MKAZI wa kijiji cha Turiani, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga,
Athuman Rashid (25) amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela na
adhabu ya kuchapwa viboko sita baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti
mtoto wa miaka saba.
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe, Arnold Kirekiano.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa na
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Janson Zakaria alidai Athuman alitenda
kosa hilo Juni 21 mwaka jana, saa 11.00 jioni katika kijiji cha Turiani
wilayani hapo.
Hati hiyo ya mashitaka inadai Athuman alimuita mtoto huyo ambaye alikuwa
akiishi na bibi yake kijijini hapo kwa lengo la kumtuma dukani ndipo
alipomtendea unyama huo.
“Alipokuwa akifanyiwa tendo hilo mtoto huyo alipiga kelele na baadhi ya
majirani kujitokeza kufika eneo hilo huku, mtoto huyo akilalamika kwa
maumivu sehemu ya siri na akimtaja mtuhumiwa,” alidai Zakaria.
Kabla ya Hakimu Kirekiano kutoa hukumu alimtaka mshitakiwa kama ana
chochote cha kujitetea aeleze mahakamani; naye akasema hana cha
kujitetea, Mahakama iamue.
Hakimu alisema kifungo hicho cha maisha jela na viboko sita, iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Post a Comment