Rais Mstaafu,
Benjamin Mkapa amesifia utawala wake kwa kuongoza taifa bila ya kubaguana na
amesikitishwa na matukio ya udini, ambayo yanaashiria kuvuruga amani na utulivu
wa Tanzania katika siku za karibuni.
Akitoa salamu
zake baada ya kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Desdelius
Rwoma, Mkapa alisema anachojivunia ni kuheshimiwa na waumini wa
madhehebu
yote.
“Katika kipindi cha uongozi wangu, viongozi wa
madhehebu yote walikuwa wakinisisitizia kuwa sisi sote ni ndugu pamoja na
tofauti zetu za kiimani. Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu
wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika jamii,”
alisema Mkapa, ambaye aliiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1995-2005.
Mkapa alionya kuwa taifa limeacha misingi aliyoiacha
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara zote alisimamia umoja wa
taifa.
“Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu
wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika jamii,”
alisema.
Mkapa ambaye hakupanga kuongea lolote katika tukio
hilo, alitaka taifa lijenge utamaduni wa kupendana, huku akilaumu kuwa kizazi
kipya cha uongozi kimeanzisha mambo ya ajabu ya kukosa upendo na
kudhalilishana.
Pia alitahadharisha kuwa
zama hizi kumeibuka mitafaruku mbalimbali na kuwakumbusha Watanzania kuwa ni
wakati wa kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Mkapa alisema mara nyingi alishauriana na viongozi wa
dini katika masuala ya kijamii na kiroho na kumtaja askofu mpya wa Bukoba, Rwoma
na Mtangulizi wake aliyestaafu Nestory Timanywa kuwa alishirikiana nao katika
masuala ya wananchi. Onyo la Mkapa limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya
Kikwete kukemea mambo ya kidini na kutetea Serikali yake haiongozi kwa misingi
ya ubaguzi.
Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete
alikwenda mbali zaidi na kudai amekuwa akilalamikiwa na viongozi wa madhehebu ya
Kikristo na yale ya Kiislamu.
Maneno ya Mkapa na Kikwete yamekuwa katika kipindi
hiki taifa likiwa limetikiswa na matukio yenye mwelekeo wa chuki za kidini.
Matukio makubwa yakiwa yale ya kuuawa wa Padri Evarist Mushi huko Zanzibar na
Mchungaji Mathayo Kachila wa Geita.
Pia kupigwa risasi kwa Padre Ambrose Mkenda na
kumwagiwa tindikali kwa Sheikh Fadhil Soraga na vurugu za mambo ya kuchinja huko
Geita na Tunduma.
Askofu Mpya wa Bukoba
Rwoma alimshukuru Mkapa kwa kuzungumzia umuhimu wa amani ya nchi, huku
akisisitiza suala la upendo miongoni mwa
wananchi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye
jana alitaja vyanzo vya vurugu zinazoendelea nchini kuwa unatokana na tofauti
kubwa kati ya walionacho na wasionacho.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua santuri ya
nyimbo za dini kwa Kwaya ya Mt Joseph, Mfanyakazi ya Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM).
Sumaye alionya kuwa kama hali ya utajiri kwa baadhi ya
watu itaachwa na kuendelea hivyo, ni wazi kuwa nchi haitatawalika kwa
amani.
“Binadamu mwenye njaa na
aliyekata tamaa kamwe hawezi kutawalika kwani kila wakati anahisi kutengwa na
kundi jingine,” alisisitiza Sumaye.
SOURCE::MWANANCHI::
Post a Comment