Watumishi wa vituo vya afya na zahanati nchini,
wametakiwa kuwasilisha mapema oda zao za dawa kwa waganga wakuu wa wilaya
mwishoni mwa juma la kwanza la mzunguko wa ugavi shirikishi.
Hayo yamesemwa leo na KAIMU Mkurugenzi wa Bohari
Kuu ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani alipokuwa akizungumza na wakurugenzi wa
halmashauri, waganga wakuu, wafamasia pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za
Mashirika ya Dini.
Mwaifwani alisema utaratibu huo utawawezesha MSD
kutumia majuma nane kuchambua oda, kutengeneza Ankara za mauzo na kuzifungusha
na kuzifikisha dawa moja kwa moja kituo cha afya na zahanati ifikapo juma la
kumi na mbili.
“ili tuweze kuwahudumia kwa kiwango kizuri
tunahitaji hospitali ziwasilishe mahitaji yake siku kumi na nne kabla ili sisi
tuweze kujiandaa vya kutosha na kukamilisha oda kwa wakati”.
Aidha,alisema kuwa, malalamiko mengi ya kutokuwa
na dawa katika vituo vya afya nchini, yanasababishwa na watendaji wasio
waaminifu ambao hawazifikishi vituoni.
Mwaifwani alisema hayo Pia alisema wengine
huziuza kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi ili kujipatia utajiri wa haraka
haraka.
“Ili kuzuia mwanya huu, MSD itakuwa inafikisha
dawa hadi ngazi ya zahanati na vituo vya afya nchini nzima kuanzia Julai mwaka
huu,” alisema.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kunapokuwepo na
shida ya utendaji au ushauri wowote kuhusu MSD inapaswa kuzitumia ofisi zao za
kanda zilizopo nchini nzima, mteja asiporidhika malalamiko hayo yapelekwe katika
ofisi yake.
Awali Meneja wa MSD kanda ya Kaskazini, Celestine
Haule alisema kuwa, bohari kuu ya dawa nchini ilipewa agizo na Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii la kufikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi hadi ngazi ya
zahanati.
Alisema lengo lilikuwa ni kupunguza mlolongo
mrefu uliopo kwa sasa katika ufikishaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi
katika vituo vya kutolea huduma ya afya.
Mwisho
Na.
Catherine Sungura,
Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii
Morogoro
8/4/2013
Post a Comment