KUNDI la wafanyabiashara walemavu wamevamia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ilala kupinga kuondolewa kwenye eneo wanalofanya biashara, Buguruni Chama jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabishara Walemavu Dares Salaam (UWAWADA), Mohamed Kidumke, alisema walikabidhiwa barua ya kuwataka kuondoka katika eneo hilo Aprili 4 mwaka huu, ambako barua hiyo inaonesha kuwa iliandikwa tangu Januari 24 mwaka huu.
Alisema chimbuko la kutakiwa kuondoka katika eneo hilo ni kutokana na madai kuwa wafanyabiashara hao wamevamia eneo la hifadhi ya barabara.
Kidumke alisema walikwenda kumuomba Mkurugenzi abatilishe uwamuzi huo kutokana na walemavu hao kutegemea biashara katika shughuli za maisha yao ikiwemo kulipia ada za shule na mikopo waliokopa kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya biashara hizo.
“Angalia hii barua inavyotuelekeza kuwa kwa notisi hii tunaamriwa kuondoa umbo au biashara tulizoweka katika hifadhi ya barabara ndani ya siku saba kuanzia tarehe ya notisi hii”alisema Kidumke.
Kidumke alisema hiyo ni mara ya pili kwa Halmashari hiyo kutaka kuwaondoa katika eneo hilo ambapo mara ya kwanza walishindwa baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuingilia kati ikidai waachwe kwa kuwa vibanda vyao ni vya kusogea pindi wangehitaji kupanua barabara hiyo wangewataka wavisogeze.
“Unajua hili eneo si la Halmashauri bali ni la TANROADS), tunashangaa kuona wanatufuata tena leo tumekuja atueleze lakini tumefika hapa tunaambiwa hayupo wakati tulimuona”alisema.
Kidumke aliongeza kuwa wanashangazwa na hatua hiyo wakati mwaka 2007, vibanda hivyo vya walemavu vilitakiwakuondolewa sambamba na urekebishaji, uvunjaji wa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Buguruni na Mabanda ya Mama/ Baba lishe.
Naye Msemji wa Halmashauri hiyo, Tabu Shaibu aliwataka wafanyabiashara hao kufanyasubira ili waweze kuonana na Kaimu Mkurugenzi ili aweze kuwatatulia shida zao.
credits: Fullshangwe
Post a Comment