WAZAZI
wa Kata ya Saranga wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam wameitaka
serikali kumuondoa haraka Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Saranga
kwa madai kuwa hana sifa za uwalimu, vyeti vyake vinaonesha kuwa ana taaluma ya uuguzi.
Akizungumza na wandishi wa
habari jijini jana, Diwani wa Kata hiyo, Efraim Kinyafu (Chadema),
alisema wazazi hao pia walikuwa wakishangazwa na shule hiyo kuendeshwa
bila ya kuwa na Kamati kwa kipindi cha miaka minne huku mwalimu huyo
akikwepa kukutana na viongozi mbalimbali walipotaka kukutana naye.
Alisema uamuzi huo, ulitokana na
matokeo mabaya kitaaluma katika shule hiyo, hali iliyowafanya wazazi
hao kuchunguza uwezo wa mwalimu huyo na kubaini kuwa hakuwa na sifa ya
uwalimu bali aliingia kiujanja ujanja wakati shule hiyo inaanzishwa.
Kinyafu alisema wazazi hao
waliuchukulia ukosefu wa taaluma kwa mwalimu huyo kuwa ni kikwazo cha
maendeleo kitaaluma katika shule hiyo.
Hivyo wazazi hao waliadhimia kwa
pamoja katika mkutano wao wa hadhara kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo, kumuondoa mwalimu huyo na ikiwezekana amrudishe kwenye kazi yake
ya kuhudumia wagonjwa hospitalini.
“Kero nyingine zilizotajwa na
wazazi hao ni kulazimisha michango bila kufuata taratibu za shule
kujichukulia uamuzi wa kuwarudisha nyumbani watoto wanaoshindwa kulipia
tuition na kushindwa kuwaheshimu viongozi wake katika wilaya
hiyo”alisema Kinyafu.
Alisema malalamiko kuhusu
mwalimu huyo yanafahamika kutokana na mawasiliano ya mara kwa mara kati
ya wazazi hao na mkurugenzi kupitia kwa diwani huyo.
Wakazi wa eneo hilo walikuwa na
mkutano wa hadhara uliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo ambapo
mwalimu huyo pamoja na kupewa jukumu la kuwasambaza taarifa kwa wazazi,
alishindwa kuhudhuria bila ya taarifa yoyote.
Post a Comment