MBUNGE wa Rombo, Joseph
Selasini (Chadema) amewasilisha bungeni CD za video zenye ushahidi wa namna
baadhi ya taasisi za kiserikali nchini zinavyokumbatia na kuchochea suala la
udini kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Selasini alisema CD hizo mbili zina ushahidi
wa namna polisi wanavyoshindwa kuwakamata baadhi ya watu ambao wanazungumza kwa
uwazi kuwa ukiona mtu wa dini fulani chinja jambo ambalo alisema ni hatari kwa
ustawi wa amani nchini.
Kuhusu Chuo Kikuu cha Dodoma, Selasini
alisema CD hiyo inaonesha chuo hicho kinavyoendeshwa kidini kwani wanaonekana
baadhi ya wahadhiri wakiwa wamewakusanya wanafunzi wa dini moja na kuwalisha
maneno ya chuki dhidi ya wanafunzi wa dini nyingine.
“Baada ya wanafunzi hao kulishwa maneno ya
chuki na wahadhiri hao wa dini fulani, wakahoji huko vyumbani tunakaa na
wanafunzi wa vyuo vingine tuwafanyeje?
Lakini licha ya kuwepo ushahidi wa mikanda
hiyo, Selasini alisema hakuna mtu ambaye ameshakamatwa kutoka katika taasisi
hiyo ya Serikali inayoongozwa na Mkuu wa Chuo, Benjamin Mkapa na Makamu wake ni
Profesa Idris Kikula.
Mbunge huyo pia alisema jijini Dar es Salaam
katika baadhi ya shule kuna walimu wa dini moja wanawachukua wanafunzi wa dini
yao na kwenda kuwafundisha na viongozi wanaohusika na kulinda amani ya nchi
wamekaa kimya.
“Tusiwe wanafiki wa kukemea udini kwa nje
wakati ndani ya mioyo yetu kuna chuki kubwa dhidi ya watu wa dini nyingine,”
alisema Selasini.
Alitoa mfano kuwa katika Jiji la Dar es
Salaam ipo mikanda imesambazwa mitaani na watu wa dini moja ambayo inawataka
waumini wake kuwaua viongozi na waumini wa dini nyingine na polisi haijachukua
hatua yoyote.
“Wako wapi polisi wetu wanaosifiwa, kwa nini
wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya mikanda hii inayouzwa kama njugu pale Dar es
Salaam?Alihoji mbunge huyo. Mbunge huyo alieleza kusitikishwa na taifa hili
kuacha misingi aliyoiacha mwasisi wa taifa letu Mwalimu Julius Nyerere ambaye
katika kipindi chake hakukuwa na suala la udini kutokana na watu kuoleana na
kuishi pamoja kama ndugu. Baada ya kutoa hoja hiyo, Mbunge wa Kondoa Kusini Juma
Nkamia (CCM) alidai chuo kikuu cha Dodoma kimetulia na hayo mambo yanayosemwa na
Selasini hayapo.
“Nadhani tatizo la pale UDOM ni Profesa
Kikula na Profesa Mlacha (Shaban ) wanahukumiwa kwa dini zao, leo hii kungekuwa
na Lyimo pale haya yasingezungumzwa humu bungeni,” alisema Nkamia ambaye alidai
anasoma hapo kwa sasa. Nkamia alisema yeye akiwa mwanafunzi hapo hajasikia suala
la udini .
“Hii mikanda ya mbunge aliyoiwasilisha hapa
bungeni ni za mitaani tu zisitiliwe maanani, Udom kwa sasa
kumetulia.”
Post a Comment