Wabunge watano wa Chadema
jana walitimuliwa bungeni na kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano kutokana
na vurugu zilizotokea jana usiku.Wabunge hao ni Lissu, Hezekiah Wenje
(Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) Godbless
Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Chanzo za kufukuzwa kwao ni
kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na
Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya
Mbunge wa Iramba
Mashariki, Mwigulu Nchemba.
Kutokana na tafrani hiyo,
Nchemba hakuweza kuhitimisha hotuba yake hivyo Ndugai alilazimika kukatisha
mkutano wa Bunge.Hata hivyo wakati akiahirisha mkutano huo, tayari wabunge hao
walikuwa wameshatolewa nje baada ya askari kuongezwa.
Mapema Mbunge wa Kigoma Mjini
(CCM), Peter Serukamba alitoa tusi zito la nguoni wakati wa hotuba ya Msemaji
Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
licha ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kupiga mkwara wa kuwashughulikia wabunge
watakaorusha matusi.
Mbali na tukio hilo Lema naye
alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu viongozi wa CCM akiwamo Rais Jakaya
Kikwete kwa udini, madai ambayo Bunge limempa siku saba
kuyathibitisha.
Lema aliituhumu CCM
na Serikali yake chini ya Rais Kikwete kwa kushindwa kutatua mgogoro wa kidini
na badala yake kuwa kama analikwepa tatizo. Alionya kuwa Taifa linapasuka kwa
migogoro kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa
kulishughulikia.
Kauli iliwanyanyua vitini
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu na Sera), William
Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Lukuvi na Jaji
Werema walisimama wakidai kuwa Lema alikuwa amemdhihaki Rais Kikwete kwa kauli
zake za kumhusisha na masuala ya udini.
Hata hivyo, Mnadhimu Mkuu wa
Upinzani, Lissu alisimama kumtetea Lema akidai hakuwa amemdhihaki Rais bali
alikuwa amemkosoa kitu ambacho kanuni za Bunge zinaruhusu.
Lema aliruhusiwa
kuendelea na hoja yake na ndipo akamtolea mfano Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira wakati alipokwenda Mwanza kutatua mgogoro
baina ya Wakristo na Waislamu kuhusu suala la
kuchinja.
“Wassira akifahamu yeye
ndiye, Waziri alikwenda Mwanza na kuwaacha viongozi wa dini za Kikristo na
Kiislamu watatue wenyewe suala la kuchinja. Sasa alitaka diwani atatue mgogoro
ule?”
Baada ya kumaliza kuchangia,
Naibu Spika alitangaza kuwa Lema anatakiwa kuwasilisha katika muda wa siku saba
uthibitisho kuwa Rais anahusika na tatizo la udini.
Serukamba
Serukamba
alipewa nafasi ya kutoa taarifa wakati wabunge walipokuwa wakilumbana juu ya
uhalali wa Msemaji wa Upinzani, Profesa Kulikoyela Kahigi kuzungumzia bungeni
masuala yaliyoko mahakamani na shughuli za Idara ya Usalama wa
Taifa.
Wakati akijiandaa kusoma
vifungu vya kukatiza hotuba ya Profesa Kahigi, alitukana tusi zito la nguoni kwa
lugha ya kimombo ambalo kwa sababu za kimaadili hatukuweza kuliandika, kisha
akaendelea kuzungumza huku baadhi ya wabunge wakipigwa
butwaa.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job
Ndugai aliyekuwa akiongoza shughuli za Bunge wakati huo, hakutoa karipio lolote
huku akimruhusu Serukamba kuendelea kwa muda kabla ya kumkatiza na kumruhusu
Mbunge wa Simanjiaro (CCM), Christopher Ole Sendeka kuzungumza.
Ubishi
ulivyoanza
Muda mfupi
kabla ya Profesa Kahigi kuanza kusoma hotuba yake, Serukamba alisimama na kuomba
mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 68(1) akitaka isisomwe kuanzia ukurasa wa
kwanza hadi wa nne kwa kuwa unaingilia uhuru wa Mahakama... “Ni juzi tu Akoonay
(Mustapha, Mbunge wa Mbulu - Chadema), alitukumbusha kwamba mambo hayo ni
‘prejudice’ kwa Mahakama kwa hiyo ukiruhusu hilo Naibu Spika itakuwa ni
ajabu.”
Kabla Naibu Spika
hajatoa mwongozo wake, alimtaka Profesa Kahigi kuzungumza kama anakubaliana na
Serukamba, lakini Profesa Kahigi alisema anaomba kuendelea kusoma hotuba yake
kama ilivyo
Baadaye Mbunge wa
Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba kumpa taarifa Serukamba kwamba katika
kurasa alizozitaja hakuna jambo lolote lililopo mahakamani hivyo aangalie
vizuri.
“Mheshimiwa Naibu Spika
napenda kumpa taarifa mtoa taarifa kwamba hakuna lolote lililopo mahakamani,
ukurasa wa kwanza unazungumzia Idara ya Usalama wa Taifa, haipo mahakamani,
ukurasa wa pili umemtaja Dk Stephen Ulimboka, halipo mahakamani hivyo hakuna
lolote lililopo mahakamani,” alisema.
Baada ya hapo Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama na
kueleza kuwa aliyoyasema Serukamba ni kwamba hotuba hiyo inafanya kesi iliyopo
mahakamani kuwa ya kisiasa akisema... “Kifungu cha 16 cha Sheria ya Usalama wa
Taifa hakiruhusu watumishi wa Usalama wa Taifa kutajwa humu ndani wala
kuchapishwa popote.”
Naibu Spika
alisimama na kusema jambo hilo limeshajitokeza ndani ya Bunge na Akoonay
alishawakumbusha kuwa ni kuingilia Mahakama.
“Jambo hili lilishaleta
kasheshe humu ndani na ruling (uamuzi) ya hili ilishatolewa na Spika, ‘ruling’
yangu ni kwamba kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa nne, mambo ya Dk Ulimboka,
Usalama wa Taifa na Lwakatare.........,” aliishia hapo Ndugai na kuwaruhusu
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Ole Sendeka
kuzungumza.
Mdee alisema ukurasa wa
kwanza mpaka wa tatu wa hotuba hiyo hakuna sehemu jina la Lwakatare lilipotajwa
na kwamba ukurasa wa nne uliotaja jina la Lwakatare hauzungumzii mwenendo wa
kesi... “Hoja anazoleta Lukuvi atusomee hiyo Sheria ya Usalama na atuelezee na
alinganishe na kilichopo hapa.”
Mdee aliungwa mkono na Lissu
aliyesema kuwa sheria anayozungumzia Lukuvi ipo lakini haikatazi kutajwa majina
ya wanausalama ndani ya Bunge... “Ninayo hiyo sheria hapa ya mwaka 1996, haya
maneno kwamba Sheria ya Usalama inakataza masuala ya Usalama wa Taifa kutajwa ni
uchochezi. Hicho kinachoelezwa kukataza ‘disclosure’ (kuwataja) ni huko nje na
si humu ndani.”
Lissu alisema sheria hiyo
inakataza kuchapishwa majina hayo nje ya Bunge na si vinginevyo.
Kairuki alipingana na Lissu akieleza kuwa amepotosha
kwa kuwa sheria hiyo ya Usalama wa Taifa hairuhusu kuwataja watumishi wake bila
kuomba ruhusa kwa waziri.
“Lissu
anapotosha kwa kuwa hairuhusiwi mtu yeyote kuchapisha jina la mtumishi wa
Usalama wa Taifa bila kuomba ruhusa kwa waziri,” alisema Kairuki.Ndipo Naibu
Spika alipompa tena nafasi Serukamba na alipoanza tu kuchangia kuliibuka maneno
ya chinichini ambayo yalionekana kumkera ndipo alipotoa neno hilo
zito.
Baadaye
Ndugai alisema kwa kuwa hilo suala ni la kikanuni, anaiagiza Kamati ya Kanuni
ikutane ili tujadili suala hilo.
Katika hotuba hiyo ambayo awali, waandishi walipata
nakala yake, Profesa Kahigi alikuwa ameandika mambo mbalimbali yanayohusu
kutekwa na kuteswa kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven
Ulimboka na masuala mengine yanayohusiana na kesi ya ugaidi inayomkabili
Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare.
SOURCE:;MWANANCHI
Post a Comment