* POLISI WADAIWA KUMFANYIA
UNYAMA KADA WA CHADEMA
HATIMAYE Naibu Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba, amekiri kuhusika na
video inayomwonesha Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare.
Nchemba amekuwa akitajwa
na viongozi wa CHADEMA kuwa anahusika kutengeneza video hiyo, kwa kuwa aliwahi
kutamba wakati akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni kuwa anayo video
inayowaonesha viongozi wa chama hicho wakipanga mauaji.
Hata hivyo, tangu
Nchemba atoe kauli hiyo Januari mwaka huu, Jeshi la Polisi lilikaa kimya hadi
Machi 12 lilipomkamata na kumhoji Lwakatare, siku moja baada ya video hiyo
kuwekwa kwenye mtandao wa You tube na mtu anayejiita ‘Bukoba
Boy’.
Akizungumza na gazeti
hili kwa simu jana, Nchemba alikiri kuwa ndiye aliyeipeleka video ya Lwakatare
polisi na kwamba alifanya hivyo baada ya kuripoti kuandikiwa ujumbe wa simu wa
kutishiwa maisha na baadhi ya viongozi wa CHADEMA.
“Niliwapelekea mimi hiyo
video polisi na wakati nasema kwenye televisheni nilikuwa tayari nimewapa. Na
pale nilisema makusudi baada ya Zitto Kabwe kudai kuwa mwaka jana kulitokea
mauaji mengi, ndipo nikataka kumuonesha kuwa chama chake kinahusika na mikakati
hiyo,” alisema.
Alipoulizwa
aliipataje video hiyo na kwanini hajahojiwa polisi ili kutoa uthibitisho wa
uhalali wake, Nchemba alisema: “Kuna msamaria mwema aliniletea.”
Nchemba alipobanwa ana
uhakika gani kama video hiyo ina ukweli, alijibu kuwa: “Ile huhitaji akili kubwa
kutambua uhalisia wake. Suala la Lwakatare CHADEMA wakubali tu na wajitokeze
hadharani kwenye makanisa na misikiti, watubu na kuomba radhi kwa
umma.”
Hata hivyo katika kile
kinachoweza kuongeza mashaka ya Nchemba kuhusishwa kutengeneza video hiyo,
alikwenda mbali zaidi akitoa hata siri za polisi, akisimulia maelezo aliyodai
kuwa ndiyo yalitolewa na Lwakatare wakati akihojiwa na polisi.
“Pale video inaonesha ni
nyumbani kwake, tena jikoni na hilo amekiri katika maelezo yake polisi. Pia
amekubali kuwa siku hiyo alipiga chafya kama inavyoonekana. Sasa wewe mwandishi
unatetea nini wakati yeye amekiri polisi kila kitu kilichomo mle,”
alisema.
Maelezo ya Nchemba
yalionekana kumtia hofu mmoja wa mawakili wa Lwakatare, ambaye alikuwepo wakati
wote wa mahojiano polisi, Nyaronyo Kicheere, akidai kuwa ni wazi jeshi hilo
linafanya kazi ya propaganda za CCM.
“Nchemba hakuwepo wakati
Lwakatare akihojiwa na hata baadhi ya wanasheria katika kesi yake ya ugaidi
inayomkabili hawajui alichokisema polisi, sasa huyo amepata wapi siri za polisi
kama si mchezo unachezwa?” alihoji.
Kuhusu mahusiano yake na
mshtakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, Ludovick Joseph, ambaye anadaiwa na
baadhi ya watu kuwa ndiye aliyerekodi video hiyo, Nchemba alisema walifahamiana
kupitia mtandao wa kijamii wa facebook.
Alipotakiwa kufafanua
ukaribu wao hadi kufikia hatua ya kumtumia fedha kwa njia ya M-Pesa kupitia simu
yake, Nchemba alisema: “Mimi nilimtumia kama ninavyowapa watu wengine hata wa
CHADEMA.
“Mimi sijui kama
Ludovick ndiye alirekodi video hiyo, wala sikuwahi kumtuma kufanya hivyo na
fedha niliyomtumia si kwamba nilikuwa nikimlipa ujira. Kwani unaweza kumpa mtu
sh 50,000 tu kwa kazi hiyo?” alihoji.
Tanzania Daima
lilipotaka kufahamu kama anahusika kushirikiana na vyombo vya dola kuwarubuni
baadhi ya vijana wa Makao Makuu CHADEMA kwa fedha ili watumike kutoa ushahidi wa
kumwangamiza Lwakatare mahakamani, Nchemba alisema: “CHADEMA haijawahi kuongoza
serikali, hivyo hawajui mikono ya serikali.”
Alipotakiwa kufafanua
kikao baina yake na vijana hao kilichofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff ya
jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita na kisha kuwatumia fedha kwa
njia ya M-Pesa, Nchemba aling’aka na kuuliza: “Hiyo Hoteli ya Sea Cliff iko
wapi? Maana sipajui na sijawahi kufika.”
Mwishoni mwa wiki
iliyopita, Mkurugenzi wa Mambo ya Katiba wa CHADEMA, Tundu Lissu, alifichua
njama zinazofanywa ili kutengeneza ushahidi wa uongo kwa ajili ya kuutumia
katika kesi ya ugaidi inayomkabili Wilfred Lwakatare.
Lissu alidai kuwa njama
hizo zinafanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
usalama na ujasusi ili kutumia ushahidi huo mahakamani dhidi ya
Lwakatare.
Alisema kuna baadhi ya
vijana wa CHADEMA wa Idara ya Ulinzi na Usalama wanaopewa fedha na kuahidiwa
kufundishwa namna ya kuzungumza katika kesi hiyo ya Lwakatare.
Lissu alisema kuna
baadhi ya vijana wakiongozwa na Saumu Mulugu, ambaye alifukuzwa kazi CHADEMA
mwanzoni mwa mwaka jana, wamepokea fedha kutoka kwa kigogo mmoja wa CCM (jina
linahifadhiwa) ili kufanikisha mpango huo.
Lissu alisema hadi sasa
vijana hao wameshapewa sh 400,000 ili wakubali kwenda kufundishwa jinsi ya
kuzungumza mahakamani kuwa CHADEMA ni chama cha kigaidi, kwamba Lwakatare
alipanga mikakati ya kigaidi.
“Awali walipewa sh
400,000, wakapewa tena sh 300,000, pia wakapewa sh 35,000 mara mbili. Na fedha
zote hizi walikuwa wanapewa kwa njia ya M-Pesa,” alisema Lissu.
Alidai kuwa Saumu ndiye
anayeratibu mpango wote kati ya Jeshi la Polisi na vijana hao wa CHADEMA kwa
kuwarubuni kwa fedha.
Alisema vikao baina ya
vijana hao wa CHADEMA na Saumu vimewahi kufanyika mara kadhaa katika moja ya
hoteli maarufu nchini juu ya mambo ya kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari
au mahakamani kwenye kesi ya Lwakatare.
Siku moja baada ya madai
ya Lissu, gazeti hili lilimnasa Saumu akiwa anawasiliana na wenzake, huku
akiwatuhumu baadhi yao kuwa ndio waliovujisha siri kwa Lissu.
Vilevile alionekana
akiwasiliana na kigogo mmoja wa CCM ambaye alikuwa akimwita ‘mkuu’ huku
akimsomea baadhi ya taarifa zilizoandikwa magazetini jana yake kuhusu kuvuja kwa
siri zao.
Saumu akiwa katika
grosari karibu na baa maarufu kwa jina la Kwa Kimaro, jirani na eneo la Benki
Kuu ya Damu Salama, Mchikichini jijini Dar es Salaam, alisikika akiwalalamikia
wenzake kwa kumsaliti na kuvujisha mkakati wao kwa Lissu.
“Kwanini mmelikisha siri
zetu kwa Lissu hadi amejua tulikutana katika hoteli ya kifahari na Mwigu…? Sasa
nitawaonesha, maana laki tano zenu ninazo mimi. Siwapi bali nitazitumia
kujilinda,” alitamba.
Saumu ambaye alikuwa
akizungumza kwa sauti kubwa ya ghadhabu kupitia simu, aling’aka: “Nyie kwanini
mmeniuza kwenye ishu ambayo tumeipanga wote?”
Baada ya kupokea
maelekezo kutoka kwa ‘mkuu wake’ aliendelea kupiga simu akimlalamikia mtu ambaye
hakumtaja, kuwa alikuwa amezima simu yake makusudi kwa kuwa ndiye alivujisha
siri zao kwa CHADEMA.
“Mimi sitakubali na
nimehakikishiwa na bosi wetu kuwa huyo aliyetusaliti tutatumia wale askari
kumwekea hata unga. Haiwezekani fedha tumepokea za kwanza, za pili na tatu
kwanini tuuzane dakika za mwisho?” alidai Saumu huku akiendelea kugida bia
yake.
Huku akihaha huku na
kule, Saumu alikuwa akiwapigia simu baadhi ya madereva wa CHADEMA makao makuu na
kuwaomba simu za baadhi ya watu, na hata wakati mwingine kuwafokea akidai ndio
waliofichua siri hiyo.
Hata hivyo, baada ya
kutilia shaka nyendo za chanzo chetu kudaka siri zake, ghafla alitokomea na
kuzima simu zake mara moja kwani hata alipotafutwa baadaye hakupatikana hadi
leo.
Polisi wafanya
unyama
Katika hatua nyingine,
Jeshi la Polisi nchini limemkamata kada wa CHADEMA mjini Bukoba, Evodius
Justinian na kumshikilia kwa siku kadhaa kisha kumsafirisha hadi jijini Dar es
Salaam huku akipewa mateso makali ya kulazimishwa akubali kutengeneza video ya
Lwakatare.
Justinian (30), ambaye
ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) mjini Bukoba, alikamatwa
Jumanne ya wiki iliyopita akidaiwa kukabiliwa na makosa ya
jinai.
Alishikiliwa kwa siku
mbili mfululizo kabla ya kumsafirisha kwenda wilayani Igunga, Tabora ambako
alidaiwa kuwa alitenda makosa hayo ya jinai lakini alifichwa jijini
Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kagera, Philip Kalangi hakutaka kulizungumzia kwa undani suala hilo lakini
aligusia kuwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka ya kushambulia na kujeruhi mtu
huko wilayani Igunga.
Hata hivyo, kada huyo
alisafirishwa hadi uwanja wa ndege wa jijini hapa juzi, lakini akanyang’anywa
simu na kukatazwa kuzungumza na ndugu zake.
Taarifa za kada huyo
kuletwa jijini hapa zilikuwa za kificho kwani wakili wake Nyaronyo Kicheere
akiongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walifika Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam na kuelezwa kuwa amepelekwa makao makuu.
Walipofika makao makuu
kumwona na kumpatia chakula, polisi walisema hawana mtu kama huyo, hivyo
wakarudi tena Kanda Maalumu walipohakikishiwa kuwa yuko makao
makuu.
Akizungumza mbele ya
wakili wake, Kicheere, mtuhumiwa huyo alieleza unyama aliofanyiwa na jeshi hilo
wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na jijini hapa.
Katika maelezo yake
yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate Nyombi, Justinian
alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri bila ndugu zake kujua,
alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila kuruhusiwa kuonana na wakili
wake.
Alieleza kuwa wakati
wote wa mahojiano hayo alikuwa akilazimishwa kukiri kurekodi video ya Lwakatare
inayoonesha mikakati ya ugaidi.
Alisema alisafirishwa
kwa siri kwa ndege hadi Dar es Salaam, akapelekwa chooni na kumpiga, kutishiwa
na kuteswa kwa nyaya za umeme na kumnyima fursa ya kupewa
chakula.
Justinian ambaye
anaendelea kushikiliwa na polisi, anatarajiwa kufikishwa mahakamani
leo.
Kabla ya maelezo hayo,
Kicheere akiwa na Uloleulole Juma Athumani, ambaye ni ndugu wa Justinian,
alijitambulisha kwa Nyombi akimweleza kuwa walikuja kuonana na mteja wake pamoja
na kumletea chakula.
Hata hivyo, Nyombi
alisema hakuwa na habari za kukamatwa kwa kada huyo na kwamba angekuwa
amelimaliza mapema suala hilo.
Kada huyo alisimulia
unyama aliofanyiwa akisema: “Nimepigwa na polisi nikiwa Mwanza, nikiwa chooni
Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni
mtu hatari sana, niseme nilifanya nini Igunga.
“Nikiwa Uwanja wa Ndege
wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia pamoja na mimi wakanipiga
sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa, niliomba kuwa na wakili
wakanikatalia,” alisema.
Aliongeza kuwa akiwa Dar
es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya Lwakatare. Akawajibu kuwa
ilifanyiwa uhariri na Ludovick lakini akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya
za umeme za kutesea.
“Waliposimama kuleta
nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni yangu.
Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia dawa nilizonunuliwa na Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kagera tarehe 4 Aprili,”
alisema.
Justinian aliongeza kuwa
hakula chakula chochote cha polisi kwa kuwa hawaamini, ila kuhara kulipozidi
alikubali kula chakula chao.
Wakili Kicheere alisema
ni makosa makubwa sana kumtesa mtu kwa kipigo na vitisho vya umeme na kwamba
hayakubaliki hata mahakamani.
“Polisi hawakutaka
nionane naye kwa makusudi hadi walipomaliza kumhoji na kumtesa ndipo
wakaniruhusu,” alisema.
Tanzania
Daima
Post a Comment