UKATILI wa kusikitisha! Watoto watatu wa famila moja, wameuawa kikatili kwa kunyongwa huku mama yao akishuhudia. Miili yao pamoja na mama yao akiwa hai, wakatumbukizwa katika kisima cha maji. Baba wa watoto hao, Justine Albert (24) anatuhumiwa kufanya unyama huo.
Kabla ya mauaji hayo, inadaiwa baba huyo alimfunga
kamba mkewe na kumziba mdomo kwa kitambaa ili asipige kelele, kisha akaanza
kuwanyonga watoto wake wote watatu kwa zamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari,
alisema mauaji hayo ya kikatili yalifanyika juzi saa 11:30 alfajiri katika
Kijiji cha Majimoto, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Mlele mkoani
humo.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, kisa cha kufanya
mauaji hayo ni mzozo wa mtuhumiwa na mkewe, Jacqueline Luvika (21), kwamba
baadhi ya watoto hao mama huyo kazaa na jirani yao.
Watoto hao ni Frank Justine (6), Elizabeth Justine (4)
na kitinda mimba Maria Justine, mwenye umri wa miezi minne.
Baada ya kuwanyonga watoto hao, inadaiwa baba huyo alibeba miili ya watoto Frank na
Eliza, na kwenda kuwatumbukiza kwenye kisima cha jirani yao, Kawaida
Jonas.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kidavashari, mtuhumiwa
baada ya kuwatumbukiza watoto hao kisimani, alimfungua
kamba mkewe na kumtoa kitamba alichomziba mdomoni, kisha akamburuta hadi kwenye
kisima hicho na kumtumbukiza.
Kugundulika Baada ya matukio hayo yanayodaiwa kufanyika
alfajiri, kulipopambazuka baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, waliodamka kwenda
katika shughuli zao, waliuona mwili wa mtoto ukiwa umetelekeza kando ya njia na
kutambua kuwa ni Maria, ambaye ni kitindamimba katika familia hiyo.
Inadaiwa wakazi hao walisitisha safari yao na kwenda
nyumbani kwa mtuhumiwa, kumpatia taarifa hiyo ya kuhuzunisha, huku wakiuliza
mama wa mtoto aliko.
Kamanda Kidavashari alidai mtuhumiwa aliwaeleza wakazi
hao kuwa mama wa mtoto huyo, alikuwa ametoroka kwenda kusikofahamika na watoto
wote.
Majibu hayo ‘rahisi’ kwa mujibu Kamanda Kidavashari,
yalisababisha wakazi hao wamtilie shaka mtuhumiwa, wakaamua kutoa taarifa kituo
cha Polisi kijijini hapo, ambao walifika ulipo mwili wa mtoto
Maria.
Wakati wakiwa katika eneo la tukio, Kamanda Kidavashari
alidai walibaini alama za mburuzo ardhini, wakaanza kuifuatilia na zikawafikisha
kisimani. Walipofungua mfuniko wa kisima hicho, walishtuka kuona miili wa watu
watatu, ikielea kwenye maji kisimani humo.
Askari Polisi kwa kushirikiana na wakazi wa kijiji
hicho, waliopoa miili yote, lakini watoto hao wawili tayari walikuwa wamefariki,
huku mama yao akiwa amekunywa maji mengi na kupoteza fahamu.
Kutokana na hali hiyo, wakazi hao walipandwa na hasira
na kwenda kuvamia nyumba ya mtuhumiwa na kumkamata ili wamchome moto. Hata
hivyo, Kidavashari alisema polisi walifanikiwa kufika kwa wakati katika eneo
hilo na kumwokoa mtuhumiwa, ambaye kwa sasa bado ameshikiliwa Polisi kwa
mahojiano.
Mama wa watoto hao kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari,
alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Kijijini cha Mamba wilayani humo, ambako
amelazwa kwa matibabu, lakini hadi jana bado alikuwa amezirai. Mtuhumiwa
anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi wa awali wa shauri
lake kukamilika.
Post a Comment