*****
Mwanza. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta amesema wakati ukifika, yeye na rafiki zake
Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri
wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe, watachagua mmoja wao watakayeona anafaa kuwania urais katika
Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Waziri Sitta aliyasema hayo jana katika Kongamamo
la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya
Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Mwanza.
Mara ya kwanza, Sitta aliwataja rafiki zake hao
juzi wakati wa harambee ya kuchangia Kanisa Katoliki, Josephine Bakita,
Parokia ya Igoma, Mwanza.
Pia alisema hatagombea tena Ubunge Urambo ya
Mashariki baada ya kuwa katika ulingo wa siasa kwa miaka 35 na badala
yake ataangalia namna nyingine ya kuwatumikia wananchi huku akigusia
mchakato wa kuwania urais ambao, alisema anamwachia Mungu.
“Kwa ubunge nimekwisha waeleza inatosha sitagombea
tena kwani miaka 35 inatosha, … lakini hatima yangu ni nini siwezi
kujua lakini nina afya nzuri na mmoja wa wanasiasa wakongwe, wenye afya
nzuri, mnaona ninavyopendeza... kwa urais namwachia Mungu tutaona,”
alisema Sitta.
Alisema yeye rafiki zake hao wana mawazo
yanayolingana katika mustakabali wa nchi hii na kwamba wataendelea
kutembea sehemu mbalimbali za nchi kuwajengea wananchi uelewa ili wajue
kuwa uongozi ni lazima ukae katika mikono salama.
“Tutaendelea kupita katika nchi hii kuwaeleza
wananchi kujua uongozi wa nchi hii lazima ukae katika mikono safi na
ikitokea mmoja wetu akatamani urais, basi tutaona inavyofaa, lakini
tutasubiri watu wanavyosema pia kuhusiana na nasi,” alisema.
Akijibu swali la mwanafunzi wa SAUT kuhusiana na
kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita
ilhali akijua kwamba hawezi kuwaletea maisha bora wananchi, alisema
kwake ilikuwa ni sawa na kuchumbia na kwamba wakati wa uchumba, mchumba
huonekana kuwa bora lakini anaweza kubadilika wakati wa ndoa.
“Sikufanya kosa kuwa katika mtandao wa Rais
Kikwete, hii ni sawa na kuoa. Unachumbia. Mchumba hawezi kuwa sawa
wakati wa ndoa au wa kuwa mke, inawezekana katika kugombea mtu akawa
sawa lakini baadaye akajifunua zaidi mambo yake, huwezi kumjua zaidi mtu
labda uwe na Umungu,” alisema Sitta na kusema: “Hata wapiga kura
huwakuta hilo kwa kuchagua mtu ambaye huenda kinyume na matarajio yao.”
Hata hivyo, alisema kauli hiyo haina maana kwamba
Rais Kikwete hakufanya kitu, bali amefanya mambo mengi na kusema uzuri
wa uongozi unapimika wakati anapotoka madarakani hasa pale historia
inapoandikwa na kulinganishwa na marais wengine wajao na waliopita.
Katika kongamano hilo la SAUT, Waziri Sitta alifuatana na kada wa CCM, Paul Makonda.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment