Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein
Mwinyi akizungumza na wajumbe wa Baraza la Usajili wa Wataalam wa
Afya ya Mazingira nchini, leo wakati wa uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii Dk. Hussein Mwinyi , akimkabidhi cheti cha usajili wa utaalamu wa afya
ya mazingira, Mary Swai ambaye ni Mwenyekiti mpya wa awamu ya pili ya Baraza
la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini, leo wakati wa uzinduzi
wa baraza hilo jijini Dar es Salaam.
Frank John na Hassan
Silayo- Maelezo
Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii Dk. Hussein Mwinyi amewataka wajumbe wa Baraza la Usajili wa Wataalam wa
Afya ya Mazingira nchini, kufanya kazi kwa kujituma na ushirikiano ili
kupambana na changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuzuia maambukizi ya
magonjwa.
Dk. mwinyi ameyasema hayo
leo wakati wa uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika jana jijini Dar es salaam
ambapo alisema sekta ya afya na ustawi wa jamii inakabiliwa na changamoto
nyingi ikiwemo ongezeko la milipuko ya magonjwa kutokana na uchafuzi wa
mazingira.
Amebainisha kuwa afya ya
mazingira ni suala mtabuka ambalo linahitaji ushirikishwaji wa wadau wa sekta
ya afya ya mazingira ili kutoa matokeo yenye tija na ubora wa hali ya juu
katika kupambana na magonjwa hayo.
Ameongeza kuwa serikali
inatarajia kwamba kwa kutumia baraza hilo huduma ya afya ya jamii itatolewa kwa
wananchi kwa viwango vinavyotakiwa na hivyo, kuboresha maisha ya wananchi kwa
kusimamia na kudhibiti utoaji wa huduma ya afya ya mazingira kwa misingi ya
haki.
“Pia wataalam wa kada hii
watajiendeleza na kufikia kiwango cha juu cha elimu tofauti na miaka iliyopita
ampapo wengi waliridhika na kubaki katika eneo moja kwa muda mrefu na
kusababisha kudumaa kwa taaluma,amesema Dk.Mwinyi.
Amesema kwa kufanya ,
hivyo upo uwezekano mkubwa wa kupunguza ongezeko la kasi ya magonjwa, vifo na
madhara mengine katika jamii yatapungua ikiwa huduma ya afya ya jamii
itaboreshwa.
Naye Mwenyekiti wa baraza
hilo , lililomaliza muda wake Bwana Fabian Magoma alisema linakabiliwa na
changamoto za upungufu wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za baraza
na ukosefu wa mitaala hivyo linahitaji ushirikiano wa karibu na taasisi
zinazoandaa mitaala ya elimu nchini.
Magoma alishauri baraza
hilo, liangalie sheria zinazohusiana na afya ya mazingira, ili waweze kutambua
taaluma hiyo. Huku akiongeza kuwa watu wanaoteuliwa kufanya kazi hiyo wawe ni
wa kada hiyo.
Kwa upande wake mjumbe wa
baraza jipya Haji Mdemu alishauri serikali kuzingatia mbinu za zamani za afya
mazingira , kuzifufua ili kuimarisha afya mazingira na uwajibikaji wa maafisa
afya.
Baraza hilo lilizinduliwa
rasmi mwaka 2009 ikiwa ni matokeo ya sheria ya kusajili wataalam wa afya
mazingira ya mwaka 2007 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania likiwa na majukumu ya kusajili, kudhibiti nidhamu kiutendaji katika
kada ya afya ya mazingira pamoja na kumshauri waziri husika juu ya masuala
yote yahusuyo afya ya mazingira
nchini.
Post a Comment