UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na Taarifa
zilizowasilishwa leo na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati
ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Kamati ya Uchumi, Viwanda na
Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya ndani ya Bunge lako
Tukufu ambazo zimechambua Bajeti ya Mafungu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako
sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali
kwa mwaka 2012/2013 na Mwelekeo kwa mwaka 2013/2014. Vilevile, naliomba Bunge
lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi
zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka
2013/2014.
2. Mheshimiwa
Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi
kubwa anayoifanya kwa maslahi ya Nchi yetu. Mheshimiwa Rais ameiletea Tanzania
sifa, heshima na kuiwezesha kutambulika zaidi Kimataifa katika Nyanja
mbalimbali. Ziara ya kihistoria ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya
Watu wa China aliyoifanya Nchini tarehe 24 hadi 25 Machi 2013 ni ushahidi tosha
wa kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais ya kukuza ushirikiano wenye maslahi ya kiuchumi
kati ya Nchi yetu na Nchi nyingine. Katika ziara hiyo, Mikataba 16 ya
ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ilitiwa saini. Utekelezaji
wa Miradi hiyo utachochea uwekezaji na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na
kupunguza umaskini.
3. Mheshimiwa
Spika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge
waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.
Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania
katika Taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Ni matumaini yangu kwamba
wote walioteuliwa na kuchaguliwa watatumia nafasi hizo kwa manufaa ya Bunge na
kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla. Hongereni
Sana!
4. Mheshimiwa
Spika, niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala inayoongozwa na Mheshimiwa Pindi Hazara
Chana, Mbunge wa Viti Maalum na Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea
Kigwangalla, Mbunge wa Nzega. Nawashukuru pia Wajumbe wa Kamati ya
Uchumi, Viwanda na Biashara inayoongozwa na Mheshimiwa Mahmoud Hassan
Mgimwa, Mbunge waMufindi Kaskazini na Kamati ya Masuala ya UKIMWI na
Dawa za Kulevya inayoongozwa na Mheshimiwa Lediana Mafuru
Mng’ong’o Mbunge wa Viti Maalum. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa
wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Mafungu ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa na Mfuko wa Bunge. Aidha, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za
Bunge lako Tukufu kwa ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka
za Serikali za Mitaa. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha
mjadala wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji
wake.
5. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
mwaka 2012/2013, kumekuwa na majanga na matukio mbalimbali yaliyosababisha vifo,
majeruhi na uharibifu wa mali. Miongoni mwa matukio hayo ni ajali mbaya ya
Jahazi la Sunrise iliyotokea Wangwi katika Bahari ya Hindi mwezi Januari
2013 na ajali mbalimbali za vyombo vingine vya usafiri ambapo watu walipoteza
maisha na wengine kupata majeraha. Hivi karibuni pia tumeshuhudia ajali mbaya
ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 Jijini Dar es Salaam ambalo
limesababisha vifo vya watu 34 na tukio linguine ni vifo 13 vilivyotokana
na kufukiwa na kifusi cha ‘moram’ katika machimbo ya Mushono
Jijini Arusha. Aidha, tumempoteza ghafla Mbunge mwenzetu,Mheshimiwa Salim
Hemed Khamis, Mbunge wa Chambani na baadhi yetu tumepoteza Ndugu,
wakiwemo wazazi na watoto kutokana na sababu mbalimbali.Wote nawapa Pole
Sana!
MZUNGUKO MPYA WA BAJETI
6. Mheshimiwa
Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014,
tumekubaliana kuanza Mzunguko Mpya wa Bajeti ambao utatuwezesha kukamilisha
mjadala wa Bajeti ya Serikali mapema. Lengo ni kwamba ifikapo tarehe 30 Juni
ya kila mwaka, taratibu zote za kuandaa, kuchambua na kupitisha Bajeti ya
Serikali ziwe zimekamilika na utekelezaji wa Bajeti kuanza ifikapo tarehe
1 Julai. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo Bajeti ya Serikali ilikuwa
ikijadiliwa na kupitishwa kwanza na kufuatiwa na Bajeti za Kisekta, sasa
makadirio na matumizi ya Wizara yatajadilwa kwanza na hatimaye kuhitimishwa na
majadiliano ya kina ya Bajeti ya Serikali. Moja ya faida kubwa ya utaratibu huu
mpya ni kwamba, mwaka mpya wa fedha unapoanza utekelezaji wa kazi za Serikali
unaanza mara moja. Utaratibu huo utawawezesha Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge
pamoja na Watendaji wa Serikali kurejea katika kazi zao na kusimamia kikamilifu
utekelezaji wa Bajeti na Mpango wa Maendeleo. Kwa kuwa tunaanza kwa mara ya
kwanza kutumia utaratibu huo hazitakosekana dosari chache ambazo zitafanyiwa
kazi kadri tunavyoendelea kuutumia.
Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kutumia fursa hii kutoa maoni na
ushauri utakaosaidia kuboresha Bajeti ya Serikali ili iwe bora zaidi na yenye
maslahi makubwa kwa wananchi wetu.
7. Mheshimiwa
Spika, maandalizi ya Bajeti yamezingatia Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa
Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Awamu ya Pili ya Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea
kuimarisha usimamizi wa rasilimali chache tulizonazo ili kutekeleza Miradi ya
Maendeleo ya Kipaumbele ambayo itachochea ukuaji wa haraka wa
uchumi.
8. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii
kumpongeza sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bwana Ludovick
Utouh, pamoja na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kusimamia rasilimali za Serikali. Matunda ya kazi hii
yameonekana hadi nje ya Nchi na ndiyo maana Ofisi hii sasa imepandishwa hadhi
kutoka Daraja la Kwanza hadi la Tatu kwa vigezo vinavyotumiwa na Muungano wa
Ofisi za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika Bara la Afrika kwa Nchi
zinazotumia Lugha ya Kiingereza.
HALI
YA SIASA
9. Mheshimiwa
Spika, Nchi yetu imepiga hatua ya kuridhisha katika kuimarisha Demokrasia ya
Vyama vingi. Kwa ujumla hali ya kisiasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa
vinaendelea kutekeleza majukumu yake. Idadi ya Vyama vya Siasa vyenye usajili wa
kudumu imefikia 20 baada ya Chama cha Alliance for Democratic
Change (ADC) kupata usajili wa kudumu. Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA)
kilipata usajili wa muda na zoezi la uhakiki wa wanachama linaendelea. Chama
cha Movement for Democratic and Economic Change kilifutwa baada ya kukosa
sifa za kupata usajili wa kudumu.
10. Mheshimiwa
Spika, ili Demokrasia Nchini izidi kuimarika na Wananchi washiriki
kikamilifu kwenye siasa, Viongozi wote wa Vyama vya Siasa wana wajibu mkubwa wa
kuendesha Siasa za kistaarabu zinazozingatia maadili ya Kitanzania na kufuata
Sheria, Kanuni na Taratibu. Wito wangu kwa Vyama vyote ni kuendelea kuvumiliana
na kutohamasisha siasa za chuki au vurugu ambazo zitatugawa na kuhatarisha
Amani, Utulivu na Umoja wetu ambao umewekezwa kwa miaka mingi.Mwenye Macho
haambiwi Tazama. Wote ni mashahidi wa matatizo makubwa ambayo yamezikumba
Nchi zilizoingia katika siasa za chuki na vurugu.
11. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaandaa
mapendekezo ya kufanya mapitio ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na
Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010. Aidha, itaendelea na usajili wa
Vyama vya Siasa, kutoa elimu ya Demokrasia kwa Wananchi na kuboresha Baraza la
Vyama vya Siasa. Hatua hizo zitazidi kuimarisha Demokrasia ya Vyama Vingi
Nchini.
ULINZI
NA USALAMA
HALI YA MIPAKA YA NCHI
12. Mheshimiwa
Spika, kwa ujumla hali ya mipaka ya Nchi yetu ni shwari na Wananchi
wanafanya shughuli zao bila vikwazo. Katika kuimarisha usalama wa mipaka yetu,
Viongozi wa Mikoa ya Kagera, Kigoma, Rukwa na Tanga wamefanya vikao vya ujirani
mwema na wenzao wa Mikoa ya mipakani mwa Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo, Rwanda, Burundi, Zambia na Kenya. Pamoja na hali nzuri ya usalama wa
mipaka yetu, bado tunakabiliwa na changamoto ya Wahamiaji haramu wanaotumia
Nchi yetu kama mapito ya kuelekea Nchi nyingine au kufanya makao Nchini.
Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali inaendesha misako ya kuwabaini,
kuwakamata na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria. Serikali pia, imeendelea
kutoa elimu kwa Wananchi wa Mikoa ya mipakani ili kutoa taarifa za Wahamiaji
haramu. Natoa wito kwa Wananchi wote kushirikiana na Serikali kuwabaini na
kuwafichua wahamiaji haramu na wale wanaowasafirisha ili wachukuliwe hatua
stahiki za Kisheria.
HALI YA UHALIFU NCHINI
13. Mheshimiwa
Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na jamii kupitia dhana ya Ulinzi
Shirikishi inafanya kazi nzuri ya kudhibiti vitendo vya uhalifu Nchini. Jumla ya
makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika Vituo vya Polisi Nchini
yalipungua kutoka 69,678 mwaka 2011 hadi 66,255 mwaka 2012. Katika kipindi cha
Januari hadi Februari 2013 makosa ya jinai yalikuwa 10,548 ikilinganishwa na
makosa 10,989 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Jeshi la
Polisi pia limedhibiti kwa kiasi kikubwa uingizaji wa silaha haramu ambapo jumla
ya silaha 405 zilikamatwa katika operesheni mbalimbali kati ya Januari na
Desemba 2012. Natumia fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya
kutekeleza kikamilifu dhana ya Ulinzi Shirikishi na kuwahamasisha Wananchi
kuhusu Utii wa Sheria bila Shuruti. Aidha, napenda kuwakumbusha Wananchi wote
kwamba, suala la Ulinzi na Usalama wa Nchi yetu ni jukumu letu sote. Ni wajibu
wetu kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu kwa Jeshi letu ili hatua za kudhibiti
vitendo hivyo zichukuliwe.
MAUAJI
YA KISHIRIKINA
14. Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za
Serikali za kuwahudumia wazee na watu wenye ulemavu, siku za karibuni kumeibuka
tena dalili za vitendo vya ukatili dhidi ya wazee, wanawake na walemavu wa
ngozi katika baadhi ya Mikoa kwa sababu za kishirikina. Ukatili huo siyo tu
unyama uliopindukia kwa Binadamu wenzetu bali pia unaondoa sifa kubwa ya jamii
yetu ya kupendana pasipo kujali rangi, dini au kabila. Nitumie fursa hii
kuwahakikishia ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, akina mama na wazee kwamba,
Serikali haitavumila kuona ukatili wowote unafanywa dhidi yao.
Naziagiza
Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya zote Nchini kwa kushirikiana na
Jamii kuwabaini na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria wale wote wanaojihusisha
na vitendo hivyo viovu.
MIGOGORO YA DINI
15. Mheshimiwa
Spika, Serikali imetoa uhuru kwa Wananchi wake kuabudu, kila mtu kwa Dini
anayoitaka. Hata hivyo, hivi karibuni kumejitokeza migongano na chokochoko za
kidini ambazo zimeanza kueneza chuki miongoni mwetu. Chokochoko zinazojitokeza
si dalili nzuri kwa mustakabali wa Nchi yetu inayopenda kudumisha Amani,
Utulivu na Umoja wa Kitaifa.
Uzoefu
wa Mataifa mbalimbali umeonesha kwamba chokochoko za kidini zimesababisha
machafuko makubwa na kutoweka kwa amani katika Nchi hizo. Tukumbuke kwamba
yakitokea machafuko ya namna hiyo na kuvurugika kwa amani na utulivu, hakuna
atakayesalimika. Hivyo, natoa wito kwa Viongozi wa Madhehebu ya Dini kuelimisha
Waumini wao kuthamini na kuheshimu dini za wengine na kuepuka vitendo vyovyote
vinavyoamsha hisia za chuki miongoni mwa wafuasi wa Dini
mbalimbali.
MAFUNZO YA JESHI LA KUJENGA TAIFA
16. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali iliahidi kukarabati na kujenga
Makambi kwa ajili ya kuchukua Vijana watakaojiunga na mafunzo ya Jeshi la
Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu
kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imetekeleza ahadi ilizotoa mwaka jana kwa
ufanisi mkubwa. Mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria yameanza mwaka huu kwa
kuchukua Vijana 4,711 sambamba na Vijana 5,893 wa kujitolea wakiwemo baadhi ya
Waheshimiwa Wabunge. Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge vijana
waliojiunga na mafunzo ya JKT mwaka huu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea kuchukua vijana kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa
Sheria.
SHUGHULI
ZA UCHAGUZI, BUNGE, VITAMBULISHO VYA TAIFA, SENSA NA MUUNGANO
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
17. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliendesha Chaguzi
Ndogo za Madiwani katika Kata 29 Tanzania Bara ili kujaza nafasi wazi za Viti
vya Udiwani. Katika chaguzi hizo, Chama Cha Mapinduzi kilishinda Viti 22,
CHADEMA Viti 5 na CUF na TLP Kiti kimoja kimoja. Vilevile, Tume ilifanya teuzi
15 ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi za Udiwani wa Viti Maalum. Katika uteuzi
huo, CCM ilipata viti 10, CHADEMA viti vinne na TLP kiti kimoja. Katika mwaka
2013/2014, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaboresha Daftari la Wapiga Kura ambapo
Awamu ya Kwanza itakamilika mwezi Desemba, 2013. Uboreshaji huo utawezesha
kuchapishwa kwa Daftari la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
MAANDALIZI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA
MITAA
18. Mheshimiwa
Spika, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa
unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2014. Kazi za awali za uchaguzi huo
zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kupitia upya Kanuni za Uchaguzi
zitakazojumuisha maoni ya wadau mbalimbali. Ili kufanikisha uchaguzi huo,
Halmashauri zote Nchini zinatakiwa kuanza maandalizi mapema kwa kupitia na
kuhakiki orodha ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa. Baada ya kuhakiki orodha hiyo,
maombi mapya ya kugawa Vitongoji, Vijiji au Mitaa yawasilishwe katika ngazi
husika kabla ya tarehe 31 Desemba 2013 kwa kuzingatia Sheria na Taratibu
zilizopo.
SHUGHULI ZA BUNGE
19. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Bunge limeendelea kutekeleza majukumu yake ya
kuisimamia na kuishauri Serikali katika nyanja mbalimbali. Aidha, Bunge
limefanya Mikutano mitatu, kupitisha Miswada minne ya Sheria na kuridhia
Maazimio nane. Katika kuboresha utendaji wa Kamati za Kudumu za Bunge, Wajumbe
wa Kamati hizo walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kumudu majukumu yao
vizuri katika nyanja za utafiti, uchambuzi wa Miswada, Sera na Bajeti, utunzaji
wa kumbukumbu na taratibu za uendeshaji wa Bunge. Vilevile, kuanzia tarehe 4
hadi 7 Desemba 2012 Bunge liliandaa kwa mafanikio Mkutano wa Umoja wa Mabunge
Duniani uliofanyika Dar es Salaam ukiwa na kauli mbiu ya “Vita dhidi ya Ukatili
wa Wanawake”.
20. Mheshimiwa
Spika, ili kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi, Kamati za Kudumu za
Bunge zimefanyiwa mabadiliko makubwa kwa kuunda Kamati mpya ya Bajeti na
kugawanya baadhi ya Kamati. Iliyokuwa Kamati ya Nje, Ulinzi na Usalama
imegawanywa mara mbili na kuwa Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Ulinzi na
Usalama. Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala imegawanywa na kuwa Kamati ya
Sheria, Katiba na Utawala na Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Vilevile, Kamati zilizokuwepo awali nazo zimeundwa upya na baadhi kuongezewa
majukumu. Ni imani yangu kwamba Kamati hizo, zitatekeleza wajibu wake kikamilifu
kwa maslahi ya Taifa.
MUUNGANO
21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013,
Serikali imeendelea kuratibu masuala yote ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa
lengo la kudumisha Muungano na ushirikiano wa Serikali zote mbili. Katika
kudumisha ushirikiano huo,Kikao cha Kamati ya Pamoja ya
SMT na SMZ cha kushughulikia Masuala ya Muungano kilifanyika na kujadili Hoja
zinazohusu utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; ushiriki wa Zanzibar
katika Taasisi za Nje na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Ongezeko la gharama
za umeme wa TANESCO kwa ZECO; Usajili wa vyombo vya moto, malalamiko ya
wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili na mgawanyo wa
mapato.
MABADILIKO YA KATIBA
22. Mheshimiwa
Spika, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea
kuratibu, kukusanya na kuchambua maoni ya Wananchi ili kupata Katiba Mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na ridhaa ya Wananchi wenyewe
ifikapo mwaka 2014. Katika mwaka 2012/2013, Tume imekusanya maoni ya Wananchi
kupitia njia mbalimbali na kuanza uchambuzi wa maoni yaliyotolewa ili kuandaa
Rasimu ya Katiba. Tume pia, imeanza maandalizi ya kuunda Mabaraza ya Katiba
katika Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Katiba
yanayojumuisha Asasi, Taasisi na Makundi Maalum ya Watu. Mabaraza hayo yatakuwa
na jukumu la kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa
na Tume. Mabaraza ya Katiba yatawashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi kutoka
makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii.
23. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Tume itaratibu,
Mikutano ya Mabaraza ya Katiba Mpya, kuchambua maoni ya Mabaraza ya Katiba
na kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya itakayowasilishwa katika Bunge Maalum la
Katiba. Vilevile, itachapisha Katiba iliyotokana na maoni ya Bunge Maalum la
Katiba kwa ajili ya kupigiwa Kura ya Maoni. Naipongeza sana Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi sasa. Nawasihi Watanzania wote
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume ili iweze kukamilisha kazi hii muhimu kwa
Taifa letu.
SENSA YA WATU NA MAKAZI 2012
24. Mheshimiwa
Spika, mwaka 2012 ulikuwa ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi ambayo ni ya
tano kufanyika tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Matokeo
yanaonesha kuwa idadi ya watu Nchini imeongezeka kutoka watu milioni 34.5 mwaka
2002 hadi milioni 44.9 mwaka 2012. Hilo ni ongezeko la watu Milioni 10.4 kwa
kipindi cha miaka kumi, sawa na ukuaji wa wastani wa Asilimia 2.7 kwa mwaka. Kwa
ujumla matokeo ya Sensa yanaonesha kasi ya ongezeko la watu ni kubwa
ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa. Kwa kutambua changamoto hiyo,
Serikali pamoja na mambo mengine inaendelea kutekeleza Sera ya Idadi ya Watu ya
mwaka 2006 kwa kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa Uzazi wa Mpango. Nitumie
fursa hii kulikumbusha Bunge lako Tukufu na Watanzania kazi ya uchambuzi wa
takwimu inaendelea ili kupata mchanganuo wa kina zaidi utakaoiwezesha Serikali
kupanga vizuri Mipango yake ya Maendeleo. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itasambaza taarifa mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi zenye mchanganuo wa
kitakwimu na kuhamasisha matumizi yake katika tafiti na kuandaa Mipango ya
Maendeleo katika ngazi zote.
VITAMBULISHO VYA TAIFA
25. Mheshimiwa Spika, Tarehe 07 Februari 2013,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alizindua rasmi Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu, Jijini Dar es Salaam.
Vilevile, tarehe 13 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamedi Shein, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alizindua Zoezi hilo kwa upande
wa Zanzibar. Kuzinduliwa rasmi kwa mfumo huo ni mwanzo wa utoaji wa Vitambulisho
vya Taifa ambavyo vitasaidia kuwatambua na kuwahudumia Wananchi ipasavyo. Zoezi
la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa linaendelea kwa watumishi wa umma waliokuwa
wamesajiliwa na kuhakikiwa. Zoezi la kuingiza taarifa za Wananchi 220,000 kwa
ajili ya kupatiwa Vitambulisho vya Taifa katika Wilaya ya Kilombero iliyoteuliwa
kuwa Wilaya ya mfano limekamilika na uchambuzi wa taarifa za Wakazi wa Dar es
Salaam 2,159,822 waliojiandikisha zinaendelea. Aidha, Wakaazi wa Zanzibar
160,645 na Wageni 180 wameandikishwa. Kazi ya Utambuzi na Usajili wa Watu katika
Mikoa mbalimbali Nchini inaendelea sambamba na utoaji wa Vitambulisho kwa wale
walioandikishwa na kuhakikiwa.
MASUALA
YA UCHUMI
HALI YA UCHUMI
26. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012, Pato halisi la Taifa lilikua kwa Asilimia 6.9
ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.4 mwaka 2011. Sekta zilizochangia zaidi
katika ukuaji huo ni pamoja na Mawasiliano, Fedha, Viwanda, Ujenzi, Madini,
Biashara na Utalii. Kutokana na ukuaji huo, Wastani wa Pato la Mtanzania
umeongezeka kutoka Shilingi 869,436 mwaka 2011 hadi Shilingi 995,298 mwaka
2012, sawa na ongezeko la Asilimia 12.6. Mfumuko wa Bei umepungua kutoka
Asilimia 19.4 mwezi Februari 2012 hadi Asilimia 9.8 mwezi Machi 2013.
Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa na jitihada za Serikali za kuongeza
usambazaji wa vyakula kwenye masoko, kupunguza ujazi wa fedha kwenye soko,
kudhibiti upandaji wa bei ya mafuta ya petroli na kuimarika kwa upatikanaji wa
umeme viwandani ikilinganishwa na mwaka 2011/2012.
MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA
MITANO
27. Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano ambao ulipitishwa na Bunge lako Tukufu Mwaka
2011/2012. Katika kutekeleza Mpango huo, Tume ya Mipango imeweka
utaratibu wa kuchambua kwa kina maandiko ya miradi yote ya kisekta ili
kuhakikisha kwamba imezingatia vipaumbele ambavyo sote tumekubaliana. Baada ya
uchambuzi huo, ndipo fedha hutolewa kwa ajili ya utekelezaji. Pamoja na
utaratibu huo, Serikali imeona ni muhimu kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango
wa Maendeleo kwa kuanzisha Mfumo imara zaidi wa kupanga Vipaumbele, kufuatilia
na kutathmini Utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati ya Maendeleo. Mfumo huo ambao
utasimamiwa na Chombo Maalum (President’s Delivery Bureau) chini ya Ofisi
ya Rais, Ikulu, unazingatia uzoefu wa Nchi ya Malaysia. Chini ya Mfumo huo,
Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa itatengewa fedha za kutosha na usimamizi
wa kina utafanyika kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa
yanafikiwa.
28. Mheshimiwa
Spika, ili Mfumo huo ufanikiwe inabidi kwanza wadau
wote wakubaliane kimsingi vipaumbele ambavyo vitatoa matokeo makubwa na ya
haraka na kisha wataalamu kutoka Serikalini, Sekta Binafsi na Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali kukaa pamoja na kuchambua kwa undani vipaumbele hivyo, namna ya
kuvitekeleza, kubaini watekelezaji na kuibua viashiria vya kupima matokeo.
Tayari zoezi hilo la awali limefanyika ambapo maeneo sita ya kwanza ya
kipaumbele yamefanyiwa uchambuzi wa kina kwa utaratibu unaojulikana kama Maabara
(Labs). Utaratibu huo wa maabara unatoa fursa kwa wataalam na watunga
Sera kukaa pamoja, kufikiri na kuendesha majadiliano ya wazi hadi pale
wanapokubaliana kwamba ufumbuzi wa tatizo umepatikana.Maeneo yaliyojadiliwa
katika awamu ya kwanza ni Nishati na Gesi Asilia, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji
na Kupanua wigo wa Mapato ya Serikali. Baada ya uchambuzi huo kukamilika,
matokeo yake ikiwemo miradi iliyoandaliwa pamoja na Bajeti ya utekelezaji
itawekwa hadharani ili kila Mtanzania ajue kitakachofanyika, kutoa maoni na
kufuatilia kwa kina utekelezaji.
29. Mheshimiwa
Spika, ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo na
uwajibikaji wa kutosha katika kutekeleza vipaumbele vya Kitaifa, Chombo
kitakachoanzishwa (President’s Delivery Bureau) kitakuwa na jukumu la
kuhakikisha kwamba kila Waziri wa Kisekta na Watendaji Wakuu wanawajibika
kusimamia utekelezaji wa miradi ya kipaumbele na pia kufanya tathmini za mara
kwa mara kupima matokeo. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mawaziri
wanaosimamia maeneo sita ambayo tumeanza nayo walitoa ahadi kwamba watakuwa
mstari wa mbele kusimamia kwa weledi utekelezaji wa miradi ya Sekta zao. Ahadi
hizo walizitoa wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza ya mfumo wa maabara
uliofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 22 Februari 2013. Ni matumani yangu kuwa,
utaratibu huo utasaidia sana kuimarisha uwajibikaji, ufuatiliaji na hatimaye
kupata matokeo ya haraka ambayo yatasaidia uchumi kukua kwa kasi zaidi na
hivyo kupunguza umaskini miongoni mwa watu wetu. Ni vyema ieleweke wazi kwamba,
maeneo ya kipaumbele yaliyochaguliwa yatapata sehemu kubwa ya fedha za
maendeleo. Hii ndiyo maana ya dhana ya kupanga ni kuchagua na haina maana
kwamba kazi nyingine za uendeshaji wa Serikali zitasimama. Katika Mwaka
2013/2014, kutafanyika uchambuzi wa kina wa maeneo mengine ya kipaumbele ambayo
yatasaidia Serikali kupanga Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka
2014/2015.
MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI NA
UWEKEZAJI
30. Mheshimiwa
Spika, Serikali inaratibu utekelezaji wa Mpango Kazi
wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini. Lengo ni kuimarisha
ushiriki wa Sekta Binafsi katika shughuli za uwekezaji na Biashara Nchini.
Katika utekelezaji wa Mpango Kazi huo, Serikali imeazimia kupunguza muda
unaotumika kupitisha mizigo Bandarini na Mipakani kwa kuanzisha utaratibu wa
kubadilishana taarifa zinazohusu mizigo kwa njia za kielektroniki kabla mizigo
haijafika kwenye Vituo vya Forodha. Vilevile, Kamati za Pamoja (Joint Border
Post Committees) zimeundwa kwenye Vituo vya Mipakani vya Tunduma, Kabanga,
Mutukula, Holili, Sirari na Namanga. Kupitia Kamati hizo wadau wote
wanaoshughulika na utoaji huduma mipakani hufanya kazi kwa
pamoja.
31. Mheshimiwa
Spika, Serikali imekamilisha Mkakati na Mpango Kazi
wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Vilevile, Mwongozo wa Utendaji kwa ajili ya kutekeleza Sera, Sheria na Kanuni za
Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi umekamilika. Aidha, Serikali
imefanya tathmini ya Sera zinazohusu Uwekezaji kwa kutumia Mfumo wa Tathmini
unaotumiwa na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo
(OECD). Taarifa ya tathmini ya Sera hizo itachangia katika kufanya mapitio ya
Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 pamoja na Sheria yake ya mwaka 1997.
Nazihimiza Wizara na Taasisi za Serikali kuongeza juhudi katika kuainisha miradi
inayokidhi vigezo vya kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP ili Nchi iweze kunufaika
na fursa zinazotokana na utaratibu huo.
32. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kuratibu majadiliano
baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuibua fursa zilizopo na kupata
ufumbuzi wa changamoto za kisera, kisheria na kitaasisi zinazokwamisha biashara
na uwekezaji. Kutokana na umuhimu wa majadiliano hayo, Tanzania itakuwa mwenyeji
wa Mkutano wa Kimataifa wa “Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya
Wote wa mwaka 2013” (Global 2013 Smart Partnership
Dialogue) utakaofanyika mwezi Julai 2013, Jijini Dar es Salaam.
Maandalizi ya Mkutano huo yanaendelea ambapo Mkutano maalum kwa Wakuu wa Mikoa,
Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa ulifanyika mjini Dodoma mwezi Novemba 2012.
Katika Mkutano huo, washiriki walipata uelewa wa pamoja wa dhana ya majadiliano
ya ushirikiano kwa manufaa ya wote yatakayowasaidia kusimamia majadiliano katika
maeneo yao.
33. Mheshimwa
Spika, Serikali imetoa mwongozo kwa Mabaraza ya
Biashara ya Mikoa na Wilaya kuendesha majadiliano katika maeneo yao ili matokeo
ya majadiliano hayo yatumike kikamilifu wakati wa majadiliano ya Kimataifa mwezi
Julai 2013. Uzoefu wa Nchi ambazo zimeandaa majadiliano kama hayo umeonesha
kwamba kuna manufaa makubwa yakiwemo kubaini wagunduzi na wabunifu, kuibua fursa
mpya za teknolojia na uwekezaji na pia kupata uzoefu wa Mataifa mengine katika
masuala mbalimbali. Natoa wito kwa Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya
kuendesha majadiliano katika maeneo yao na kujiandaa kikamilifu kushiriki katika
Mkutano huo.
34. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
Januari 2012 hadi Desemba 2012, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kilisajili Miradi
869 yenye thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 30,866. Kati ya miradi
hiyo, Miradi 469 sawa na Asilimia 54 ni miradi ya wawekezaji wa ndani, Miradi
195 sawa na Asilimia 22 ni ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na Nje na Miradi
205, sawa na Asilimia 24 ni ya wawekezaji kutoka Nje. Usajili wa miradi
hiyo umeongeza ajira Nchini ambapo zaidi ya Watanzania 174,412 walipata ajira
kwenye miradi hiyo. Tathmini ya thamani ya uwekezaji kisekta inaonesha kwamba
katika mwaka 2012 miradi ya Sekta ya Kilimo inaongoza ikiwa imechangia Shilingi
Bilioni 14,226 ikifuatiwa na Sekta ya Uzalishaji Viwandani iliyochangia
Shilingi Bilioni 4,672. Sekta hizo zinafuatiwa na Sekta ya Mawasiliano
iliyochangia Shilingi Bilioni 4,663 na Sekta ya Nishati iliyochangia Shilingi
Bilioni 2,110. Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa ya kufanya
kazi kama Timu moja katika kuvutia wawekezaji. Ili kuweza kuvutia wawekezaji
katika hali endelevu, ni muhimu sana Sera na Sheria za Uwekezaji zikatoa
Mwongozo ambao unatabirika kwa muda mrefu.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
35. Mheshimiwa Spika, Serikali imeratibu na kufanya tathmini ya Mifuko mbalimbali ya
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji wa
Mwananchi, Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, SIDO,
SELF, Agriculture Input Trust Fund na Presidential Trust Fund.
Mifuko mingine ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake,
Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya Nje na Mfuko wa Kudhamini Taasisi za
Fedha Kutoa Mikopo kwa Miradi Midogo na ya Kati. Katika Makubaliano
yaliyofikiwa baina ya Serikali na Taasisi za Fedha zilizoteuliwa kutoa mikopo
kwa wajasiriamali ni kwamba Taasisi hizo zikopeshe mara tatu zaidi ya dhamana
iliyotolewa na Serikali. Katika kutekeleza makubaliano hayo, hadi Desemba 2012
Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira ulitoa mikopo kwa
Wajasiriamali 76,546 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 50.06. Urejeshaji wa
mikopo hiyo umefikia wastani wa Asilimia 82. Aidha, katika kipindi hicho,
Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi umetoa mikopo ya Shillingi Bilioni 8.6 kwa
Mikoa 11, Wilaya 27, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOs) 49 na Wajasiriamali
8,497. Ufuatiliaji wa maendeleo ya Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji unaonesha
kuwa Wananchi waliopata mikopo wameweza kupiga hatua za kimaendeleo kwa kuongeza
tija na uzalishaji katika shughuli zao na hatimaye kuongeza kipato na kuboresha
hali zao za maisha.
36. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa awamu ya pili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
ulikamilika mwaka 2012. Tathmini ya utekelezaji imeonesha kwamba TASAF imetoa
mchango mkubwa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo
Vijijini iliyoibuliwa na Wananchi. Katika utekelezaji wa awamu hiyo, jumla ya
Miradi 1,010 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 20 iliibuliwa na kuwezeshwa
katika Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, mafunzo ya
ujasiriamali yalitolewa kwa Vikundi 1,778 vyenye wanachama 22,712 katika
Halmashauri 44 kwa lengo la kuviimarisha ili kuongeza ufanisi zaidi katika
shughuli zao.
37. Mheshimiwa Spika, kutokana na mafanikio hayo,
tarehe 15 Agosti 2012, awamu ya tatu ya TASAF ilizinduliwa Mjini Dodoma na
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Awamu hiyo itakayogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 440 inatekeleza Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini Zilizo Katika Mazingira Hatarishi. Mpango huo unalenga
kuziwezesha kaya maskini kupata chakula na kujiongezea fursa za kipato kwa
kuzipatia fedha ili kumudu mahitaji ya msingi kama vile lishe bora, huduma za
afya na elimu. Mpango huo utakaotekelezwa kwa awamu katika Halmashauri zote
Tanzania Bara na Zanzibar, umeanza kwa utambuzi wa Kaya maskini katika Vijiji 20
vya Halmashauri ya Bagamoyo ambapo jumla ya Kaya 3,056 zimetambuliwa. Zoezi hilo
linaendelea kwenye Halmashauri nyingine 13 na ifikapo Juni 2014, Halmashauri
zote Nchini zitafikiwa.
UZALISHAJI MALI
KILIMO CHA MAZAO YA CHAKULA NA
BIASHARA
38. Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kuongeza tija
na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Hatua hizo ni pamoja na
kutekeleza Azma ya KILIMO KWANZA, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP),
Mpango wa Utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo na Dawa za Kilimo, Programu ya Kuendeleza
Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Programu Kabambe ya
Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development
Programme – CAADP) na kuboresha huduma za ugani na utafiti katika Sekta ya
Kilimo. Hatua nyingine ni pamoja na kuvutia Wawekezaji katika Sekta ya Kilimo,
kuhimiza Kilimo cha Umwagiliaji, kuongeza fursa za upatikanaji wa zana bora za
kilimo hasa matrekta, kuimarisha masoko na kurahisisha upatikanaji wa mitaji
kutoka Vyombo vya Fedha, hususan kupitia Dirisha la Kilimo katika Benki ya
Maendeleo Tanzania.
39. Mheshimiwa
Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa jitihada za kuendeleza
Kilimo zimeanza kuleta matumaini hasa katika kuongeza upatikanaji wa Pembejeo za
Kilimo na kuongeza tija na uzalishaji. Kwa mfano, katika mwaka 2012/2013, Tani
226,092 za mbolea zilifikishwa kwa Wakulima 3,792,000 Nchini na
upatikanaji wa mbegu bora ulifikia Tani 30,443 ikilinganishwa na Tani 28,612
zilizozalishwa mwaka 2011/2012. Kutokana na ongezeko la matumizi ya mbolea na
Wakulima kuzingatia Kanuni za Kilimo Bora, tija anayopata mkulima katika zao la
mahindi chotara kwa sasa ni Wastani wa Tani 3.9 kwa hekta na tija ya uzalishaji
wa zao la mpunga ni Tani 3.8 kwa hekta katika maeneo ya
umwagiliaji.
40. Mheshimiwa
Spika, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa utoaji ruzuku ya mbolea na
mbegu bora kwa kutumia utaratibu wa Vocha mwaka 2008/2009. Pamoja na mafanikio
yaliyopatikana kutokana na utaratibu huo, hasa kuongezeka kwa upatikanaji na
matumizi ya mbolea na mbegu bora pamoja na tija katika uzalishaji wa mazao
ya kilimo, mpango huo umekuwa na changamoto kadhaa. Changamoto zilizojitokeza
ni pamoja na mbolea na Vocha kuchelewa kufika kwa walengwa; uteuzi wa Mawakala
usiozingatia vigezo na udanganyifu uliofanywa na baadhi ya Mawakala kwa
kushirikiana na Watumishi wasio waaminifu pamoja na Wajumbe wa Kamati za
Pembejeo katika ngazi mbalimbali za utekelezaji. Serikali imechukua hatua kwa
kufanya ukaguzi maalum kwenye maeneo yaliyokuwa na upungufu huo na waliobainika
kuhusika na udanganyifu wamefikishwa kwenye Vyombo vya
Sheria.
41. Mheshimiwa
Spika, mwaka jana Serikali iliahidi kufanya mapitio ya Mfumo wa utoaji wa
mbolea ya ruzuku na mbegu bora kwa kutumia utaratibu wa Vocha ili kuondoa
upungufu uliojitokeza. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali
imeboresha mfumo huo na kuanzia mwaka 2013/2014 ruzuku ya pembejeo za kilimo
itatolewa kwa Mikopo kupitia Vikundi vya Wakulima.
UMWAGILIAJI
42. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imepanua eneo la Kilimo cha
Umwagiliaji Nchini. Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa
miundombinu katika skimu 21 za umwagiliaji zenye eneo la hekta 19,567. Kazi
nyingine zinazoendelea ni kukamilisha ujenzi wa Mabwawa matano ya Umwagiliaji ya
Mahiga (Kwimba); Inala (Tabora); Lwanyo (Mbarali); Mesaga (Serengeti) na
Dongobesh (Mbulu). Miradi mingine iliyotekelezwa ni Skimu 34 zenye eneo la Hekta
17,824 kwa kutumia Mfuko wa Wilaya wa Kuendeleza Umwagiliaji. Katika mwaka
2013/2014, Serikali itaanza ujenzi wa mabwawa matatu ya Idodi (Iringa); Manyoni
(Singida) na Masengwa (Shinyanga Vijijini).
KILIMO CHA MATUNDA NA MBOGA
43. Mheshimiwa
Spika, Kilimo cha matunda na mboga kina mchango mkubwa katika ukuaji uchumi,
fursa za ajira, lishe na kupunguza umaskini. Kwa kuzingatia umuhimu
huo, Serikali inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Mazao ya
Bustani wa mwaka 2010/2011 – 2020/2021. Utekelezaji wa Mkakati huo unaolenga
kukuza uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mazao ya bustani; ujenzi wa
miundombinu; uhifadhi bora wa Mazao ya Bustani; ujenzi na utafutaji wa masoko;
na ukuzaji rasilimali watu umeanza kuonesha matokeo mazuri. Uzalishaji wa mazao
ya bustani umeongezeka kutoka Tani milioni 4.1 mwaka 2009/2010 hadi Tani milioni
5.1 mwaka 2012/2013 na mauzo ya mazao hayo nje ya Nchi yameongezeka kutoka
Shilingi Bilioni 159.8 mwaka 2009 hadi Bilioni 602.1 mwaka 2012. Mafanikio haya
ni ya kuridhisha ingawa bado kuna fursa kubwa ya kuongeza tija na ufanisi katika
sekta hii. Tayari tunao Mwongozo wa Kilimo cha Embe ambao utatuwezesha kuongeza
tija na uzalishaji wa zao hilo. Miongozo ya Uzalishaji bora wenye tija kwa mazao
mengine ya bustani itaandaliwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itatoa
mafunzo ya teknolojia za uzalishaji wa miche bora ya mazao ya bustani hususan
kwa vikundi vya Vijana.
MWENENDO WA BEI ZA MAZAO MAKUU
44. Mheshimiwa
Spika, mwenendo wa bei za mazao makuu ya biashara Nchini ambayo ni Pamba,
Kahawa, Chai, Tumbaku, Korosho, Katani na Pareto umekuwa ukibadilika mara kwa
mara kwa kutegemea bei za Soko la Dunia. Mabadiliko hayo yanawaathiri sana
wakulima wetu pale bei zinaposhuka. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilikutana na
Wadau wa mazao makuu asilia ya biashara Nchini ili kuangalia uwezekano wa
kuanzisha Mfuko Maalum wa kufidia bei za Mazao kwa wakulima pale zinaposhuka
(Price Stabilization Fund). Lengo ni kuwawezesha wakulima kupata bei
nzuri ya mazao na kuwaepusha na hasara inayotokana na kushuka kwa bei hizo
katika masoko ya kimataifa na pia kuwahamasisha wakulima kuendelea kulima mazao
husika. Serikali kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Bodi Sita za mazao
inayafanyia kazi maoni ya wadau kuhusu kuanzisha Mfuko Maalum wa Kufidia Bei za
mazao.
45. Mheshimiwa
Spika, mwezi Septemba na Novemba 2012, niliongoza Mikutano mikubwa
iliyolenga kuwaleta pamoja Watunga Sera, Washirika wa Maendeleo na Wawekezaji
ili kujadili fursa na changamoto mbalimbali za Sekta ya Kilimo. Katika Mikutano
hiyo, wadau waliandaa na kukubaliana Mpango Kazi ulioainisha majukumu
yatakayotekelezwa na kila mdau ili kuongeza uwekezaji katika Ukanda wa SAGCOT.
Majukumu ya Serikali ni pamoja na upimaji ardhi kwa ajili ya kilimo,
ujenzi wa miundombinu ya msingi na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji
katika Sekta ya Kilimo. Serikali imechukua hatua kwa kuainisha na kuweka mipaka
ya ardhi kwa kuanzia na Wilaya za Kilombero, Ulanga na Rufiji. Zoezi hilo la
kuanisha ardhi limelenga kutoa kipaumbele cha kwanza katika upatikanaji wa ardhi
kwa ajili ya wakulima wadogo. Hadi sasa ardhi ya Vijiji 100 katika Wilaya ya
Kilombero imepimwa.
46. Mheshimiwa
Spika, wawekezaji wengi wa ndani na nje ya Nchi wameonesha mwamko mkubwa wa
kuwekeza katika ukanda wa SAGCOT. Msisitizo wa Serikali ni kwamba kila mwekezaji
mkubwa atakayewekeza atalazimika kuwa na Mpango wa kuendeleza na kushirikiana na
wakulima wadogo. Hatua hiyo itamsaidia mkulima mdogo kupata teknolojia mpya,
uhakika wa pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji pamoja na soko la uhakika.
Tayari utaratibu wa namna hiyo umeanza kuonesha matokeo mazuri Wilayani
Kilombero.
47. Mheshimiwa
Spika, katika hatua nyingine, Washirika wa Maendeleo ambao ni Shirika la
Maendeleo la Marekani, Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Uingereza
wamekubali kusaidia ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 103 kwa kiwango
cha lami ambayo itaunganisha Mikumi na Ifakara katika Bonde la Kilombero. Hatua
za awali za ujenzi wa barabara hiyo zimeanza. Kukamilika kwa barabara hiyo
muhimu kutafungua fursa zaidi za uwekezaji na kurahisisha usafiri na
usafirishaji wa mazao ya wakulima. Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati
Washirika wetu hao wa Maendeleo kwa kukubali kusaidia utekelezaji wa mradi
huo.
MIUNDOMBINU YA MASOKO YA MAZAO
48. Mheshimiwa
Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya masoko ya
mazao kama moja ya mkakati madhubuti wa kumrahisishia mkulima kufikisha mazao
yake sokoni na kuongeza bei ya mazao hayo. Chini ya Programu ya Miundombinu
ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini, Serikali,
imekamilisha usanifu na kutangaza zabuni za ujenzi wa barabara zenye
jumla ya Kilometa 210.8 katika Halmashauri za Mbulu, Njombe, Iringa Vijijini,
Kahama, Lushoto, Rufiji, Songea Vijijini na Singida Vijijini. Aidha, zabuni kwa
ajili ya ujenzi wa maghala mawili katika Halmashauri za Wilaya ya Iringa
Vijijini na Njombe zimetangazwa na taratibu za ujenzi wa ghala katika
Halmashauri ya Mbulu zinakamilishwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea
na ujenzi wa barabara na miundombinu mingine ya masoko Tanzania Bara na
Zanzibar.
MAENDELEO YA SEKTA YA MIFUGO
49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2012/2013 Serikali imeanza kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kuendeleza
Sekta ya Mifugo (2011/2012 – 2015/2016). Programu hiyo inalenga kuwa na Sekta ya
Mifugo ya kisasa itakayoongeza ukuaji wa Sekta kutoka Asilimia 2.3 hadi 4.5 kwa
mwaka ifikapo mwaka 2016. Ili kufikia malengo hayo, Serikali pamoja na mambo
mengine, imezielekeza Halmashauri zote Nchini kufanya tathmini ya uwezo wa ardhi
katika maeneo yao ili kufuga kulingana na uwezo wa eneo
lililopo.
50. Mheshimiwa
Spika, Serikali pia imeboresha huduma za uhamilishaji pamoja na kutoa
Ruzuku ya Dawa za Kuogesha Mifugo Lita 92,323 zenye thamani ya Shilingi Bilioni
1.5 ambazo zimesambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Hatua hiyo imekwenda
sambamba na kujenga Majosho Mapya 14 na kukarabati Majosho 20 katika Mikoa
ya Arusha, Iringa, Kagera, Lindi, Mara, Mbeya, Mwanza, Katavi, Rukwa, Ruvuma,
Simiyu, Singida, Geita na Tanga. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo ya
unenepeshaji mifugo kwa Wafugaji wanaozunguka Ranchi za Taifa. Pia, Miradi 13 ya
unenepeshaji mifugo imeibuliwa kupitia Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya
katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Mwanza, Shinyanga na Singida. Hatua
hiyo imeongeza idadi ya Ng’ombe walionenepeshwa kutoka 132,246 mwaka 2011 hadi
Ng’ombe 150,000 mwaka 2012. Aidha, Vijiji 781 vya Halmashauri za Wilaya 80
katika Mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Pwani, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Singida
vimepimwa ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na watumiaji
wengine wa ardhi.
51. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya
Kuendeleza Sekta ya Mifugo ili itoe mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Aidha,
itakamilisha ujenzi wa Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo ambao unatarajiwa
kuanza kazi mwezi Agosti 2013. Vilevile, itaimarisha uhamilishaji Nchini kwa
kuzalisha Dozi za mbegu bora za uhamilishaji.
MAENDELEO YA SEKTA YA UVUVI
52. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeanza kupitia Sera ya Taifa ya
Uvuvi ya mwaka 1997 na kuandaa Mkakati wa utekelezaji. Lengo ni kuihuisha Sera
hiyo ili iendane na mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii yaliyojitokeza pamoja na
kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia katika Sekta ya Uvuvi. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali itakamilisha kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka
1997 na kuendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Aidha, Vikundi
vya Ulinzi Shirikishi vya Kudhibiti Uvuvi Haramu na Vituo vya Doria
vitaimarishwa. Serikali pia itaendelea kusimamia shughuli za ukuzaji wa viumbe
kwenye maji ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kuzalisha vifaranga vya
samaki.
UFUGAJI NYUKI
53. Mheshimiwa Spika, Uzalishaji wa Asali na Nta kwa miaka ya hivi
karibuni unatupa moyo kwamba, Ufugaji wa Nyuki unaweza kuwa ni shughuli ya
kiuchumi inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea umaskini.
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita 2009 - 2012, uzalishaji wa Asali
ulifikia Wastani wa Tani 8,747 na Nta Tani 583. Katika juhudi za kuongeza
uzalishaji, Serikali imetoa elimu ya ufugaji nyuki katika
Wilaya za Kahama (Vijiji 7), Chunya (Vijiji 4), Same (Vijiji 2), Manyoni (Vijiji
3), Singida (Vijiji 2) na Kibondo (Vijiji 13). Aidha, Mizinga 500 imesambazwa
katika Wilaya za Ruangwa, Mtwara, Newala, Tunduru na Namtumbo ambapo kila Wilaya
ilipata Mizinga 100. Pamoja na juhudi hizo, Hekta 56,290 zimepimwa kwa ajili ya
kutenga hifadhi za nyuki katika Vijiji mbalimbali
Nchini.
54. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa
Sekta ndogo ya Ufugaji Nyuki kwa maendeleo ya Wananchi, niliahidi kwamba
yatafanyika Maonesho Maalum ya Ufugaji Nyuki. Maonesho hayo yamefanyika Kitaifa
Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 - 7 Oktoba 2012 katika Viwanja vya Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere ambapo yalitanguliwa na Kongamano lililofanyika tarehe 3
Oktoba 2012. Kauli Mbiu ya Maonesho ilikuwa ni “ASALI KWA AFYA NA USTAWI”.
Maonesho hayo yameleta chachu na matumaini makubwa ya kukua kwa biashara ya
mazao ya Nyuki kwani tangu kumalizika, Wafugaji Nyuki wa Tanzania wamepata soko
la kuuza zaidi ya Tani 100 za Asali Nchini Ujerumani. Aidha, Wajasiriamali wengi
wamepata Alama ya Utambulisho wa Biashara (Barcode) kwa ajili ya
kutambulisha Asali yao. Vilevile, kutokana na wananchi kuhamasika kufuga nyuki,
Serikali imeanza kutengeneza mizinga bora ipatayo 70,000, kuiwekea chambo na
kuisambaza kwa wananchi kwa gharama nafuu.
55. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Sekta
ya Nyuki, kwa mara ya kwanza Tanzania iliadhimisha siku ya Kitaifa
ya Kutundika Mizinga, tarehe 4 Machi 2013 katika Hifadhi ya Aghondi iliyopo
Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida. Katika uzinduzi huo, Wadau walipata
nafasi ya kutambua fursa kubwa zilizopo katika Sekta hiyo na kujenga mahusiano
ya karibu ya kibiashara. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itafanya mapitio ya Sera ya Ufugaji Nyuki ya
mwaka 1998 ili iendane na mabadiliko yanayotokea. Aidha, mafunzo na vifaa kwa
ajili ya ufugaji nyuki yatatolewa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa Asali na
Nta.
MAENDELEO YA VIWANDA
56. Mheshimiwa
Spika, mchango wa Sekta ya Viwanda kwenye Pato la Taifa uliongezeka na
kufikia Asilimia 9.7 mwaka 2012 ikilinganishwa na Asilimia 9.0 mwaka 2011.
Viwanda vinavyoendelea vizuri katika uzalishaji na kutoa mchango mkubwa ni
pamoja na viwanda vya saruji, bia, unga wa ngano, vinywaji baridi, sukari,
rangi, nyaya za umeme na usindikaji wa ngozi. Kwa upande wa SIDO, jumla ya
Wajasiriamali 4,766 wamepatiwa mafunzo mbalimbali ya kukuza ujuzi wao
hususan katika usindikaji wa mafuta ya kupikia, ngozi, ubanguaji wa
korosho pamoja na kuhifadhi na kusindika vyakula vya aina mbalimbali.
Aidha,
SIDO
ilitoa huduma za ugani kwa Wajasiriamali 6,779 ili kuboresha shughuli za
uzalishaji. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kubuni mikakati mipya
yenye lengo la kuendeleza na kuviwezesha viwanda vidogo na vya kati vya
wajasiriamali wa ndani pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa viwanda
Nchini.
57. Mheshimiwa Spika, ili kuhamasisha Usindikaji wa
Ngozi hapa Nchini na kuongeza thamani ya zao la ngozi, mwezi Julai 2012,
Serikali iliongeza Ushuru wa Ngozi Ghafi zinazouzwa nje ya Nchi kutoka Asilimia
40 hadi 90 kwa kilo. Kutokana na hatua hiyo, ngozi zinazosindikwa Nchini
zimeongezeka kutoka vipande vya ngozi za Ng’ombe 166,773 na vipande vya ngozi za
Mbuzi na Kondoo 778,023 kipindi cha Januari - Juni, 2012 hadi vipande vya ngozi
za Ng’ombe 343,860 na vipande vya ngozi za Mbuzi na Kondoo 1,173,875 kipindi cha
Julai - Desemba, 2012. Ongezeko hilo linathibitisha kwamba hatua zilizochukuliwa
na Serikali zimeongeza usindikaji wa ngozi na kupanua wigo wa uzalishaji wa
mazao ya ngozi Nchini. Serikali itaendelea kusimamia mafanikio hayo na kuchukua
hatua zaidi zitakazoongeza usindikaji wa ngozi hapa
Nchini.
SEKTA YA UTALII
58. Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa kuifanya Mikoa ya Dar es Salaam,
Lindi, Mtwara na Tanga kuwa vituo vya utalii wa fukwe. Mikoa hiyo ina fukwe za
kipekee zinazovutia watalii na pia zinafaa kwa uwekezaji wa kitalii. Vilevile,
Serikali imevitangaza vivutio vya utalii katika soko la ndani na nje ya nchi
kupitia Vyombo vya Habari na maonesho ya ndani na Kimataifa. Kutokana na hatua
hiyo, idadi ya Watalii walioingia nchini mwaka 2012 imeongezeka na kufikia
watalii 930,753 ikilinganishwa na watalii 867,994 mwaka 2011. Aidha, mapato
yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 2,119 mwaka 2011 hadi
Shilingi Bilioni 2,183 mwaka 2012.
59. Mheshimiwa Spika, matunda ya juhudi za
kutangaza vivutio vya utalii na pia kuhamasisha utalii wa ndani yamedhihirika
baada ya Taasisi ya The Seven Natural Wonders yenye Makao yake Nchini Marekani kuijumuisha Tanzania katika zoezi la
kutafuta Maajabu Saba ya Asili katika Bara la Afrika. Zoezi hilo lilishirikisha
wataalam wengi Duniani na kupigiwa kura na watu kutoka sehemu mbalimbali,
wakiwemo Watanzania kwa kutumia Tovuti. Matokeo ya zoezi hilo yalitangazwa
tarehe 11 Februari 2013, Jijini Arusha, ambapo Tanzania iliibuka mshindi kwa
vivutio vitatu vya Maajabu Saba ya Asili ya Afrika yakijumuisha Mlima
Kilimanjaro,Ngorongoro Crater na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Napenda
kutumia fursa hii kuwashukuru Watanzania wote wa ndani na nje ya Nchi
walioshiriki kupiga kura na hatimaye kutuwezesha kupata ushindi huo. Aidha,
namshukuru Dkt. Philip Imler ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi ya The Seven
Natural Wonders aliyesimamia zoezi hilo. Pia, nayashukuru Makampuni yote
yaliyofadhili mashindano hayo na kutangaza vivutio vya Tanzania Barani Afrika na
Duniani kote. Natoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha kwamba tunavilinda,
tunavitunza na kuviendeleza vivutio hivyo kwa manufaa ya Taifa letu. Tutumie pia
ushindi huo kutangaza zaidi utalii wetu ili rasilimali hizi nzuri tulizo nazo
ziendelee kuvutia watalii wengi na kuongeza mapato yetu.
SEKTA YA MADINI
60. Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wa madini wana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa
Nchi yetu. Ili kuwaendeleza wachimbaji hao, Serikali imekamilisha Mkakati,
Mpango Kazi na Programu ya Mafunzo pamoja na kuwatengea maeneo wachimbaji
wadogo kwa mujibu wa Sheria. Maeneo hayo ni Mpambaa (Singida), Kilindi
(Tanga), Dete na Melela (Morogoro), Winza (Dodoma), Songwe (Mbeya), Nyakunguru
(Mara), Nyamilonge na Ilagala (Kigoma), Mihama (Katavi), Mwajanga (Manyara),
Makanya (Kilimanjaro) na Mbesa (Ruvuma). Aidha, Serikali imekusanya takwimu na
taarifa muhimu za wachimbaji wadogo kote Nchini kwa lengo la kuwatambua,
kufahamu changamoto walizonazo na kujenga kanzidata
(database).
61. Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa Mwanachama kamili wa Mpango wa Kimataifa Unaohimiza
Uwazi katika Sekta ya Madini (Extractive Industries Transparency
Initiatives- EITI) baada ya kutimiza vigezo vilivyowekwa kimataifa katika
Sekta ya Madini. Hatua hiyo imeiwezesha Tanzania kuwa na mfumo thabiti wa utoaji
taarifa za malipo na mapato kutoka katika kampuni zinazojishughulisha na
uchimbaji wa Madini, Gesi Asilia na Mafuta ambao unamwezesha mwananchi kufahamu
na kujadili mchango wa Kampuni hizo katika Pato la Taifa. Katika mwaka
2013/2014, Serikali itaimarisha ukaguzi kwenye uzalishaji na biashara ya madini
pamoja na kuimarisha STAMICO ili itekeleze majukumu yake
kikamilifu.
HALI YA AJIRA NCHINI
62. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu
wa kuongeza fursa za ajira kwa vijana wengi wanaoingia kwenye soko la ajira
kila mwaka. Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Ajira na Kipato Nchini wa
mwaka 2010/2011, Ajira ziliongezeka kutoka 1,276,982 mwaka 2010 hadi Ajira
1,362,559 mwaka 2011, sawa na ongezeko la Asilimia 6.7. Ili kuongeza kasi ya
ukuaji wa ajira, Serikali inakamilisha Programu ya Kitaifa ya
Kukuza Ajira kwa Vijana. Programu hiyo ya miaka mitatu itaongeza fursa za
Vijana 301,100 kuweza kujiajiri au kuajiriwa.Msukumo zaidi utawekwa katika Miradi ya Kilimo, Viwanda
Vidogo, Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZ na SEZ), Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Sambamba na hatua hiyo, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa
wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi na vya Elimu ya Juu ili kuwawezesha kujiajiri baada
ya kuhitimu mafunzo yao.
HUDUMA
ZA KIUCHUMI
ARDHI
63. Mheshimiwa
Spika, pamoja na Nchi yetu kuwa na ardhi ya kutosha na inayofaa kwa Kilimo
na uwekezaji mwingine, bado hatujakamilisha zoezi la uwekaji mipaka, kupima na
kutoa Hati kwa matumizi mbalimbali. Hali hiyo inachangia migogoro ya ardhi na
kukwamisha uwekezaji kwa kiasi kikubwa. Serikali imechukua hatua muhimu kwa
kutumia teknolojia ya kisasa itakayoharakisha zoezi la upimaji ardhi. Katika
kutekeleza kazi hiyo, Awamu ya Kwanza ya usimikaji wa Mtandao wa Alama za Msingi
za Upimaji Ardhi Nchini (Geodetic Control Network) imekamilika. Mikoa
iliyohusika ni Pwani, Morogoro, Mara, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Lindi, Tabora
na Dodoma. Tayari majaribio ya matumizi ya Alama hizo yamefanyika katika Wilaya
za Ngorongoro na Kilombero na kudhihirisha kuwa gharama na muda wa kupima ardhi
zimepungua. Awamu ya Pili ya usimikaji wa Alama hizo utaendelea katika Mikoa
iliyobaki na kuanza upimaji wa viwanja na mashamba kwa kutumia utaratibu mpya wa
upimaji wa ardhi.
64. Mheshimiwa
Spika, ili kuwa na mfumo endelevu wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi,
Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi.
Mfumo huo utakaounganisha Ofisi za Ardhi Nchini unategemewa kukamilika mwaka
2014 na utaiwezesha Tanzania kuwa na kumbukumbu sahihi za ardhi. Vilevile,
utaharakisha na kurahisisha utoaji wa maamuzi, upimaji na utoaji wa Hati Miliki
na hivyo kupunguza migogoro ya ardhi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea na ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za ardhi na
kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
NISHATI
65. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusogeza huduma ya nishati ya umeme karibu na
Wananchi ili kuharakisha maendeleo yao. Katika kutekeleza azma hiyo,
gharama za kuunganisha umeme wa njia moja kwa wateja wadogo Vijijini na
Mijini zimepunguzwa kwa wastani wa kati ya Shilingi Milioni 1,311,000 na
Shilingi 114,000. Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi kumudu gharama ya
kuunganisha umeme na kuongeza kasi ya usambazaji umeme Nchini. Serikali pia,
imefikisha umeme katika Makao Makuu ya Wilaya za Nkasi na Namtumbo, hivyo
kufanya idadi ya Makao Makuu ya Wilaya zenye umeme kuwa 117, sawa na Asilimia 88
ya Wilaya zote Nchini. Vilevile, Serikali inatekeleza Programu Kabambe ya
Kusambaza Umeme Vijijini ambapo wateja 8,046 wamelipiwa gharama za kuunganishiwa
umeme kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini. Aidha, kazi ya kusambaza na kuboresha
miundombinu ya umeme katika Mikoa ya Mtwara na Lindi inaendelea
kufanyika.
66. Mheshimiwa Spika, Sekta ndogo ya Gesi Asilia inakua kwa kasi ambapo hadi kufikia Januari
2013, kiasi cha futi za ujazo Trilioni 35 zimegundulika Nchini. Ili kusimamia
rasilimali hiyo muhimu, Serikali imeandaa rasimu ya Sera ya Gesi Asilia na
kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali. Aidha, tarehe 8 Novemba 2012,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar
es Salaam. Mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme na kupunguza gharama za umeme
Nchini.
67. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mradi wa
bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ujenzi wa Mitambo ya
kuzalisha umeme wa Kinyerezi (MW 200). Vilevile, itaanza kutekeleza Awamu ya
Pili ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini na kufikisha umeme wa gridi
kwenye Makao Makuu ya Wilaya zisizokuwa na umeme.
TEKNOLOJIA YA HABARI NA
MAWASILIANO
68. Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa
Taifa wenye Awamu Tano. Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Ujenzi wa Mkongo huo
wenye urefu wa Kilomita 7,560 imekamilika na kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa
24 ya Tanzania Bara. Kazi ya kuunganisha Kisiwa cha Unguja na
Mkongo huo kupitia Dar es Salaam itakamilika mwaka 2013. Tayari Makampuni ya
Simu na Mawasiliano ya hapa Nchini yameunganishwa kwenye Mkongo hatua ambayo
imewezesha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano katika eneo kubwa zaidi na
kwa gharama nafuu. Sambamba na hatua hiyo, Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo wa
Kuratibu Huduma za Mawasiliano Nchini (Traffic Monitoring System). Mfumo
huo utasaidia kuhakikisha mapato yanayotokana na huduma katika Sekta ya
Mawasiliano yanajulikana ili Makampuni ya Mawasiliano Nchini yalipe kodi stahiki
kwa Serikali.
69. Mheshimiwa
Spika, Tanzania pamoja na Nchi zote Duniani kupitia Umoja wa Mawasiliano
Duniani (ITU) zimekubaliana kusitisha matumizi ya teknolojia ya utangazaji
kutoka Mfumo wa Analojia na kuanza Matumizi ya Teknolojia ya Dijitali ifikapo
Juni 2015. Hapa Nchini, usitishaji wa matumizi ya mfumo wa mitambo ya analojia
umeanza kutekelezwa tarehe 31 Desemba 2012 kwa awamu kwa kuanzia na Jiji la
Dar es Salaam na kufuatiwa na Mikoa ya Dodoma, Tanga na Mwanza. Matangazo
ya analojia yataendelea kusitishwa katika Mikoa mingine Nchini kulingana na
ratiba iliyowekwa. Natambua kwamba kuna changamoto zilizojitokeza katika
utekelezaji wa zoezi hilo la mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko hayo yanalenga
kuimarisha mawasiliano na kuiwezesha Nchi yetu kuendana na hali halisi ya
mabadiliko ya teknolojia Duniani. Katika mazingira ya sasa, sisi kama Taifa
siyo vyema kubaki kama kisiwa wakati tumeunganishwa na mifumo ya
teknolojia ya kidunia.
Hivyo,
ni busara tuendelee na mabadiliko hayo sasa kuliko kusubiri na hatimaye
tukajikuta tuko nyuma na nje ya mstari. Natoa wito kwa Watanzania wote kuyaona
mabadiliko hayo kwa mtazamo chanya na kuyakubali kama hatua kubwa sana ya
maendeleo ya teknolojia Nchini.
SAYANSI NA TEKNOLOJIA
70. Mheshimiwa
Spika, Serikali inafanya jitihada kubwa za kuendeleza Sayansi na Teknolojia
kama njia ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Jitihada hizo ni pamoja na
kutenga fedha za kutosha kila mwaka kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya
kisayansi. Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia
ya Nelson Mandela iliyopo Mkoani Arusha ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 2
Novemba 2012. Kukamilika kwa ujenzi wa Taasisi hiyo kumeongeza udahili wa
wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu kutoka wanafunzi 83 mwaka 2011/2012
hadi wanafunzi 135 mwaka 2012/2013.
71. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kueneza Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake katika maeneo mbalimbali Nchini na Nchi
jirani. Vilevile, Serikali itaendelea na zoezi la kuhama kutoka katika mfumo wa
analojia kwenda dijitali na kupanua na kuboresha Mtandao wa Huduma za
Mawasiliano ya simu na intaneti Nchini.
BARABARA NA MADARAJA
72. Mheshimiwa Spika, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika kujenga, kukarabati na
kuboresha mtandao wa Barabara Kuu, za Mikoa, Wilaya pamoja na za Vijijini ili
zipitike wakati wote wa mwaka. Lengo ni kuwa na mtandao bora wa barabara
utakaowezesha Wananchi, hasa Wakulima kusafirisha mazao yao hadi kwenye
Masoko ya ndani na nje ya Nchi. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imejenga
jumla ya Kilometa 294.4 za kiwango cha lami katika Barabara Kuu na za
Mikoa na kukarabati kwa kiwango cha lami jumla ya Kilometa 111.8 katika
barabara hizo. Aidha, kazi za ujenzi na ukarabati wa Barabara Kuu na za Mikoa
zenye urefu wa Kilometa 179 kwa kiwango cha lami unaendelea katika maeneo
mbalimbali Nchini.
73. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imedhamiria kujenga na kukamilisha ujenzi wa
Madaraja makubwa na ya kisasa mawili ambayo ni Daraja la Mto Malagarasi na
Daraja la Kigamboni. Ujenzi wa Daraja la Mto Malagarasi unaojumuisha ujenzi
wa Daraja kubwa lenye urefu wa Meta 200 na Madaraja mengine madogo katika Bonde
la Mto Malagarasi unaendelea vizuri. Hadi mwezi Machi 2013, Mkandarasi
amekamilisha ujenzi kwa Asilimia 85. Sambamba na hatua hiyo, taratibu
zimekamilika za kupata mkopo wa nyongeza kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa
Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiungo za Daraja
hilo zenye urefu wa Kilometa 37 kwa kiwango cha
lami.
74. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Daraja la Kigamboni lenye urefu wa Meta 680
linalojengwa kuunganisha eneo la Kurasini na Kigamboni katika Bahari ya Hindi,
tayari Mkandarasi amekamilisha kazi za maandalizi kwa Asilimia 90. Kazi ya
ujenzi wa Daraja la Kudumu na Barabara zake inatarajiwa kuanza wakati wowote
kuanzia sasa. Daraja hili linajengwa kwa Ubia kati ya Serikali na Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF). Lengo ni kukamilisha ujenzi wa Daraja hilo mwanzoni mwa
mwaka 2015.
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Serikali itajenga Barabara Kuu kwa kiwango cha
lami zenye urefu wa Kilometa 495 na kukarabati Barabara zenye urefu wa Kilometa
190 na Madaraja 11. Serikali pia, itajenga barabara za Mikoa za lami zenye urefu
wa Kilometa 54.3 na kukarabati Kilometa 855 kwa kiwango cha changarawe na
Madaraja 36. Aidha, matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum ya
Barabara Kuu na za Mikoa yataendelea kufanyika katika kipindi
kijacho.
USAFIRI WA BARABARA KATIKA JIJI LA DAR ES
SALAAM
76. Mheshimiwa Spika, msongamano wa magari katika barabara za Jiji la Dar es Salaam ni moja
ya changamoto ambayo Serikali inaendelea kuifanyia kazi. Jitihada zinazofanyika
kupunguza msongamano wa magari barabarani ni pamoja na kujenga miundombinu zaidi
ya barabara mpya za kuingia na kutoka katikati ya Jiji; kuanzisha usafiri wa
Treni ya Abiria; kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka
(DART); na kuimarisha usimamizi wa Sheria za Usalama
Barabarani.
77. Mheshimiwa
Spika, kuhusu ujenzi wa barabara mpya za kupunguza msongamano katika Jiji la
Dar es Salaam, hadi Machi, 2013 ujenzi wa Barabara ya kiwango cha lami yenye
urefu wa Kilometa 6.4 kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo - Kigogo hadi
mzunguko wa barabara ya Kawawa imekamilika na barabara yenye urefu wa Kilometa
2.7 kutoka barabara ya Kawawa – Bonde la Msimbazi hadi Makutano ya Jangwani na
Twiga imekamilika kwa Asilimia 70. Aidha, ujenzi wa Barabara yenye urefu wa
Kilometa 10.3 kutoka Jet Corner - Vituka hadi Davis
Corner imekamilika kwa Asilimia 90. Vilevile, utekelezaji wa Awamu ya
Kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka unaendelea ambapo kazi zilizofanyika
ni pamoja na ujenzi wa barabara za DART na za magari mchanganyiko na baiskeli
katika Barabara ya Morogoro, na ujenzi wa Miundombinu ya Mifumo ya Maji, Vituo
vya Mabasi na Madaraja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa
barabara nyingine za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na
ujenzi wa miundombinu ya DART.
HALI
YA UCHUKUZI
HUDUMA ZA USAFIRI WA RELI JIJINI DAR ES
SALAAM
78. Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2012, Serikali ilianzisha huduma ya usafiri wa treni ya
abiria Jijini Dar es Salaam kupitia Kampuni ya Reli (TRL) na TAZARA kwa lengo la
kukabiliana na tatizo la msongamano wa magari na abiria. Wastani wa idadi ya
Abiria wanaosafiri kwa Treni ya TAZARA ni 4,500 kwa siku na TRL ni Abiria 5,000.
Takwimu zinaonesha kuwa, Abiria 9,500 wanaosafiri kila siku kwa njia ya treni
wangehitaji kutumia mabasi zaidi ya 380 yenye uwezo wa kubeba Abiria 25 kila
moja. Kwa ujumla mwitikio wa wananchi wa kutumia huduma ya treni ya abiria ni
mkubwa ikilinganishwa na uwezo wa kutoa huduma hiyo. Kwa kuzingatia mahitaji
hayo makubwa, Serikali imeunda Kamati maalum ya wadau wa usafiri Jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kuchambua, kuanisha na kushauri mipango na mikakati ya
baadaye ya kuboresha huduma hiyo ili iwe endelevu na salama. Ni mategemeo yangu
kwamba Kamati hiyo itaandaa Mpango mzuri zaidi wa kupanua huduma hiyo muhimu kwa
Jiji la Dar es Salaam ambalo kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012 lina idadi ya watu Milioni 4.36, sawa na Asilimia 10 ya Wakazi wote
wa Tanzania Bara. Ongezeko hilo ni kubwa na hivyo linahitaji Mpango Kabambe wa
usafiri na usafirishaji.
USAFIRI WA RELI YA KATI NA
TAZARA
79. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya reli ya kati kwa
kujenga na kukarabati maeneo mbalimbali ili kuiwezesha kupitika wakati wote.
Pamoja na ukarabati huo, usanifu wa kina wa Mradi wa Uendelezaji
na Ujenzi wa Reli kutoka Dar es Salaam - Isaka - Keza - Kigali na Keza -
Musongati kwa kiwango cha Kimataifa umekamilika mwezi Februari 2013.
Serikali pia, imekamilisha mchakato wa kumpata Mshauri mwelekezi atakayefanya
upembuzi yakinifu wa kuinua kiwango cha reli kuwa katika kiwango cha kimataifa
kutoka Tabora hadi Kigoma, Kaliua hadi Mpanda na Isaka hadi Mwanza. Lengo ni
kuwezesha reli hiyo ifanane na inayotarajiwa kujengwa kutoka Dar es
Salaam-Isaka-Kigali/Musongati. Upembuzi Yakinifu wa reli ya kutoka Dar es Salaam
hadi Rwanda na Burundi na kutoka Arusha hadi Musoma unatarajiwa kuanza mwaka
2013/2014.
80. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa
kwamba mwezi Machi 2012, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China zilitia saini Itifaki ya 15 ya kuboresha Reli ya
TAZARA.
Tayari Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa jumla ya Shilingi
Bilioni 38.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyo chini ya Itifaki hiyo ambayo
inajumuisha kufanya upembuzi yakinifu wa kuboresha reli hiyo, kukarabati njia
ya reli, kununua vichwa vipya vya treni na kukarabati mabehewa ya
abiria. Hatua hizi zikikamilika zitaboresha kwa kiwango
kikubwa usafiri wa Reli ya TAZARA.
BANDARI
81. Mheshimiwa Spika, Serikali
inachukua hatua mbalimbali za kuongeza uwezo na ufanisi wa bandari zake kwa
kutekeleza Mpango Kabambe wa Mamlaka ya Bandari. Baadhi ya Miradi inayotekelezwa
chini ya Mpango huo ni Upembuzi Yakinifu kwa ajili ya kuimarisha na kuongeza
kina cha maji katika Gati Namba 1 hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam na
kuanza awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta. Mradi
mwingine ni kufanya Upembuzi Yakinifu wa ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhia
mizigo ya kwenda Nchi jirani katika eneo la
Kisarawe.
82. Mheshimiwa Spika, kutokana na nafasi ya Nchi
yetu kijiografia na ongezeko kubwa la biashara na uingizaji wa mizigo ya hapa
Nchini na Nchi jirani ambazo hazina bandari, uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam
kuhimili ongezeko hilo unapungua. Pamoja na jitihada zinazoendelea za kupanua
miundombinu ya bandari hiyo, Serikali imeona umuhimu wa kuwa na Bandari mpya ya
Bagamoyo ili isaidiane na Bandari zilizopo kukabiliana na ongezeko hilo. Tarehe
24 Machi 2013, Serikali ya Tanzania na China zimetia saini makubaliano ya
kujenga Bandari mpya ya Bagamoyo ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika Ukanda
wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati. Makubaliano hayo yanajumuisha pia ujenzi wa
eneo huru la biashara na miundombinu mingine muhimu ikiwemo reli
itakayounganisha Bandari ya Bagamoyo na Reli ya Kati na ya TAZARA pamoja na
barabara ya lami kutoka Bagamoyo hadi Mlandizi. Huu ni mradi mkubwa na wa
kimkakati ambao utabadili kabisa mfumo wa uendeshaji wa Bandari na usafirishaji
Nchini.
USAFIRI WA ANGA
83. Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza kwa mafanikio Awamu ya Kwanza ya Uboreshaji
na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Tabora, Kigoma na Bukoba. Ujenzi wa barabara
ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami katika kiwanja cha Ndege cha
Tabora umekamilika na kazi za ujenzi zinazoendelea katika kiwanja cha Kigoma
zinatarajiwa kumalizika mwezi Juni 2013. Kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha
Bukoba, ukarabati wa njia ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami
unaendelea. Aidha, Kiwanja kipya cha Kimataifa cha Songwe, Mbeya kilianza kutoa
huduma tarehe 13 Desemba, 2012. Kiwanja hicho ambacho kijiografia kipo karibu na
Nchi za Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Nchi nyingine za
Kusini mwa Afrika ni kichocheo muhimu cha shughuli za uchumi na kijamii zikiwemo
utalii na kilimo hasa cha matunda, mbogamboga na maua kwa Mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini. Ni muhimu sana wananchi wa maeneo hayo na mengine wahamasishwe na
kujipanga kutumia fursa za kiuchumi zitakazoambatana na kukamilika kwa kiwanja
hicho.
84. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Upanuzi na Uboreshaji
wa Viwanja vya Ndege. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na Upembuzi Yakinifu na
usanifu wa kina wa ukarabati kwa kiwango cha lami wa njia za kuruka na kutua
ndege kwa viwanja vya Iringa, Kilwa Masoko, Ziwa Manyara, Musoma, Mtwara,
Njombe, Songea, Singida na Tanga.
MAENDELEO YA SEKTA YA ELIMU
ELIMU YA MSINGI
85. Mheshimiwa
Spika, Serikali ilianza kutekeleza Programu kubwa za
kuendeleza elimu Nchini mwaka 2001 kwa lengo la kuongeza idadi ya Wanafunzi wa
rika lengwa wanaojiunga na shule na kuboresha elimu. Utekelezaji wa Awamu ya
Kwanza na ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM I & II)
umeleta mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, kuandikisha
Wanafunzi wa rika lengwa na kupunguza pengo la uandikishaji kati ya Wanafunzi wa
Kike na wa Kiume. Mafanikio hayo yaliambatana na changamoto za upungufu wa
Walimu, Vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na madawati. Kwa kutambua
changamoto hizo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 inaelekeza Serikali
kulinda mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka msisitizo mkubwa katika ubora
wa elimu.
86. Mheshimiwa
Spika, ili kuendeleza kasi tuliyoanza nayo, Serikali
inatekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM III)
unaolenga kuboresha elimu kwa kuongeza idadi ya Walimu, vitabu vya ziada na
kiada na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Jitihada za
Serikali za kuajiri walimu zinaendelea ambapo Walimu wapya 13,568 wameajiriwa
katika Shule za Msingi mwaka 2012/2013. Serikali itaendelea kuweka msisitizo
katika kuboresha Elimu ya Msingi Nchini kwa kuzingatia manufaa makubwa
yanayopatikana katika ngazi hiyo muhimu ya elimu.
ELIMU YA SEKONDARI
87. Mheshimiwa
Spika, mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Msingi Nchini ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi
ya wahitimu wanaofaulu ngazi hiyo, yameongeza mahitaji ya nafasi zaidi katika
Shule za Sekondari. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilianza kutekeleza Mpango
wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) mwaka 2006. Mpango huo umesaidia sana
kukabiliana na changamoto ya nafasi zaidi katika Shule za Sekondari kwa kujenga
Shule nyingi za Sekondari na hivyo kuwa na wanafunzi wengi zaidi. Ni dhahiri
kuwa ongezeko hilo la Wanafunzi lilihitaji Walimu wengi zaidi, Maabara,
Vitabu na Vifaa vingine muhimu. Aidha, Serikali iligatua usimamizi wa Shule za
Sekondari kutoka Serikali Kuu kwenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili
kuboresha usimamizi wa shule hizo pamoja na kuanzisha programu kabambe ya
kufundisha walimu zaidi ili wafundishe katika shule zinazoongezeka. Katika mwaka
2012/2013, Serikali imeajiri jumla ya Walimu 12,969 ambao watafundisha katika
Shule mbalimbali za Sekondari Nchini. Hatua hizo zote ni uwekezaji mkubwa ambao
matokeo yake yatawezesha kuboresha elimu Nchini hatua kwa
hatua.
88. Mheshimiwa
Spika, sote tumehuzunishwa sana na matokeo
yasiyoridhisha ya mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2012. Matokeo hayo siyo
tu kwamba yamewahuzunisha wazazi ambao wamewekeza rasilimali kwa Watoto wao bali
pia Serikali ambayo imetumia rasilimali nyingi kwenye Sekta ya Elimu. Huu siyo
wakati wa kulaumiana ama kutafuta mchawi wa matokeo hayo yasiyoridhisha. Ni
lazima tutafute suluhisho, kusonga mbele na kubuni mikakati na hatua za haraka
za kusaidia Watoto hao ambao wamepata matokeo mabaya. Tumeanza kwa kuunda Tume
yenye Watu makini ambayo itachunguza chanzo cha matokeo hayo mabaya na kutoa
mapendekezo ya namna ya kutatua tatizo hilo katika muda mfupi, kati na mrefu na
pia kupendekeza suluhisho la haraka kwa wale waliopata daraja la IV na sifuri.
Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba, matokeo ya
Tume hiyo yatawekwa bayana na hatua zitakazopendekezwa zenye lengo la kuimarisha
elimu Nchini zitachukuliwa. Hata hivyo, ni vyema tukumbuke kwamba, sote tuna
wajibu wa kutoa mwongozo na mapendekezo yatakayosaidia kutoka hapa tulipo.
Wazazi, Wanafunzi na Jamii nzima wana nafasi yao pia katika kuboresha elimu ya
Nchi hii. Hili siyo suala la Serikali
pekee.
ELIMU MAALUM
89. Mheshimiwa
Spika, Serikali inaendelea kuweka msukumo wa kipekee katika kutoa Elimu
Maalum kwa watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye Ulemavu wa Ngozi, Uoni
Hafifu na Usikivu. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imeandaa Mwongozo wa
kufundishia Wanafunzi wenye Ulemavu wa Ngozi na Uoni Hafifu. Aidha, Serikali
imenunua na kusambaza vifaa maalum na visaidizi vya kufundishia na kujifunzia
kuanzia ngazi ya Elimu ya Awali hadi Chuo Kikuu. Kazi nyingine zilizofanyika ni
kukarabati na kujenga majengo rafiki kwa walemavu katika Chuo cha Ualimu
Patandi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa Elimu
Maalum hususan baada ya kupata takwimu sahihi za walemavu kutokana na Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012.
ELIMU YA JUU
90. Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa
Elimu ya Juu kwa kupanua na kuongeza Taasisi za Elimu ya Juu za Serikali na
Binafsi.Katika kipindi
takribani cha miaka 8 idadi ya wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Elimu ya Juu Nchini
imeongezeka kutoka 40,993 mwaka 2005/2006 hadi 166,484 mwaka 2012/2013, sawa na
ongezeko la Asilimia 306. Serikali pia, inatoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vya
Elimu ya Juu vya Umma na vile vya Mashirika ya Dini na vya Sekta Binafsi. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali imetoa mikopo ya Shilingi
Bilioni 345 kwa wanafunzi 98,772 ikilinganishwa na mikopo ya Shilingi Bilioni
291 kwa wanafunzi 93,784 mwaka 2011/2012.
91. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea
kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya Mikopo ya Elimu ya Juu na kuimarisha
usimamizi wa urejeshaji wa mikopo ili wanafunzi wengi zaidi waweze kunufaika.
Nitumie fursa hii kuwakumbusha wale wote walionufaika na mikopo ya elimu ya juu
kulipa mikopo hiyo yenye masharti nafuu sana ili wanafunzi zaidi waweze
kunufaika nayo. Aidha, waajiri watimize wajibu wao kwa kuwataka waajiriwa
walionufaika kulipa mikopo hiyo. Vilevile, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
iongeze kasi ya kukusanya madeni na kuchukua hatua stahiki kwa wale wasiolipa
kwa mujibu wa Sheria.
MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA
VITUO VYA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA
NCHINI
92. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeweka jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba Vituo vya
Utoaji wa Huduma za Afya katika ngazi zote Nchini vinapatiwa dawa muhimu na
vifaa vya Teknolojia ya kisasa vya kuchunguza na kutibu magonjwa. Katika mwaka
2012/2013, Serikali imenunua Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na vitendanishi na
kuvisambaza kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zote za Serikali
Nchini. Serikali pia, imeongeza uwezo wa ndani wa kutibu maradhi mbalimbali.
Mathalan, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imewezeshwa kutoa huduma za Afya za
ubingwa wa juu ikiwa ni pamoja na upasuaji wa moyo ambapo hadi sasa zaidi ya
Wagonjwa 450 wamepatiwa huduma hiyo. Vilevile, huduma ya usafishaji damu
kwa Wagonjwa wa figo na Upasuaji kupitia tundu dogo pamoja na uchunguzi wa
magonjwa kwa kutumia mashine za kisasa unafanyika hapa Nchini. Hatua hiyo
imewezesha Serikali na Wananchi kuokoa fedha nyingi zinazotumika kupeleka
wagonjwa kutibiwa nje ya Nchi. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Madaktari,
Wauguzi na Wataalam wengine wa Afya kwa kuliwezesha Taifa letu kupiga hatua
kubwa katika kutibu magonjwa hayo na mengine yanayohitaji utaalam na ubingwa wa
hali ya juu.
93. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeimarisha huduma ya tiba ya saratani Nchini kwa
kukamilisha ujenzi wa Jengo la kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Saratani
ya Ocean Road na hivyo kuongeza uwezo wake kutoka vitanda 120 hadi 270.
Aidha, Serikali imesogeza huduma ya tiba ya saratani karibu na Wananchi kwa
kukamilisha ujenzi wa Jengo Maalum la kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya
Bugando. Hatua hiyo itapanua wigo wa kutoa huduma ya tiba ya saratani na
kupunguza msongamano wa Wagonjwa wa saratani kutoka Mikoa mbalimbali waliokuwa
wanalazimika kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Saratani yaOcean
Road Jijini Dar es Salaam.
UDHIBITI WA MAAMBUKIZI YA MALARIA NA
UKIMWI
94. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012, Serikali ilifanya Utafiti kuhusu Viashiria vya
UKIMWI na Malaria. Taarifa ya matokeo ya utafiti huo inaonesha kuwa kiwango cha
Malaria Nchini kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kimepungua kutoka
Asilimia 18 mwaka 2007 hadi Asilimia Tisa mwaka 2012. Hali hii imechangiwa zaidi
na ongezeko kubwa la matumizi ya Vyandarua vilivyowekwa Viuatilifu vya muda
mrefu ambapo zaidi ya Vyandarua milioni 34 vimesambazwa katika Kaya zenye Watoto
walio na umri chini ya miaka mitano na Wanawake Wajawazito. Kutokana na
usambazaji huo, matumizi ya Vyandarua yameongezeka kutoka Asilimia 26 mwaka 2007
hadi Asilimia 72 mwaka 2012 kwa Watoto wenye umri chini ya miaka Mitano. Kwa
Wanawake Wajawazito, matumizi ya Vyandarua yameongezeka kutoka Asilimia 27 mwaka
2007 hadi Asilimia 75 mwaka 2012. Ni dhahiri kupungua kwa kiwango cha Malaria
Nchini ni jitihada za kipekee za Serikali ya Awamu ya Nne kwa kushirikiana na
Wananchi na Washirika wa Maendeleo kupitia Kampeni mbalimbali za Kudhibiti
Malaria.
95. Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Wananchi na
Wadau wote walioshirikiana na Serikali katika kupata mafanikio haya ambayo
yanatokana na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria Nchini na
Mpango wa Hati Punguzo kwa Wanawake Wajawazito ulioanza kutekelezwa mwaka 2008
hadi 2012. Natoa wito kwa Wananchi wote kuendeleza juhudi za Kujikinga na
Malaria, hususan kwa kutumia Vyandarua vyenye Viuatilifu vya muda mrefu na
kutokomeza Mazalia ya Mbu.
96. Mheshimiwa Spika, juhudi za Serikali za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI Nchini pia
zimeanza kuzaa matunda. Kwa mujibu wa Utafiti wa mwaka 2011 - 2012 wa Viashiria
vya Malaria na UKIMWI, maambukizi ya Virusi vya UKIMWI yamepungua kutoka
Asilimia 5.7 mwaka 2007/2008 hadi Asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 kwa wanawake na
wanaume wa umri wa miaka 15 - 49. Ili kuendelea kupunguza kasi ya maambukizi ya
UKIMWI Nchini, Serikali inaendelea kutoa
elimu ya UKIMWI; kutoa ushauri nasaha na kuhamasisha upimaji wa hiari.
Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaanza kutekeleza Mkakati Mpya wa Taifa
wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013 hadi 2017 unaolenga kuwa na Sifuri tatu, yaani Kutokuwa na
Maambukizi Mapya; Kukomesha Vifo Vitokanavyo na UKIMWI na Kuondoa Kabisa
Unyanyapaa na Ubaguzi. Lengo hilo litatimia iwapo sote tutabadili tabia
zinazosababisha maambukizi mapya.
LISHE
97. Mheshimiwa
Spika, Serikali inachukua hatua thabiti za kupambana na utapiamlo hususan
udumavu unaoathiri watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Katika hotuba yangu
ya mwaka 2012/2013 nilieleza kwamba Serikali imezindua Mkakati wa Kitaifa wa
Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015. Mkakati huo umeanza kutekelezwa kwa
kuandaliwa Mpango wa Utekelezaji ulioainisha gharama na majukumu ya kila mdau
katika kupunguza Utapiamlo Nchini. Pamoja na mambo mengine, Mpango huo
umesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu lishe bora hasa kwa mama
wajawazito na watoto wachanga, kuongeza viini lishe kwenye vyakula pamoja na
kuingiza masuala ya lishe kwenye Sera na Mipango mbalimbali ya Serikali. Tayari
hatua zimechukuliwa ambapo masuala ya lishe yameingizwa kwenye Mpango wa Taifa
wa Uwekezaji katika Kilimo na Chakula (Tanzania Agriculture and Food Security
Investment Plan - TAFSIP). Vilevile, Serikali inaendelea na zoezi la kuhuisha
Sera ya Usalama wa Chakula na Lishe ya mwaka 1992 ili iendane na Mkakati wa
Taifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015.
98. Mheshimiwa Spika, tunayo kazi kubwa mbele
yetu ya kupambana na tatizo la lishe duni katika maeneo yote Nchini. Takwimu
zinabainisha kwamba, hakuna tofauti kubwa ya kiwango cha udumavu katika Mikoa
inayozalisha chakula kwa wingi na ile yenye uhaba wa chakula. Napenda
kusisitiza tena kwamba hali ya udumavu humtokea mtoto katika siku elfu moja za
kwanza za uhai wake, yaani tangu kutungwa mimba hadi umri wa miaka miwili.
Hivyo, tunahitaji kuimarisha utoaji elimu ya lishe kwa Wajawazito na Mama
wanaonyonyesha ili wapate mlo kamili na kunyonyesha watoto wao kikamilifu
hususan miezi sita ya mwanzo tangu kuzaliwa. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge
zaidi kujiunga na Kikundi cha Wabunge kinachohamasisha umuhimu wa Lishe Bora ili
kuongeza kasi na chachu ya kutoa elimu ya lishe katika maeneo yetu ya
uwakilishi.
HALI YA UPATIKANAJI MAJI NCHINI
HUDUMA YA MAJI VIJIJINI
99. Mheshimiwa
Spika, upatikanaji wa maji ya uhakika na ya kutosha
kwa wananchi Vijijini bado ni changamoto inayohitaji nguvu zaidi na mbinu mpya
kwa kuzingatia ongezeko kubwa la watu pamoja na mabadiliko ya Tabianchi. Katika
kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imetenga na kupima maeneo ya
vyanzo vya maji na kuyawekea mipaka ili kuzuia uchafuzi na uharibifu wa vyanzo
hivyo. Aidha, Vituo mbalimbali vya kuchotea maji vimeainishwa katika
Halmashauri 122 na kuwekwa kwenye ramani ili vifahamike. Ujenzi wa miradi mipya,
upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji Vijijini pia umefanyika katika
maeneo mbalimbali ili kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi. Kutokana na
juhudi hizo, idadi ya Wananchi wanaoishi Vijijini ambao wanapata huduma ya
majisafi, salama na ya kutosha karibu na makazi imeongezeka kutoka watu Milioni
16.3 mwaka 2006 hadi Milioni 20.6 mwaka 2012.
HUDUMA YA MAJI MIJINI
100. Mheshimiwa Spika, huduma ya Maji Mijini
inasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka 19 za Majisafi na Usafi wa Mazingira
katika Miji Mikuu ya Mikoa, Mamlaka 109 katika ngazi za Wilaya, Miji Midogo
na Miradi ya Maji ya Kitaifa. Serikali kupitia Mamlaka hizo imeongeza
kiwango cha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Miji hiyo kutoka Asilimia 84 mwaka
2010/2011 hadi Asilimia 86 mwaka 2011/2012. Katika Jiji la Dar es Salaam,
Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa kupanua uwezo wa mtambo wa
maji wa Ruvu Chini ambapoujenzi umefikia Asilimia 85.
Kazi ya kulaza bomba kuu la pili lenye kipenyo cha Meta 1.8 na urefu wa km 55.5, kutoka
Ruvu Chini hadi kwenye matanki ya kuhifadhia maji yaliyopo eneo la Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam inatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2014.
Aidha, kazi ya usanifu wa Mradi wa Kuchimba Visima Virefu 12 katika maeneo ya
Kimbiji na Visima 8 katika eneo la Mpera imekamilika na Wananchi
waliohamishwa wamelipwa fidia. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea kukarabati na kujenga miradi ya maji Mijini na Vijijini pamoja na
kujenga mabwawa kwa ajili ya matumizi ya majumbani na mifugo hususan katika
maeneo kame.
TAWALA
ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
UANZISHAJI WA MAENEO MAPYA YA
UTAWALA
101. Mheshimiwa
Spika, Serikali imekamilisha taratibu za kuanzisha Halmashauri Mpya 31 ili
kusogeza huduma karibu na Wananchi. Halmashauri hizo ni Jiji la Arusha, Manispaa
ya Ilemela, Manispaa ya Lindi na Halmashauri za Miji ya Kahama, Masasi,
Makambako, Geita na Bariadi. Vilevile, imeanzisha Halmashauri za Wilaya ya
Kalambo, Busega, Nsimbo, Bumbuli, Mlele, Ushetu, Msalala, Momba, Mbogwe, Kyerwa,
Busokelo na Buhigwe. Halmashauri nyingine zilizoanzishwa ni Nyangh’wale,
Wanging’ombe, Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Kakonko, Itilima, Uvinza, Ikungi na
Kaliua. Serikali itaendelea kuzipatia Halmashauri mpya vitendea kazi, Watumishi
pamoja na kujenga miundombinu muhimu hatua kwa hatua.
MASUALA
MTAMBUKA
VITA DHIDI YA RUSHWA
102. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kwa
kuelimisha Umma kuhusu athari za Rushwa, kuziba mianya ya rushwa na kuwasihi
Wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa. Aidha, Vyombo vya Dola
vimechunguza tuhuma za makosa ya Rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya
Vyombo vya Kisheria. Hadi kufikia Desemba 2012, tuhuma 2,911 zilichunguzwa
ambapo uchunguzi wa tuhuma 390 umekamilika na Kesi
121 zimefunguliwa Mahakamani. Katika mwaka 2013/2014, TAKUKURU itaendelea na uchunguzi wa tuhuma zilizopo na mpya zitakazojitokeza,
kuendesha Kesi nyingine zilizopo Mahakamani na zitakazoendelea kufunguliwa
kutokana na kukamilika kwa chunguzi mbalimbali. Serikali pia itaendelea kutoa
elimu kwa umma kuhusu athari za rushwa.
MAAFA
103. Mheshimiwa
Spika, changamoto kubwa iliyoikumba Nchi yetu kwa mwaka 2012/2013 ni ukame
uliosababisha upungufu mkubwa wa Chakula katika baadhi ya maeneo
Nchini. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilifanyaTathmini za kina za Hali ya
Chakula na Lishe Nchini na kubaini kwamba Watu 1,615,440 katika Halmashauri 47
Nchini wanahitaji msaada wa chakula. Katika kukabiliana na hali hiyo, kuanzia
mwezi Julai 2012 hadi Machi 2013, Serikali imetoa Tani 69,452 za chakula cha
msaada chenye thamani ya Shilingi Bilioni 26.39 kwa walengwa katika maeneo yenye
upungufu. Serikali pia imetoa Shilingi Bilioni 4.6 kwa ajili ya usafirishaji wa
chakula hicho.
104. Mheshimiwa
Spika, katika kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika wa Mabomu eneo la
Gongolamboto, Serikali imekamilisha ujenzi wa Nyumba 36 eneo la Msongola
Wilayani Ilala na Nyumba moja eneo la Mbweni Wilayani Kinondoni. Zoezi
hilo kwa ujumla limegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.75. Nyumba hizo ambazo
zimewekewa huduma za msingi za maji na umeme zilikabidhiwa kwa walengwa na
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
tarehe 11 Desemba 2012.
105. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mafuriko yaliyotokea Dar es Salaam mwezi Desemba
2011 yalisababisha Kaya 1,007 za waathirika waliokuwa wanaishi katika
maeneo hatarishi zaidi kuhamishiwa katika eneo la Mabwepande Wilayani Kinondoni.
Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuwapatia huduma mbalimbali za
kijamii na kuwajengea miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji, umeme,
shule, zahanati na Kituo cha Polisi. Aidha, hivi karibuni Serikali imetoa
Mifuko 100 ya Saruji kwa kila Kaya ili kuziwezesha kujenga nyumba bora na za
kudumu. Napenda kutoa wito kwa Wananchi ambao bado wanaishi mabondeni kuhama ili
kuepuka athari zinazoweza kuwapata. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini
ziendelee kutenga maeneo yenye usalama kwa ajili ya kuwahamisha wananchi
wanaokaa katika maeneo hatarishi.
DAWA ZA KULEVYA
106. Mheshimiwa
Spika, biashara na matumizi ya Dawa haramu za Kulevya bado ni tatizo Nchini.
Hali hii inadhihirishwa na idadi kubwa ya watumiaji walio mitaani na wale
wanaojitokeza kupata tiba. Hata hivyo, kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa
na Serikali kwa kutumia Kikosi Kazi Maalum cha Kitaifa cha Udhibiti wa Dawa za
Kulevya, jumla ya Kilo 255 za Heroin na Kilo 151 za Cocaine zilikamatwa mwaka
2012 na Watuhumiwa 45 walikamatwa. Vilevile, jumla ya Ekari
184 za Mashamba ya Bangi na Kilo 3,200 za Bangi kavu ziliteketezwa na Kilo 4,840
za mirungi zilikamatwa. Katika kipindi hicho, Waathirika wa
Dawa za Kulevya wapatao 20,426 walijitokeza katika Vituo mbalimbali vya
tiba. Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe imekuwa ikipokea
wastani wa Waathirika 400 kila mwaka.
107. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
itakamilisha Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini na kuandaa
Mkakati wake wa Utekelezaji. Serikali pia itaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya
madhara ya Dawa za Kulevya na kupanua huduma za matibabu kwa waathirika wa Dawa
za Kulevya. Wito wangu kwa jamii nzima ni kuendelea kupambana kwa nguvu
zote na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kunusuru vijana
wetu. Wasafirishaji na watumiaji wa dawa hizo tunaishi nao mitaani na ni wajibu
wa kila mmoja wetu kuwabaini na kutoa taarifa katika Vyombo vya
Dola.
USTAWISHAJI MAKAO MAKUU DODOMA
108. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2012/2013, Serikali imeendelea
kuimarisha miundombinu ya Manispaa ya Dodoma kwa kujenga barabara zenye jumla ya
Kilometa 20.6 kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu
na Area A. Aidha, imekarabati mtandao wa maji wenye urefu wa Kilometa 17.5 na
kusambaza umeme wa msongo mkubwa wenye urefu wa Kilometa 13.5 katika eneo la
uwekezaji la Njedengwa. Vilevile, Viwanja 1,098 vimepimwa katika maeneo ya
Ndachi, Ilazo C-centre, Nala Mizani, Mwangaza, Ipagala, Kizota Relini pamoja na
lyumbu New Town Centre.
109. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa Barabara
kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu na Area A.
Vilevile, itaendelea na ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami, usambazaji wa
umeme wa msongo mkubwa pamoja na
usambazaji wa mabomba ya maji safi katika eneo la Uwekezaji la Njedengwa. Pia, itapima Viwanja vipya 4,476 katika maeneo
ya Nzuguni, Mkonze, Ndachi na maeneo ya Viwanda. Pamoja na kazi hizo, kazi
iliyoanza ya kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma
itaendelea.
HITIMISHO
110. Mheshimiwa Spika, nimeelezea kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali imetekeleza
kwa kipindi kilichopita. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazofanyika mwaka
2013/2014. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo machache
yafuatayo:
a) Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012 yameonesha kuna ongezeko la watu Milioni 10.1 kutoka watu Milioni
34.4 mwaka 2002 hadi Milioni 44.5 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Asilimia 30.
Ni dhahiri ongezeko hilo kubwa linahitaji juhudi za pamoja kati ya Serikali,
Sekta Binafsi, Wadau wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla kuongeza uwekezaji
katika huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Rai yangu kwenu ni kuzitumia
takwimu hizo kikamilifu katika kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu
wetu.
b) Tumebakiza miaka takribani 12 kabla
ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, miaka miwili kufikia
malengo ya Maendeleo ya Milenia na miaka miwili ya kukamilisha utekelezaji wa
Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano. Mfumo mpya ulioanzishwa na Serikali wa
kufuatilia na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kipaumbele na
kufanya tathmini ya mara kwa mara ya kupima matokeo utasaidia kuharakisha
kufikiwa kwa malengo hayo mapema. Serikali itahakikisha kwamba Mfumo huo
unaimarisha uwajibikaji na kuleta matokeo makubwa na ya haraka katika kipindi
kifupi.
c) Jitihada za Serikali ya Awamu ya Nne
katika kuvutia uwekezaji katika kilimo hususan katika Ukanda wa Kilimo wa Kusini
mwa Tanzania (SAGCOT) zimeleta mwamko na matumaini makubwa. Azma ya Serikali ni
kuona kwamba Wawekezaji wakubwa wanashirikiana kwa karibu na wakulima wadogo ili
waweze kuondoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha kisasa
chenye tija na cha kibiashara. Nawahakikishia Watanzania wote kwamba upatikanaji
wa ardhi iliyopimwa kwa ajili ya Mkulima mdogo ndicho kipaumbele cha
Serikali.
d) Mchakato wa kuandaa Katiba Mpya
umeingia katika hatua ya kuunda Mabaraza ya Katiba katika ngazi mbalimbali
yatakayopitia Rasimu ya Katiba Mpya na kutoa maoni. Tume baada ya kuzingatia
maoni ya Mabaraza itaandaa Rasimu ya Katiba Mpya itakayowasilishwa katika Bunge
Maalum la Katiba. Natoa wito kwa wananchi watoe ushirikiano kwa Tume iweze
kukamilisha zoezi hilo muhimu kwa ufanisi na kwa
wakati.
e) Amani iliyopo Nchini imetujengea
heshima kubwa katika Bara la Afrika na Duniani kote. Sote tuna wajibu wa kuienzi
na kuisimamia isitoweke. Serikali ya awamu ya Nne itahakikisha kwamba Amani na
umoja wa Kitaifa vinadumishwa ili kuwawezesha Wananchi kuendelea kufanya
shughuli zao za maendeleo bila hofu. Serikali haitavumilia kuona mtu au kikundi
cha watu wenye dhamira mbaya wakivuruga Amani, Umoja na Mshikamano uliopo Nchini
kwa kisingizio chochote. Sote tuna wajibu wa kuheshimu utawala wa Sheria, Kanuni
na Taratibu zilizopo.
111. Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman
Ghasia (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika katika mwaka 2012/2013 na
Mwelekeo wa Kazi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2013/2014.
SHUKRANI
112. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa
ushirikiano walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru Watumishi wote wa
Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
Ombeni Yohana Sefue kwa kusimamia Shughuli za Serikali vizuri. Nawashukuru
Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo kwa michango yao ambayo
imewezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa
Wananchi.
113. Mheshimiwa Spika, vilevile,
napenda kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang,
Waziri wa Nchi (Uwezeshaji na Uwekezaji); Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi,
Mbunge wa Ismani, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa Aggrey Joshua Mwanry, Mbunge wa Siha, Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na
Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) kwa ushirikiano
walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru
pia Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa jitihada walizoonesha katika kipindi
hiki. Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya
Uongozi wa Katibu Mkuu, Bwana Peniel Moses Lyimo na Kaimu Katibu Mkuu, Bwana
Jumanne Abdallah Sagini kwa kazi nzuri wanayoifanya. Niwashukuru Naibu Makatibu
Wakuu, Bwana Charles Amos Pallangyo, na Bwana Alphayo Japan Kidata kwa ushauri
wao wa Kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika
kipindi hiki. Nawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya
Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka
2013/2014.
114. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na maelekezo
anayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Pia ninamshukuru Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa ushirikiano wao mkubwa. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa
Wabunge, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano
wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Niwashukuru sana Wapiga Kura wangu
wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano wanaonipa katika kuleta maendeleo ya Jimbo
letu. Nawashukuru sana!
115. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, naomba uniruhusu kutumia fursa hii kumshukuru sana
Mama Tunu Pinda na Familia yangu yote kwa kunitia moyo, kunivumilia kwa kila
hali na kunipa nguvu katika utekelezaji wa majukumu yangu ya
Kitaifa. Nawashukuru sana!!
MAKADIRIO
YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU -
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA
2013/2014
MUHTASARI
116. Mheshimiwa
Spika, kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu
likubali kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2013/2014 ya jumla
ya Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Tatu, Milioni Mia Nne na Moja, na
Hamsini na Tisa Elfu (123,401,059,000); kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, na
jumla ya Shilingi Trilioni Nne, Bilioni Mia Mbili Ishirini na Sita, Milioni
Mia Moja Ishirini na Tatu, Mia Tisa Hamsini na Nne Elfu na Mia Nane na
Mbili(4,226,123,954,802) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi
ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni Matumizi ya
Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla
wake.
117. Mheshimiwa
Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo
yanafafanua kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zake, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Ofisi ya Bunge.
118. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa
Hoja.
Post a Comment