Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es Salaam
Kuelekea uchaguzi wa chama cha Netiboli Tanzania CHANETA utakaofanyika aprili 20 mwaka huu, mikoa kadhaa imeongezeka na kulipa ada ya uanachama ili kupata vitambulisho vya kushiriki uchaguzi.
Akizungumza na mtandao huu, kaimu katibu mkuu wa chama hicho, Rose Mkisi amesema mikoa mingi imeshutuka baada ya CHANETA kuwatangazia siku chache zilizopita kuwa siku ya mwisho ni leo aprili 10.
Mkisi alisema Mkoa mpya wa Simiyu, Tanga na Rukwa tayari wameshakamilisha zoezi la ulipaji wa ada hivyo watashiriki uchaguzi wa chama hicho.
“Tunaendelea kusimamia katiba yetu, siku ya uchaguzi hakuna mtu wa kuingia bila kitambulisho, kama kuna watu wanadhani tunatania wasubiri siku husika ili waone umakini wetu”. Alisema Mkisi.
Kaimu katibu mkuu huyo aliongeza kuwa mikoa iliyobakia ni Kilimanjaro, Kigoma, Mara na Singida, na mapaka sasa hakuna taarifa yoyote kama watalipa ada hiyo ya uanachama ama la.
“Kama wana nia ya kuja kwenye uchaguzi, nafasi bado ipo, ili uwe mwanachama hai lazima uwe na kitambulisho, sisi tutakuwepo hadi tarehe 19 usiku, kama mkoa wowote utahitaji kulipia itawezekana tu”. Aliongeza Mkisi.
Mkisi alisema uchaguzi wa Chama hicho umetangazwa kwa muda mrefu sana na kila mwanachama anajua, hivyo kama mtu atalaumu kwa maamzi yoyote basi atakuwa na lake la moyoni.
Pia alisisitiza kuwa usaili wa wagombe wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho utafanyika aprili 18 huku siku inayofuata ikiwa ni nafasi kwa wanachama kupumzika na kujiandaa na zoezi la uchaguzi litakalofanyika aprili 20 mwaka huu.
Mkisi aliongeza kuwa mwaka huu wanatarajia kufanya uchaguzi huru na haki, sheria na katiba itafutwa kwa kiasi kikubwa.
CHANETA Ni moja ya taasisi kubwa za kimichezo nchini Tanzania inayoongoza mchezo wa Netiboli ambao kwa sasa unafanya vizuri sana hususani timu ya taifa ya Netiboli, Taifa Queens.
Post a Comment