Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Aprili 8, 2013 amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu wa Uingereza Mheshimiwa David Cameron kuomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bibi Margaret Thatcher ambaye amefariki dunia asubuhi ya leo kwa ugonjwa wa kiharusi akiwa na umri wa miaka 87.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Cameron: “Nimepokea kwa huzuni na mshtuko mkubwa habari za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Margaret Thatcher, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza. Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Tanzania, nakutumia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kufuatia kifo hicho na kupitia kwako nawatumia salamu kama hizo wananchi wa Uingereza na familia ya marehemu.”
Ameongeza Rais Kikwete: “ Hayati Mheshimiwa Margaret Thatcher alikuwa kiongozi mashuhuri ambaye alisifiwa na kuwavutia wengi kama “iron lady” kutokana na ushawishi wake, msimamo wake thabiti na kiongozi jasiri katika kulinda na kutetea maslahi ya nchi yake pamoja na yale ya jumuiya ya kimataifa. Kwa ajili hiyo atakumbukwa na wengi katika nchi yake na duniani. Kwa hakika, dunia imempoteza kiongozi muhimu ambaye mchango wake daima utakumbukwa.”
Rais Kikwete ameongeza kumwambia Mheshimiwa Cameron: “Mawazo na sala zetu ziko pamoja na wewe, wananchi wa Uingereza na familia ya wafiwa katika wakati huu mgumu wa msiba na huzuni. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi pema roho ya marehemu Mheshimiwa Margaret Thatcher. Amina.”
Mheshimiwa Margaret Thatcher ambaye kabla ya ndoa yake alijulikana kama Margaret Hilda Roberts alizaliwa Oktoba 13, 1987. Alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza na wa pekee mwanamke wa Uingereza. Alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 11 kati ya 1979 na 1990 aliweka rekodi ya kuwa Waziri Mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi katika kipindi cha miaka 150.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
8 Aprili, 2013