Mjukuu wake
aitwaye Omar ameiambia Bongo5 kwa simu muda mfupi uliopita kuwa Bi. Kidude
alikuwa amelazwa kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya sukari na
uvimbe kwenye kongosho.
“Kwa ufupi
alilazwa kipindi kirefu na baadaye akatolewa, lakini baadaye akaja kuendelea
kuumwa tena tukampeleka hospitali tukawa tunampeleka kwenda na kurudi hapa juzi
akaanza kuzidiwa tena tukampeleka hospitali moja inaitwa Keeni (???) Kwaajili ya
matibabu zaidi na drip na vitu vingine lakini baadaye baada ya siku ya tatu
mwenyezi Mungu akachukua roho yake,” amesema
WASIFU WA MAREHEMU FATUMA BINTI BARAKA 'BI
KIDUDE'
Marehemu Bi Kidude alikuwa
ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika. Jina lake halisi ni Fatuma binti
Baraka. Bi Kidude ni msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya muziki wa
mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu.
Muziki huu ambao ni
mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa
Kiafrikaumekita sana katika mwambao wa Afrika
Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Leo hii ni Marehemu! Nguli
na Mtunukiwa wa Nishani ya Uhuru wa Tanganyika/Tanzania 2012, Fatuma binti
Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika
familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara
wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi Kidude aliwahi
kusimulia kuwa hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba
alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla
ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa
hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka
90.
Bi Kidude aliendelea kusema
uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi na alijifunza kutoka kwa
msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad. Anasema wageni
wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na
kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka
wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani
na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye
huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba.
Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa
mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara,
baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa
aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa
akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya
1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini
ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na
shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi
moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo
anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba
na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na ameanzisha chuo chake
mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka
kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima
dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika
mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati
wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine
kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria
hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si
kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya
kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo
ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha
tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja
na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF)
mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda
kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni
pamoja na Muhogo wa Jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi
kupata elimu nyingine zaidi ya Kurani.
Bi Kidude pia amekuwa
akishirikishwa na wasanii wengi wakongwe na chipukizi katika nyimbo zao.
Miongoni mwa nyimbo zinazotamba sana siku hizi ambazo Bi Kifude ameimba na
vijana wa kisasa ni za Msanii Ali Toll maarufu AT.
Mbali na AT lakini pia Bi
Kidude amewika na kung'ara zaidi katika wimbo mwingine wa vijana wa Ahmada
Umelewa wa Msanii Offside Trick ambao umepigwa marufuku kupigwa kwa sasa
visiwani Zanzibar.







R.I.P FATUMA BARAKA “BI KIDUDE”.
on Wednesday, April 17, 2013
Post a Comment