- MAZISHI YAKE YAFANYIKA SAA SABA ZA USIKU MONDULI
WAKATI
Aprili 12 mwaka huu Watanzania wanatimiza miaka 29 tangu Waziri Mkuu
aliyeweka historia ya pekee nchini, Edward Moringe Sokoine alipofariki
dunia kwa ajali ya gari, mwili wake umehamishwa kutoka kwenye kaburi la
awali na kuzikwa katika kaburi jipya, Tanzania Daima Jumapili
limebaini. Habari
kutoka kwa ndugu wa karibu wa marehemu Sokoine, zililiambia gazeti hili
kuwa mwili wa waziri mkuu huyo ulizikwa kwenye kaburi jipya mwishoni
mwa mwaka jana mjini Monduli.
Kwa mujibu
wa habari hizo, mwili wa Sokoine umezikwa upya baada ya kaburi lake la
awali kupasuka na kuharibika kutokana na tetemeko la ardhi lililotikisa
milima ya Oldonyo Lengai mwaka jana na kusababisha maji kuingia ndani.
Mmoja wa
watoto wa kiongozi huyo wa zamani, aliliambia gazeti hili kuwa baada ya
kaburi hilo kuharibika na kuchakaa, Rais Jakaya Kikwete aliagiza
lijengwe upya.
“Lilipasuka
kiasi kwamba ukimwaga maji yalikuwa yanaingia hadi ndani. Rais Kikwete
aliagiza lijengwe upya na baadaye walitumwa wanajeshi ambao pamoja na
ndugu tulikubaliana kuchimba kaburi jipya na kuhamishia mwili huo katika
kaburi jingine,” alisema mtoa habari wetu.
Kwa mujibu
wa habari hizo, shughuli za kuhamisha mabaki ya mwili huo na kuuzika
upya katika kaburi jingine ilifanyika saa saba usiku na kushuhudiwa na
watoto wote na baadhi ya ndugu wa marehemu walioko ndani na nje ya nchi.
Pia baadhi ya viongozi, akiwamo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa walikuwapo. Inaelezwa
kuwa mwili huo uliozikwa ndani ya jeneza miaka 29 iliyopita bila
kufukiwa na udongo, bado uko katika hali nzuri kabisa na hii inatokana
na sindano aliyochomwa ambayo ina uwezo wa kuhifadhi mwili huo katika
hali nzuri ndani ya miaka takriban 40.
“Sanduku
lake bado zito na mwili upo kama ulivyokuwa wakati ule anaagwa. Tulitaka
kuufungua na kuhamishia kwenye jeneza jingine la kisasa tuliloandaa,
lakini mzee Lowassa ambaye ni baba yetu, alituzuia,” alisema mtoa habari
wetu.
Alisema hivi
sasa kaburi la awali alimozikiwa limefukiwa na kaburi jipya lipo jirani
na lile la zamani likiwa katika hali na mwonekano mzuri.
Katika hali
ya kushangaza, watoto wa marehemu Sokoine pamoja na baadhi ya ndugu bado
wanakusudia kufanya uchunguzi upya wa mwili huo ili kubaini kama kweli
kifo chake kilitokana na ajali aliyoipata au la.
Ikumbukwe
kuwa wakati wa kifo chake kulikuwa na mjadala mzito, wengi wakidai
aliuawa na kwamba kifo chake kilipangwa na mahasimu wake ndani na nje ya
serikali ambao walikerwa na operesheni yake ya kupambana na wahujumu
uchumi na mali za taifa.
Kwa mujibu
wa habari hizo, wapo baadhi ya watoto na ndugu wanaoamini kuwa kwa jinsi
msafara wa kiongozi mkubwa kama waziri mkuu unavyowekewa ulinzi, ni
vigumu gari jingine kutoka upande wa pili na kuligonga gari lake, hivyo
wanaamini aliuawa.
“Siku
tuliyozika upya, ndugu wote tulikubaliana mwakani tuombe kibali cha
serikali kuleta wataalamu kuchunguza ili kubaini chanzo cha kifo chake
kama kilitokana na ajali au la.
“Lakini mzee
Lowassa alituzuia, na kwa vile tunamheshimu sana kama baba yetu
tuliukubali ushauri wake, lakini mwakani tumepanga tuufanyie uchunguzi
mwili huo,” alisema mtoa habari wetu.
Kwa mujibu
wa sheria, mwili ukishazikwa unaruhusiwa kufanyiwa uchunguzi baada ya
miaka 30 na mwakani mwili wa Sokoine utafikisha umri wa miaka 30 tangu
ulipozikwa na huo utakuwa muda muafaka kwa wana ndugu hao kutaka kujua
ukweli wa kifo cha ndugu yao.
Sokoine alifariki dunia Aprili 12 mwaka 1984 eneo la Wami-Dakawa akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Ilikuwa majira ya saa kumi jioni, Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza kifo chake kwa sauti ya huzuni. Sokoine alikuwa kiongozi wa kweli ambaye daima alisimama upande wa umma.
Wengi wanamuelezea kwamba alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa kwani aliishi kama alivyohubiri.
Sokoine si tu kwamba hakujilimbikizia mali, bali pia alipunguza hata mali zake ili apate nafasi zaidi ya kuwatumikia Watanzania.
Itakumbukuwa
kwenye kikao cha Bunge cha mwezi Aprili 1984, Sokoine alikabiliana na
hoja za wabunge kutaka kuongezewa posho na marupurupu yao ambapo
alitamka: “Ndugu Spika, niko tayari kuwaongezea wabunge posho ya chakula
chao, lakini kamwe sitakuwa tayari kuwaongezea mishahara na marupurupu
mengine.”
Baada ya
kikao kile cha Bunge, Sokoine badala ya kupanda ndege ya serikali
kumrudisha Dar es Salaam, aliamua kurudi kwa njia ya barabara, apate
nafasi ya kuona shughuli za maendeleo.
Chanzo - Freemedia
Post a Comment