Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini Magharibi
Bwana Mohd Omar Said { Maarufu Kidevu } akielezea mkasa uliompata wa
kumwagiwa Tindi kali { Acid } mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja
kumfariji.
Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
********
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Bwana Mohd Omar Said
{ Maarufu Kidevu } anaendelea kupatiwa huduma za matibabu katika
Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja baada ya kumwagiwa Tindi kali { Acid } na
mtu asiyejuilikana.
Mkasa huo umempata jana usiku mara baada ya kurejea ibada ya sala
ya Isha wakati akiendelea na harakati za kutafuta huduma za maji na
kumwagiwa tindi kali hiyo iliyoathiri eneo la kifua chake, Bega pamoja
na sehemu za jicho la kulia.
Hili ni tukio la tatu kutokea ndani ya mkoa wa mjini Magharibi
likiwahusisha aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu
Rashid Ali Juma pamoja na Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil
Suleiman Soraga.
Sheha huyo wa Tomondo Bwana Mohd Omar Kidevu akizungumza na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali
hapo kumfariji pamoja na kumpa pole alisema alijikuta akimwagiwa tindi
kali majira ya saa 2.00 za usiku na mtu asiyemfahamu.
Bwana Mohd Kidevu alisema Mtu huyo alianza kutimua mbio baada ya
kufanikiwa kufanya dhambi hiyo kitendo ambacho akalazimika kuomba msaada
kwa wasamaria wema lakini hatimae ilishindikana kutokana na kuzidiwa
kwa maumivu makali yenye kuchoma kama moto.
Sheha huyo wa Shehia ya Tomondo aliendelea kumfahamisha Balozi Seif
kwamba hali yake hivi sasa inaendelea vyema na ameshaanza kupata
matumaini kufuatia jicho lake kuanza kuona ingawa bado anakabiliwa na
maumivu katika sehemu yake ya usoni.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimuomba Sheha
huyo wa Tomondo kuwa na moyo wa subra wakati wa kipindi hichi kigumu
cha huduma za matibabu.
Balozi Seif alimuhakikishia Bwana Mohd Kidevu kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufuatilia ushauri utakaotolewa na
Madaktari kuhusu tiba ya afya yake na kutoa msaada wowote utakaohitajika
ili kuendeleza nguvu za huduma ya tiba yake.
“ Tutafuatilia ushauri watakaotupa Madaktari kuhusu afya yao. Na
kama kuna wazo la kukusafirisha iwe Hospitali ya Rufaa Muhimbili au Nje
ya Nchi basi sisi kama Serikali tuko tayari kulitekeleza hilo “. Balozi
Seif alimuhakikishia Sheha Mohd Kidevu.
Akizungumza na vyombo vya Habari nje ya Wodi ya Mapinduzi Kongwe
katika Hospitali Kuu ya Mmnazi Mmoja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali Kuu imesikitishwa na vitendo hivi
viovu vinavyoleta athari kwa Binaadamu.
Balozi Seif alisema tabia hii mbaya inayoonekana kuanza kuchipua
hapa Nchini ikibeba ufinyu wa imani inaanza kuleta hofu miongoni mwa
wananchi katika kuendelea na harakati zao za kimaisha za kila siku.
Alisema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi itaendelea na
uchunguzi wa kufuatilia matukio hayo na haitasita kuwachukulia hatua za
kisheria kwa kuwafikisha katika mkondo wa sheria.
Zanzinews
Post a Comment