Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma.
Ili kuhakikisha watoto walio katika mazingira hatarishi hususan watoto waliotelekezwa, wanaonyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili zinalindwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Halmashauri na Wadau wa Maendeleo zimeanzisha program ya ulinzi na usalama kwa kuundwa timu za ulinzi katika ngazi ya Halmashauri, Kata na Vijiji.
Hayo yamesemwa leo Bungeni na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Dk. Seif Seleman Rashidi akijibu maswali kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii toka kwa Mbunge wa viti Maalum, Mhe. Anna Marystella John Mallac.
Dk. Seif amesema kuwa sheria ya mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 43 kinaeleza kuwa mama wa mtoto aliyetelekezwa anawajibika kuwasilisha shauri la matunzo ya mtoto katika vyombo vya sheria.
Aidha, Dk. Seif amesema kuwa Wizara yake kama msimamizi na mtekelezaji mkuu wa sheria hiyo, baada ya kupokea mashauri ya aina hiyo hufanya mawasiliano na Wakala wa Kimataifa wa Huduma za Jamii (International Social Service) ili kuweza kufanya uchunguzi na ufuatiliaji katika upande wa mlalamikiwa ambaye ndiye anayedhaniwa.
Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi huo, inapothibitika pasipo shaka yoyote kuwa mlalamikiwa ndiye baba halisi wa mtoto husika, taratibu za malezi, matunzo na ulinzi wa mtoto huyo hufanywa kwa kutumia Ofisi za Balozi za Nchi husika.
“Wizara yangu inalo jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za malezi, matunzo na ulinzi wa watoto waliozaliwa nje ya ndoa kwa mujibu wa sheria ya mtoto Na. 21 ya mwaka 2009”. Naibu Waziri alisema.
Akijibu swali la nyongeza toka kwa Mbunge huyo lililotaka kujua kama serikali iko tayari kutoa elimu kwa akina mama walioathirika na matukio ya namna hiyo, Mhe. Mbunge Sophia Mattayo Simba amekiri kuwepo kwa matukio kama hayo na ameshauri matumizi ya uzazi wa mpango na matumizi ya kinga.
Amesema katika mwaka 2013/2014 programu ya ulinzi na usalama itasambazwa katika Halmashauri 25. Hivyo, kupitia program hii matukio ya unyanyasaji, utelekezaji na ukatili kwa watoto yatazuiwa na kushughulikiwa ipasavyo.



Post a Comment