Afisa Ubalozi wa
Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bw. Justin Kisoka ambaye pia
alikuwa Mratibu wa Kamati ya Tano inayohusika na masuala ya Utawala na
Bajeti akiwasilisha siku ya Ijumaa, taarifa ya Kamati hiyo mbele ya
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo ilihusisha maazimio
Nane ambayo Baraza Kuu liliyapisha kwa kauli moja, likiwamo lile
linaloidhinisha ujenzi wa Majengo ya Taasisi ya Kimataifa ya Kumalizia
Mashauri ya Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya
Kimbari ( ICTR) Tawi la Arusha. Majengo hayo ya kisasa yatajengwa katika eneo
la Lakilaki Jijini Arusha.
*********
Na Mwandishi Maalum
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha
kwa kauli moja Azimio linalopendekeza kuidhinishwa kwa hatua
zote za Ujenzi wa Mradi wa Taasisi mpya ya
Kimataifa itakayochukua majukumu ya Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR).
Mradi huo wa majengo ya kisasa, utajengwa katika eneo la LakiLaki
Jijini Arusha-Tanzania na utahusisha Ofisi, vyumba vya
mahakama, na sehemu ya kutunzia nyaraka na kumbukumbu zote za ICTR.
Eneo hilo la Laki Laki limetolewa na Serikali ya Tanzania kwa Umoja wa
Mataifa.
Baraza Kuu limepitisha Azimio hilo katika
mkutano wake uliofanyika siku ya Ijumaa ( April 12),mkutano ambao pia,
Baraza lilipokea na kupitisha maazimio mengine Nane
yaliyowasilishwa na Kamati ya Tano inayohusika na masuala ya
Utawala na Bajeti katika Umoja wa Mataifa.
Taasisi hiyo mpya ijukulikanayo kama Mfumo wa Kimataifa wa
Kumalizia Mashauri Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari au kwa kimombo ( International Residual Mechanism for
Criminal Tribunal )- Tawi la Arusha pamoja na kuhifadhi nyaraka
itasimamia kesi za Masalia ambazo zitakuwa bado hazijakamilia baada ya
ICTR kumaliza muda wake mwakani.
Azimio hilo pamoja na mambo mengine, linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, kuweka bayana uwajibikaji na uangalizi wa kina katika ujenzi wa mradi
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria, taratibu, kanuni na
miongozo yote ya Umoja wa Mataifa inayohusu
manunuzi/ugavi inafuatwa ipasavyo katika utekelezaji wa mradi huu.
Gharama za mradi
zinatarajiwa kuwa kiasi cha dola za kimarekani 8.78 Milioni ( takribani
Sh.14 Bilioni). Fedha hizi zinalipwa na Nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa. Mradi unatarajiwa kukamilika kabla ya mwishoni mwa mwaka
2015.
Aidha kupitia Azimio
hilo, Baraza Kuu pia limeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa kuendelea na jukumu la kufuatilia kwa karibu mchakato
wote unaohusiana na utekelezaji wa mradi na vilevile katika kuhakikisha kwamba
inashirikiana na Umoja wa Mataifa kufanikisha Mradi huu.
Halikadharika
kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu limeelezea kufurahishwa
na maendeleo ya utekelezaji wa mradi hasa kwa kutumia ujuzi wa ndani,
(Local knowledge) katika ubunifu wa majengo (design),
upatikanaji wa meneja wa mradi na maandalizi ya kina ya gharama za
ujenzi.
Pamoja na pendekezo
la kuidhinishwa kwa hatua za ujenzi wa mradi , Baraza pia
kupitia Azimio hilo , linamtaka KatibuMkuu kufanya juhudi
zote zitakazo pelekea kupunguza muda wa ujenzi wa mradi .
Katika hatua
nyingine, Baraza Kuu pia linamtaka Katibu Mkuu kuanza
mazungumzo na Asasi nyingine za Kimataifa ikiwamo ile ya Mahakama Afrika
itakayoshughulikia Haki za Binadamu, juu ya namna bora
ya kushirikiana katika matumizi ya miundo mbinu hiyo katika siku za
usoni.
Mwaka 2010 Baraza Kuu
la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Azimio nambari 1966 la
kuanzisha Mfumo wa Kimataifa utakaomalizia Mashauri ya Masalia kwa
zilizokuwa Mahakama za Kimataifa za Mauaji ya Kimbari yaliyotokea
nchini Rwanda ( ICTR) na Mauaji ya halaiki yaliyotokea katika
iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani ( ICTY).
Katika azimio hilo
Baraza Kuu la Usalama lilibainisha wazi kwamba Arusha ndiyo itakuwa
makao ya Tawi la mfuno huo mpya na The Hague ikiwa ni makao
ya Tawi jingine.
Post a Comment