai. Mazingira safi yaliyotunzwa hutuepusha na magonjwa; hutuletea mvua; hurutubisha ardhi, hutuletea mazao mengi ya chakula na biashara; huzuia mmomonyoko wa ardhi na hata hutupunguzia hali ya joto Duniani.
Lakini wapo baadhi ya watu ambao kwa makusudi kabisa huamua kuharibu mazingira yetu kwa kukata miti hovyo bila ya kupanda miti mingine, wengine huchoma moto ardhi na misitu yetu, pia wapo ambao huchafua mazingira kwa kutupa takataka ovyo ovyo. Wote hawa ni waharibifu wa mazingira ukiwa kama Mwanajamii umeifanyia nini Serikali na Taifa lako kwenye hakikisho la uhifadhi na utunzaji wa mazingira?
Serikali zote zinazoshika madaraka nchini hujitahidi kweli kwenye ujenzi na uboreshaji wa miundo mbinu. Miundo mbinu huhusisha barabara, bandari, reli, madaraja, mifereji ya kupitishia maji machafu n.k. Lakini sisi jamii tumekuwa ndio watu wa kwanza kuililia na ikija huwa ni wa kwanza pia kuiharibu miundombinu iliyojengwa na kuboreshwa vyema na Serikali.
Tumeigeuza mifereji yetu barabarani kuwa ndio “dustbin” za kutupa takataka zetu; mifuniko ya “chambers” tumekuwa tuking’oa; mataruma ya reli tumekuwa tukiiba na kwenda kuiuza kama chuma chakavu. Sisi wanajamii tuna matatizo kweli kweli. Ukiwa kama Mwana jamii umeifanyia nini Taifa lako kwenye utunzaji wa miundo mbinu tuliyonayo?
Hayo ni baadhi tu ya masuala ambayo unaweza ukajiuliza umeifanyia nini Taifa lako? Jukumu la kujenga Taifa hili lipo mikononi mwetu kwani Serikali hii ni yetu na sisi raia tu sehemu ya Serikali. Hivyo Serikali ni jumuisho la viongozi na raia wake (Wananchi).
Jamii inapaswa itambue ya kwamba kila ambacho kinafanywa na Serikali za CCM si kwa ajili ya wana CCM pekee bali huwanufaisha watu wote. Mathalani barabara zilizojengwa hazitumiwi na wana CCM pekee bali watu wote hutumia; huduma za kijamii hutunufaisha sote na si tu wana CCM peke yao na ndio maana huduma kama za Elimu, Umeme, Maji, Afya, hutumiwa na watu wote bila ya kuangalia itikadi, dini wala kabila la mtu.
Serikali zetu (ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) hazibagui inakuwaje sisi raia tunabagua kwa kuvizia mpaka tuone Tanzania imekufanyia nini, na badala ya kujiuliza umeifanyia nini Tanzania?
Ndugu zangu, Tanzania bila Ukimwi inawezekana; Tanzania yenye huduma bora zaidi za kijamii inawezekana; Hakika Tanzania yenye maisha bora zaidi pia inawezekana. Hii itawezekana tu endapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu ipasavyo kwake na kwa Taifa lake. Naomba kutoa hoja.
Mwandishi wa makala hii Anapatikana kwa simu namba: 0717 – 488 622.
Post a Comment