Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jana, Jumatano, Aprili 10,
2013 ametia saini Kitabu cha Maombolezo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza,
Bi. Margaret Thatcher ambaye alifariki dunia Jumatatu wiki hii kwa ugonjwa wa
kiharusi akiwa na umri wa miaka 87.
Rais Kikwete ametia
saini Kitabu hicho kwenye Ubalozi wa Uingereza katika Tanzania ulioko Jengo la
Umoja mjini Dar es Salaam.
Rais alikaribishwa
kwenye Ubalozi huo na Balozi wa Uingereza katika Tanzania, Mheshimiwa Bi. Dianna
Melrose na wafanyakazi wengine wa ubalozi huo na amekwenda moja kwa moja kutia
saini kitabu hicho mara baada ya kuwasili kwenye Ubalozi huo.
Mara baada ya kumaliza
kutia saini Kitabu hicho, Balozi Melrose amemwambia: “Kwa niaba ya Serikali ya
Uingereza na Watu wa Uingereza nakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa heshima hii
ya kuja kutia saini Kitabu cha Maombolezo cha Mheshimiwa Margaret Thatcher.
Waziri Mkuu wa nchi yetu atafurahi kujua kuwa umepata muda wa kuja kuungana nasi
katika kuomboleza kifo hiki.”
Naye Mheshimiwa Rais
Kikwete amemjibu: “Kwa mara nyingine Mheshimiwa Balozi nakupa wewe binafsi,
Serikali na watu wa Uingereza pamoja na familia ya Bi. Margaret Thatcher salamu
zetu nyingi za rambirambi kufuatia msiba huu. Bi.Thatcher alikuwa kiongozi
mashuhuri. Alikuwa kiongozi mwenye nguvu na msimamo na ndiyo maana anaheshimiwa
na sisi sote.”
Bi. Margaret Thatcher
alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa miaka 11 kati ya 1979 na 1990. Alikuwa
mwanamke wa kwanza na pekee mpaka sasa kushikilia nafasi hiyo na ndiye alikuwa
Waziri Mkuu wa kwanza kukaa madaraka kwa muda mrefu zaidi kuliko waziri mkuu
mwingine yoyote katika kipindi cha miaka 150.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
10 Aprili,
2013
Post a Comment