| Dk Seif Seleman Rashid. |
Mama wa mtoto aliyetelekezwa anawajibika
kuwasilisha shauri la matunzo ya mtoto katika vyombo vya
sheria.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Seleman Rashid wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Anna Mallac (Chadema) aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwawajibisha wageni wanaowazalisha wanawake na kuwatelekeza ili kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na kupunguza wimbi la watoto wa mitaani.
Naibu
Waziri alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009, kifungu cha
43, mama wa mtoto aliyetelekezwa anawajibika kuwasilisha shauri la matunzo ya
mtoto katika vyombo vya sheria.
Alifafanua
“Wizara yangu kama msimamizi na mtekelezaji mkuu wa sheria hii baada ya kupokea
mashauri ya aina hiyo hufanya mawasiliano na Wakala wa Kimataifa wa Huduma za
Jamii ili kuweza kufanya uchunguzi na ufuatiliaji katika upande wa mlalamikiwa
ambaye ndiye anayedhaniwa kuwa baba wa mtoto”.
Baada ya
uchunguzi huo inapothibitishwa pasipo shaka kuwa mlalamikiwa ndiye baba halisi
wa mtoto husika , taratibu za malezi , matunzo na ulinzi wa mtoto huyo hufanywa
kwa kutumia ofisi za balozi za nchi husika.
Mbunge
huyo wa Viti Maalumu, ambaye alisimama tena kwa swali la nyongeza alilielezea
Bunge kuwa raia wa China na Uingereza wanaofanya shughuli za ukandarasi wa
ujenzi wa barabara vijijini na kwenye machimbo wamewazalisha wanawake vijijini
watoto na kisha kuwatelekeza na kurudi katika nchi zao.
“Wanawake
hao wanahangaika na watoto wao weupe wamechakaa utawaona wameshikilia muhindi
huku baba zao Wachina na Waingereza waliowazalisha wamerudi kwao je, Serikali
haioni sasa itoe elimu kwa wanawake hao ili waweze kwenda kupata haki zao,”
alihoji Mbunge huyo.
Hata
hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alimtaka
mbunge huyo na wananchi wengine kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuzuia mimba
zisizohitajika.
Katika
kuelezea suala la ulinzi Naibu Waziri Afya na Ustawi wa Jamii alisema katika
kuhakikisha haki za watoto walio katika mazingira hatarishi hususan watoto
waliotelekezwa, wanaonyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili zinalindwa,
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau wa maendeleo imeanzisha
programu ya ulinzi na usalama wa mtoto ambapo mifumo ya ulinzi na usalama wa
watoto imeimarishwa kwa kuundwa timu za ulinzi katika ngazi ya halmashauri, kata
na vijiji na mitaa.
“Hadi sasa
mifumo ya ulinzi na usalama imeanzishwa katika halmashauri za Hai, Magu, Kasulu,
Temeke, Nyamagana, Ilemela, Kinondoni, Ilala, Musoma na Bukoba. Timu hizo
hujumuisha wataalamu mbalimbali wanaohusika na ulinzi wa watoto wakiwemo maofisa
ustawi wa jamii,” alisema.
Alisema
katika mwaka wa fedha 2013/2014 programu ya ulinzi na usalama itasambazwa katika
halmashauri 25 hivyo kupitia programu hiyo matukio ya unyanyasaji, utelekezaji
na ukatili kwa watoto utazuiwa na kushughulikiwa ipasavyo.



Post a Comment