Katika hali isiyo ya kawaida kwa
akinababa wengi nchini, mkazi wa Naliendele, mkoani Mtwara, Salum Abdalah,
akihudhuria kliniki na mtoto wake, katika kituo cha afya cha Naliendele mkoani
humo jana kwa lengo la kufuatilia maendeleo ya afya ya mtoto, Zahanati hiyo ni
miongoni mwa zilizonufaika na msaada wa mashine za kisasa ‘sms printers’
zinazowezesha mchakato wa upimaji na upatikanaji wa majibu ya VVU kwa haraka kwa
watoto wachanga.
Mratibu wa
Uchunguzi wa VVU kwa Watoto Wachanga wa EGPAF, Georgiah Kasori, (kulia) akipewa
maelezo na Meneja wa Maabara wa mkoa wa Mtwara, Joachim Mrope ya jinsi mashine
‘sms printer’ zinazowezesha upimaji na upatikanaji wa majibu ya VVU kwa haraka
kwa watoto wachanga zinavyofanya kazi kwenye maabara ya hospitali hiyo jana.
Mganga Mkuu wa
mkoa wa Mtwara, Dk Salum Rashid Kabuma, akitoa tathmini ya jinsi mkoa huo
ulivyojipanga kukabiliana na Afya ya Uzazi wa mtoto, baba, na mama katika
kukabiliana na maambukizi mapya ya VVU mbele ya ujumbe kutoka Vodacom Foundation
na Taasisi inayojishughulisha na afya ya uzazi ya EGPAF (hawako pichani)
uliofanya ziara ofisini kwake. Vodacom hivi karibuni ilichangia mashine 8 za
kisasa ‘sms printers’ zenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani elfu 10
zinazowezesha upimaji na upatikanaji wa majibu ya VVU kwa watoto wachanga kwa
haraka wanaozaliwa mkoani humo.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Dk
Salum Rashid Kabuma, akiwaonesha maofisa waandamizi kutoka Vodacom Foundation na
Taasisi inayojishughulisha na tafiti za Afya ya Uzazi wa mtoto, baba na mama ya
EGPAF (hawako pichani) takwimu za kiwango cha maambukizi ya VVU ndani ya mkoa
huo, ofisini kwake jana, wakati wadau hao walipofanya ziara ya kukagua
maendeleo na ufanisi wa msaada wa mashine ‘sms printers’ zipatazo 8 zenye
thamani ya zaidi ya Dola za Marekani elfu 10, zilizotolewa na Vodacom Foundation
chini ya uratibu wa EGPAF, katika kuwezesha upimaji na upatikanaji wa majibu ya
VVU kwa watoto wachanga kwa haraka.
Akinamama wa
mkoa wa Mtwara wakihudhuria kliniki ndani ya Hospitali ya Mkoa huo, kwa lengo la
kuangalia maendeleo ya afya ya watoto wao. Vodacom Foundation walikuwa katika
ziara ya kuangalia maendeleo ya ufanisi wa mashine zake takriban 8 za kisasa
zijulikanazo kama ‘sms printer’ walizozitoa mkoani humo hivi karibuni, kuwezesha
upimaji na upatikanaji wa majibu ya VVU kwa watoto wachanga kwa
haraka.
Meneja wa Vodacom Foundation,
Grace Lyon, (kushoto) akiagana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Dk
Salum Kabuma, baada ya kupata taarifa fupi ya maendeleo ya Afya ya Uzazi wa
Mtoto, baba na mama. Vodacom Foundation walikuwa katika ziara ya kuangalia
maendeleo ya ufanisi wa mashine zake takriban 8 za kisasa zijulikanazo kama ‘sms
printer’ walizozitoa mkoani humo hivi karibuni, kuwezesha upimaji na upatikanaji
wa majibu ya VVU kwa haraka kwa watoto wachanga.
--
· Kutokana na kuzingatia
sera ya Afya ya Uzazi
· Mashine za kupima VVU
kwa watoto wachanga zachangia
KIWANGO cha maambukizi ya VVU
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kimeshuka kwa kasi
katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kufuatia mwamko na ushirikiano wa
dhati, kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa, katika kutekeleza sera ya afya ya
uzazi.
Hadi kufikia sasa, takwimu
zinaonesha kati ya watoto 100 wanaozaliwa na akinamama ambao tayari
wamegundulika kuwa na maambukizi ya VVU ni watoto 2 huzaliwa na maambukizi,
wakati wengine 98 huzaliwa wakiwa salama.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa
wa Mtwara, Dk Rashid Kabuma, aliyasema hayo ofisini kwake mkoani hapa, katika
mazungumzo yake na maofisa watendaji kutoka Vodacom Foundation na Taasisi
inayojishughulisha na Tafiti na Huduma za Afya ya Uzazi ya EGPAF.
Ujumbe huo ulikuwa katika ziara
ya kutembelea na kukagua maendeleo na ufanisi wa mashine 16 za kisasa
zinazowezesha upatikanaji wa majibu ya vipimo vya VVU kwa watoto wachanga kwa
haraka, zijulikanazo kama ‘sms printers’ kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambazo
zimegharimu zaidi ya Dola za kimarekani elfu 23 zilizotolewa kama msaada na
Vodacom Foundation, chini ya uratibu wa EGPAF.
Kabuma alibainisha kuwa siri ya
mafanikio hayo ambayo yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa nchini kote, ni mwamko wa
akinamama wajawazito katika kutambua mustakabali na thamani ya mtoto
atakayezaliwa na namna bora ya kumuandalia mazingira salama kiafya.
“Kwakweli mwamko unaridhisha, na
hata ukiangalia kiwango cha maambukizi ya VVU Mtwara ni asilimia 3.6 wakati
akinamama wajawazito wenye maambukizi hayo ni asilimia 3.2 mwamko upo. Hivi sasa
mama anapokuja kliniki anaongozana na baba na wote tunawapatia huduma na elimu
stahiki juu ya Afya ya Uzazi,” alisema.
Hadi kufikia sasa mkoa wa Mtwara
una idadi ya vituo 172 vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi toka kwa mama
kwenda kwa mtoto ambapo kati ya hivyo vituo 85 sawa na asilimia 49 vinatoa
huduma ya Afya ya uzazi. Na wazazi ambao wamepatiwa majibu ya vipimo kupitia sms
printer wanafikia 107.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya
Mkoa wa Lindi, Dk Sonda Shaaban, alisema mkoa huo una idadi ya vituo 200
vinavyotoa huduma ya tiba na ushauri dhidi ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto, na takwimu zinaonesha wanawake waliopatiwa vipimo vya VVU ni
23924, na miongoni mwao 884 sawa na asilimia 3.7 waligundulika kuwa na
maambukizi.
“Watoto wanaoendelea kufuatiliwa
kwa ajili ya kupatiwa tiba endelevu mkoa wa Lindi ni 177 wakati wazazi ambao
hadi sasa wamekwisha patiwa majibu ya vipimo vya vvu kupitia sms printer ni 71,”
alisema Shaaban.
Naye Meneja wa Vodacom
Foundation, Grace Lyon, alisema tangu Oktoba 2012 hadi sasa, Mfuko wa Kusaidia
Jamii wa Kampuni yake umekwisha changia jumla ya sms Printers 43 katika mikoa
kadhaa nchini, ikiwemo Shinyanga, Tabora, Arusha, Mtwara na Lindi.
“Tunatambua umuhimu wa huduma ya
Afya ya Uzazi kwa mtanzania ndio sababu tumetoa msaada wa mashine hizi kuepusha
usumbufu kwa wataalamu wa afya kusafiri umbali mrefu na kutumia muda mwingi
kukusanya majibu ya VVU..hadi sasa tayari tumepeleka sms printers 9 Tabora,
Shinyanga 5, Kilimanjaro 6, Arusha 6, Mtwara 8 na Lindi 8,” alisema
Lyon.
Mwisho
Post a Comment