MBUNGE wa Mwibara, Kangi
Lugola (CCM) amefichua siri ya sababu ya Kamati ya Wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kuwaweka kitimoto yeye na Mbunge wa Ludewa, Deo
Filikunjombe.
Akizungumza katika
mahojiano maalumu na gazeti hili, Lugola (pichani) alisema sababu ya kibano alichopata
ndani ya CCM ni kutokana na kauli aliyotoa hivi karibuni mkoani Iringa ya
kumuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
“Wabunge wa CCM
tunaoikosoa serikali na kuzigomea bajeti tuko wengi, kwanini ndani ya kikao
wametubana mimi na Deo tu? Mimi nadhani ile ziara tuliyoifanya hivi karibuni
kumsindikiza Lowassa mkoani Iringa ndiyo imeleta shida yote hii,”
alisema.
Mbunge huyo machachari
bungeni, alisema pamoja na maneno na vitisho alivyotolewa ndani ya kikao hicho
na baadhi ya mawaziri na wabunge wenzake wa CCM, kamwe hawezi
kuogopa.
Alisema hatua ya kutaka
kunyamazishana, hakubaliani nayo bali anaendelea na kasi yake ya kuibana
serikali pale anapoona dhahiri kwamba inakosea.
“Mimi siogopi maneno,
hata kifo chenyewe pia sikiogopi. Nitasimamia ukweli, CCM ni chama changu na
serikali ni yangu na naitakia mema ndiyo maana nipo tayari kufa kwa kusimamia
ukweli huo,” alisema.
Hivi karibuni Lowassa aliambatana na wabunge hao mkoani Iringa ambako alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na kituo cha redio cha Overcomers Power Centre (OPC) mjini Iringa.
Katika hafla hiyo
alitunukiwa tuzo maalumu kutokana na jitihada zake za kuitumikia na kuisaida
jamii nchini.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Lugola aliwashangaa watu wanaowalaumu wanasiasa kwa kuingia makanisani na
kusema kuwa kazi wanazozifanya hazina tofauti na za viongozi wa
dini.
Lugola alifananisha
matukio yaliyomkuta Lowassa sawa na matatizo yaliyomkuta Bwaba Yesu wakati
alipokuwa anahubiri duniani.
Alimmwagia sifa Lowassa
kuwa licha ya maneno mengi yanayosemwa juu yake, lakini bado ameendelea
kuitumikia jamii kupitia siasa na shughuli za kidini.
Alisema kuwa kama
ilivyokuwa kwa Yesu ambaye alipigwa na kunyanyaswa na kuyaacha yote kwa Mungu,
Lowassa naye aliandamwa na waliomzushia kesi kiasi cha kuamua kujiuzulu uwaziri
mkuu.
“Mnakumbuka kuwa
waliomchukia Yesu walimfungulia mashtaka ya uongo wakamfikisha mbele ya pilato.
Walipoambiwa watoe ushahidi wakashindwa, lakini wakapiga kelele asulubiwe. Yesu
alipigwa, akatemewa mate, lakini yeye akasema ‘ikiwezekana kikombe hiki
kiniepuke lakini si kama nitakavyo mimi bali mapenzi ya Mungu
yatimizwe’.
“Vivyo hivyo Edward,
aliposakamwa sana aliamua kujiuzulu uwaziri mkuu...lakini tunajua kuwa Yesu,
baada ya kuuawa, alifufuka na kuinuliwa. Naomba kanisa liendelee kumuombea
Lowassa ili naye ainuliwe juu katika nchi yetu ya Tanzania,” alisema
Lugola.
Filikunjombe naye
alimwaga sifa kwa Lowassa akimtaka kutokatishwa tamaa na maneno yanayosemwa, na
kuongeza kuwa siku zote mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe.
Wiki iliyopita katika
kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, Lugola na Filikunjombe walisutwa kutokana na
mwenendo wa kuikosoa serikali na kuwashambulia mawaziri.
Mbunge aliyewawashia
moto wabunge hao ni Said Nkumba wa Sikonge ambaye alihoji mwenendo
wao.
Mbele ya Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, Mkumba alisema kuwa wabunge hao wanatumika na CHADEMA na kuwataka
waamue kama wanabaki CCM au la.
Hoja hiyo iliungwa mkono
na wabunge wengi, huku mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akitolea mfano
wake.
Naibu Waziri wa Kilimo
Chakula na Ushirika, Adam Malima naye alimbana Lugola ataje majina ya mawaziri
alioliambia Bunge kwamba wanauza unga.
Chanzo: Tanzania
Daima
Post a Comment