KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa kijiji na
kata ya Mkwajuni Wilaya ya Chunya Mkoani hapa wamemzika Mwanakijiji mwenzao
akiwa hai wakimtuhumu kusababisha kifo cha Mkazi mmoja kijijini
hapo.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea Apri 26 mwaka huu
majira ya Saa Nane Mchana katika Kitongoji cha Maweni Makaburini baada ya
Mhanga aliyefahamika kwa jina la Victory Mwachirui(68) kuhudhuria mazishi ya
Pita Barton(28)aliyefariki baada ya kuugua kwa muda
mrefu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Thobias Ismail
amesema marehemu alipatwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu kwa mganga wa jadi
ambaye jina lake halikuweza kujulikana maramoja.
Amesema wakati taratibu za mazishi zikiendelea Ndugu wa
marehemu walidai kuwa kifo cha Marehemu kilisababishwa na Mwachirui ambaye ni
Katekista mstaafu kwa imani za kishirikina.
Ameongeza kuwa wakati kaburi likichimbwa kwa ajili ya
kumzika marehemu ndipo vijana waliokuwa wakichimba waliagiza Wazee wa Mila
wafike makaburini kwa ajili ya kuangalia utaratibu wa mazishi na kukagua ukubwa
wa Kaburi ambalo lilikuwa limekwisha chimbwa.
Kutokana na mwito huo walifika wazee wanne akiwemo Mzee
Mwachirui ambaye walimsisitiza kusogea jirani na kaburi ambapo baada ya kusogea
alipigwa na Sururu kichwani na kuangukia kaburini huku akisindikizwa na
marungu.
Baada ya Mzee huyo kupoteza fahamu Vijana hao walianza
kutandika fito ndani ya kaburi kisha kufukia kwa udongo kiasi kwa lengo la
kutenganisha na Mwili wa Marehemu Pita uliokuwa kwenye jeneza baada ya kuwazika
kwenye kaburi moja.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la mazishi kundi la vijana
lilielekea hadi nyumbani kwa Mzee aliyezikwa akiwa hai na kuiteketeza nyumba
yake huku wakiapa kutotoa siri wakidai Siri ya Jeshi.
Hata hivyo baadhi ya wananchi walitoa taarifa kwa
Mwenyekiti wa Kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Credo Kayanza ambaye pia
alitoa taarifa kwa Diwani wa Kata hiyo Chesco Ngairo ambao kwa pamoja walitoa
taarifa Jeshi la Polisi ambao baada ya taarifa hiyo walifika eneo la tukio huku
wakidhani lililotokea ni kuchomwa kwa nyumba pekee.
Jeshi la Polisi baada ya kufanya upelelezi na kubaini
kitendo hicho waliwaamuru baadhi ya Vijana kufukua kaburi hilo zoezi ambalo
lilifanyika baada ya Vijana hao kulipwa.
Baada ya kufukuliwa kwa kaburi hilo Mwili wa Marehemu
Mzee Mwachirui ulichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Mkwajuni
kwa ajili ya Uchunguzi huku Mwili wa Pita ukizikwa upya
palepale.
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi mwili wa marehemu
ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi ambapo Marehemu alizikwa katika eneo
tofauti na alipokuwa amefukiwa awali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo pia ametoa wito na kuwaasa wananchi
na jamii kuacha tabia ya kuamini mambo ya ushirikina na uchawi kwa madai kuwa
hauna faida kwao bali huchochea migogoro katika jamii
zao.
Aidha ameongeza kuwa wakumbuke kitendo cha kujichukulia
sheria mkononi ni kosa kisheria ambapo pia amewaomba wenye taarifa za walipo
waliohusika na mauaji hayo kuzifikisha polisi haraka ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yao ingawa hakuna aliyekamatwa kuhusika na tukio
hilo.
Picha na E. Kamanga wa Mbeya yetu
|
Post a Comment