Naibu Kaibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi upande wa Zanzibar, ndugu Vuai Ally Vuai (Pichani) ameeleza kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kudumisha muungano ulioasisiwa na muasisi wa Serikali ya mapinduzi na Chama cha ASP Marehemu Abeid Amani Karume.
Mheshimiwa Vuai ameyaeleza hayo katika Kongamano la kumuenzi muasisi wa Mapinduzi-marehemu Mzee Abeid Amani karume lililoandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) chini ya mwenyekiti wake Ndugu Sadifah Juma, lililofanyika katika Ukumbi wa chuo cha Ufundi Karume, Mbweni Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa Umoja huo akiwemo Katibu Mkuu wa UVCCM, ndugu Martine Shigela, Makatibu wa Idara za UVCCM na maafisa wengine wa Makao Makuu Bara na Zanzibar, na wajumbe wengine 600 kutoka katika Mikoa mbalimbali ya Zanzibar, pamoja na wawakilishi kutoka vyuo vikuu.
Katika Nasaha zake na salamu za ufunguzi wa Kongamano hilo, Mheshimiwa Vuai alifafanua umuhimu wa kuwaenzi waasisi wa muungano na kusema kuwa vijana wana wajibu wa kutafakari na kujifunza kutokana na viongozi wao waliopita, wajifunze ujasiri, uzalendo na kusimamia misingi ya umoja na utaifa. Alisema kuwa Mapinduzi yalikuwa ni halali kwa kuwa Serikali iliyopinduliwa ilikuwa ni Serikali chini ya Sultan ikinufaisha wachache, hivyo Mapinduzi yalilenga kuleta utawala ulio huru wa watu wa Zanzibar, yalilenga kutetea Uafrika yakiongozwa na mioyo ya kizalendo na nia ya kuijenga Zanzibar na kunufaisha wengi katika wazanzibar wenyewe.
Alisisitiza kuwa muungano una manufaa makubwa kwa wanzanzibar akitolea mifano ya manufaa yanayopatikana katika sekta mbalimbali za kimaendeleo na kijamii ambapo alianza kwa kutaja manufaa yanayopatikana katika sekta ya Elimu ambapo alitaja kuwa kupitia muungano , wanafunzi takribani 1251 waliweza kupatiwa mikopo ya elimu ya juu chini ya bodi ya mikopo ya wanafunzi (HESLB) ikiwa ni wanafunzi si zaidi ya mia nane na sitini (860) ndio ambao waliweza kupatiwa mikopo na Serikali ya Mapinduzi hii ni kulingana na bajeti na uwezo wa Serikali ya mapinduzi.
Lakini pia, Mheshimiwa Vuai alitaja fursa katika sekta ya afya, ambapo akasema kuwa wagonjwa mbalimbali ambao wamekuwa na matatizo makubwa na yanayohitajia utaalamu zaidi wamekuwa wakipelekwa katika Hospitali Kuu ya rufaa ya Muhimbili kama walivyo watanzania wengine kwa gharama ya chini sawa na watanzania wengine, na akasisitiza haya yanapatikana chini ya kivuli cha muungano. Akaeleza pamoja na fursa hii kuwepo kwa fursa nyingine za makazi, biashara n.k
Pamoja na kufafanua juu ya faida na manufaa hayo Mheshimiwa vuai alisema kuwa ni kweli kuwa zipo kero mbalimbali katika muungano, ambapo akasisitiza kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) imejadili na kutoa fursa kwa kero hizo kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi. Mheshimiwa Vuai alisema kama tatizo ni kujiunga na OIC, NEC ya CCM imetoa fursa ya kulijadli hilo na kuruhusiwa ikionekana inafaa, ama ikiwa kero ni mapato ya Bandari, ama mafuta ama takwimu basi NEC imetoa fursa ya kuyajadili haya na ikionekana inafaa yatolewe katika muungano, na pia kulibainisha suala la mahusiano ya kimataifa na suala la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Visiwa Duniani.
Akasisitiza kuwa vijana wasiwe tayari kufuata mawazo ya wapinga mapinduzi na wapinga muungano kwani hao ni watu wanaotaka kurudisha ukoloni kwa mlango wa nyuma, kwa kuwa wanapinga muungano bila ya kuwa na sababu za msingi wala hoja.
“..wakiulizwa kwanini hamtaki muungano hali ya kuwa imetolewa nafasi ya kujadili kero na kasoro zilizopo katika muungano ili uwe bora zaidi na wenye manufaa zaidi, wapinga muungano husema tu kuwa hatutaki muungano, lakini sisi wanaotuita wahafidhina tunajua kuwa wao ni mawakala wa ukoloni na wapinga mapinduzi..” alisema Mheshimiwa Vuai.
Pamoja na kuelezea kwa kina suala la muungano, Mheshimiwa Vuai aliwakumbusha Vijana juu wajibu na jukumu lao la kushiriki katika uchaguzi wa wajumbe wa mabazara ya katiba na kutumia haki yao hiyo ya kidemokrasia.
Kongamano hilo la siku moja lilimalizika saa 12: 15 jioni, ambapo mada mbalimbali kama Mchango wa Marehemu Karume katika Ukombozi wa Zanzibar iliyofikishwa na Ndugu Haji Machano Haji pamoja na mada ya Fursa za Kielimu, Kiuchumi na Kijamii, zilizopatikana baada ya Mapinduzi Matukufu ya January 12, 1964 iliyowasilishwa na Haroun Suleiman (MNEC) na Mada ya Mwisho kuwasilishwa ikiwa ni DHANA YA MAPINDUZI YA JANUARY 12, 1964 na kwanini yalifanyika ikiwasilishwa na Ramadhan A. Ramadhani (MNEC
Post a Comment