NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo
Mulugo amesema atawafikisha mahakamani watu wanaodai kuwa ameghushi vyeti vya
elimu ya sekondari. Mulugo alisema amechoshwa na kashfa hizo zinazosambazwa na
baadhi ya watu atawafikisha mahakamani endapo wataendelea
kumdhalilisha.
Mulugo alitoa kauli hiyo alipofungua mkutano wa mwaka
wa Umoja wa Wamiliki wa Shule za Sekondari na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO0)
jijini Mbeya.
“Wanasema eti nimeghushi vyeti, mara ooh sijui natumia
jina la mtu. Nimechoshwa na maneno haya… ni kweli nimerudia darasa kama
walivyorudia watu wengine, kwa nini iwe tatizo kwangu. Hata hapa tulipo wapo
wengi tu waliorudia darasa.
“Kama kweli ningekuwa
nimeghushi vyeti hivi leo ningekuwa naibu waziri wa elimu? Sasa nimechoshwa,
nitawachukulia hatua watu hawa, siwezi kusema ni lini nitafanya hivyo ila
nitakapoamua nitaanza,”alisema.
Kwa miezi kadhaa sasa Mulugo amekuwa akidaiwa kughushi
vyeti na kutumia jina la mtu ili kufikia kiwango cha elimu alichonacho madai
ambayo alisema yanamchafulia jina katika jamii.
Kuhusu suala la matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka
jana, Mulugo alisema matokeo hayo mabaya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na
mmomonyoko wa maadili miongoni mwa wanafunzi.
Naye Ruth Mnkeni kutoka Dar es Salaam anaripoti kuwa
Mlugo amezindua tovuti ya elimu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ijulikanayo
kama Shule Direct.
Muluigo alisema kuzinduliwa kwa tovuti hiyo kutawafanya
wanafunzi kupata maarifa mengi ya vitabu mbalimbali na kuinua kiwango cha elimu
nchini
Post a Comment