Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es Salaam
Baraza la wazee wa mabingwa wa Kombe la Kagame na vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu, klabu ya Yanga ya jijini Dar es salaam, limeumwagia sifa nyingi uongozi wa sasa wa klabu hiyo chini ya mwenyeki wake milionea Yusuf Manji.
Akizungumza kwa furaha nyingi, katibu mkuu wa baraza hilo,mzee Ibrahim Akilimali, amesema baraza hilo linabariki kwa moyo mkunjufu mambo yote mazuri yanayofanywa na mwenyekiti Manji pamoja na baraza la udhamini hususani mpango wa kujenga uwanja wa kisasa unaotarajia kugharimu bilioni 48 za Kitanzania.
“Tulipokuwa tunafanya Mapinduzi na kumshinikiza mwenyekiti wa wakati ule mwanasheria Lyod Nchunga, watu walidhani tunataka madaraka, sisi lengo letu lilikuwa kupata viongozi bora , lakini kwa sasa tumeridhishwa sana na uongozi wa Manji, tunabariki sana”. Alisema Akilimali.
Mzee Akilimali aliongeza kuwa hali ya klabu kwa sasa ni shwari, mipango mizuri inayofanywa na viongozi wake imesababisha baraza la wazee, wanachama na wadau wa klabu hiyo kushikamana zaidi na kuiombea dua njema.
Katibu huyo alisisitiza kuwa mwenendo wa Yanga kwa sasa unatoa picha ya kuwa timu bora zaidi siku za usoni, hivyo umoja huo usivurugwe na kikundi chochote au mtu yeyote , kama itatokea hivyo baraza la wazee litalaani vikali watu hao wenye maslahi binafsi.
“Viongozi wetu wamerudisha amani klabuni kwetu, kama atatokea mtu wa kuvuruga uongozi au wachezaji wetu, tutasimama kidete kukemea ili asitie doa mambo mazuri yanayoendelea kwa sasa”. Alisistiza Mzee Akilimali.
Akizungumzia mwenendo wa timu na benchi la ufundi, Mzee Akilimali, alisifu uwezo wa kocha wa sasa Mholanzi Ernie Brandts ambaye anaonekana kuibadilisha timu kwa kiasi kikubwa, huku akijenga umoja na mshikamano miongoni mwa wachezaji”. Alisema Akilimali.
Hivi karibuni Yanga imeanika mipango yake ya kujenga uwanja wa kisasa utakaogharimu zaidi ya biloni 48 za Kitanzania , na tayari Kampuni ya Beijing Construction ya China imewapelekea ramani tatu za uwanja huo, kilichobaki na kuchagua moja ili ujenzi uanze mara mambo ya fedha yatakapokwenda vizuri.
Endapo Yanga itafanikiwa kujenga uwanja wake, itaepukana na makato yasiyoendana na maandalizi ya mechi pamoja na kuwapunguzia adhaa ya kuhaha huku na kule kutafuta viwanja vya kufanyia mazoezi jijini Dar es salaam.
Post a Comment