Dar es Salaam. Mpenzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa, Josephine Mshumbusi ameshinda rufaa ya kupinga talaka yake, iliyofunguliwa na aliyekuwa mumewe wa ndoa, Aminiel Mahimbo.
Josephine kwa sasa amekuwa akiishi na Dk Slaa na
tayari wamefanikiwa kupata mtoto mmoja, lakini harakati zao za kufunga
ndoa zimekwama baada ya kupingwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema,
Rose Kamili akidai kuwa ana ndoa halali na Dk Slaa.
Mahimbo alikata rufaa hiyo katika Mahakama ya
Wilaya ya Kinondoni, akipinga hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza
iliyotoa talaka kwa Josephine dhidi yake, mwaka 2012.
Pamoja na mambo mengine, Mahimbo katika rufaa yake
hiyo namba 32/2012, alikuwa akidai kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha
kiasi cha kuifanya Mahakama ya Mwanzo Sinza kutoa talaka hiyo.
Hata hivyo jana, Hakimu Aniseth Wambura
aliyesikiliza rufaa hiyo, aliitupilia mbali ombi hilo akisema kuwa
ameridhika na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza kwamba kulikuwa na
ushahidi wa kutosha kutoa talaka kwa Josephine.
Hakimu Wambura alisema katika hukumu hiyo,baada ya
kupitia hoja za mrufani na za mjibu rufaa pamoja na mwenendo wa kesi ya
msingi,amekubaliana na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza kuwa ni
sahihi.
Katika kesi ya msingi Josephine, alidai talaka
kutoka kwa Mahimbo, pamoja na kudai kuwa Mahimbo hakuwa mwaminifu kwa
kuwa alikuwa akitoka nje ya ndoa na kwamba alikuwa amemtelekeza bila
kumpatia mahitaji na huduma za msingi, huku akimtesa.
Hakimu Wambura katika hukumu yake jana kwenye
rufaa hiyo alisema, kutokana na sababu zilizotolewa na Josephine katika
kesi ya msingi ni dhahiri kuwa hapakuwa na ndoa na kwamba mahakama
haiwezi kuwalazimisha watu ambao hawapatani kuishi pamoja.
“Baada ya kusikiliza hoja za mrufani na mjibu
rufaa ,mahakama hii imekubaliana hoja za mjibu rufaa (Josephine), kuwa
kwa tabia ile mbaya na ukosefu wa uaminifu katika ndoa yake hapakuwapo
na ndoa baina yao.”, alisema Hakimu Wambura.
“Hivyo mahakama hii inatangaza kuwa hukumu ya
Mahakama ya Mwanzo Sinza ambayo iliivunja ndoa hiyo ilikuwa sahihi,”
alisema kwa msisitizo Hakimu Wambura.
Wakili wa Josephine, Philemon Mutakyamilwa alisema
kuwa amefurahishwa na hukumu hiyo akidai kuwa mahakama hiyo imetenda
haki kwa mteja wake.
Licha ya kupangua kikwazo hicho, Josephine bado
anakabiliwa na kikwazo kingine kilichomweka njia panda katika mipango
yake ya kufunga ndoa na Dk Slaa. MWANANCHI
Post a Comment