Mkurugenzi wa
Idara ya Kinga Dr. Salhia Muhsin Ali akitoa maelezo mbele ya Kikao cha
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Wanafunzi
wanaosoma mafunzo ya Udaktari katika Chuo cha Afya waliopo Wawi Kisiwani
Pemba
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wanafunzi 12 wa Chuo cha Afya wanaosomea fani ya Udaktari waliopo Kisiwani Pemba.
Rais wa Wanafunzi
wa chuo cha afya waliopo Kisiwani Pemba Ali Omar Khalifa akitoa baadhi
ya changamoto zinazowakabili wanafunzi wa chuo cha afya waliopo Kisiwani
Pemba.
Mwalimu Mkuu wa
Wanafunzi wa Chuo cha Afya waliopo Pemba Dr. Maria Makdalema akielezea
furaha yake kutokana na umahiri wa wanafunzi wake mbele ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipowatembelea kwenye makazi yao
Wawi Pemba.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwalimu Mkuu wa
Wanafunzi wa chuo cha Afya waliopo Kisiwani Pemba Dr. Maria Makdalema.
Pembeni yao ni Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Mkasha Hija Mkasha na Mkurugenzi Idara ya Tiba Zanzibar Dr. Salhia Muhsin Ali.(Picha na Hassan Issa, OMPR.)
.................................................
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kumgharamia mwanafunzi yeyote atakayeamua kujiongezea taaluma ya fani yoyote ya Udaktari Bingwa kwa lengo la kuiondoshea Zanzibar uhaba wa Madaktari.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati
akizungumza na Wakufunzi pamoja na Wanafunzi wa chuo cha afya wanaosomea
fani ya Udaktari chini ya Wataalamu wa Cuba hapo Wawi chake chake
Pemba.
Balozi Seif alisema
uwamuzi huo wa serikali umelenga kukidhi ule Mpango wake uliojipangia
wa kuimarisha huduma za Afya katika kila umbali wa Kilomita Tano katika
Visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wanafunzi hao kwa ushiriki wao wa mafunzo
hayo ya miaka saba na kuelezea matumaini yake kwamba wamalizapo mafunzo
hayo ni kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya Udaktari.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kuwa na Madaktari 50 kwa mpigo jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa Serikali “. Alionyesha furaha yake Balozi Seif.
“ Historia ya kuanzishwa kwa darasa la Madaktari Zanzibar limetokana na ziara ya Dr. Sheni Nchini Cuba wakati akiwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika miaka ya 2008 “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba
wazo hili lililotolewa na Cuba lilikuwa na nia ya kusaidia gharama za
usomeshaji ambazo ni kubwa pamoja na udhibiti wa wanafunzi hao ambao
wakisoma nje ya nchi wanakuwa na mawazo ya kuikimbia nchini.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar ameahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaangalia na kuimarisha mazingira ya walimu pamoja na wanafunzi hao ili
waweze kufanikisha lengo lililokusudiwa chuoni hapo.
Alisema haipendezi
kuona wataalamu hao wamekubali kujitolea kusaidia wananchi wa Tanzania
na Zanzi bar kwa ujumla na mazingira yao hasa makazi yanakuwa hayako
katika hali ya kuridhisha.
Wakitoa baadhi ya
changamoto zinazowakabili Wanafunzi hao wa Udaktari walisema upungufu wa
vifaa limekuwa tatizo sugu linalorejesha nyuma mafunzo yao ya kila
siku.
Waliiomba Serikali kupitia Wizara ya afya kuyafanyia kazi matatizo hayo likiwemo pia tatizo la mtandao wa Internet kwa wakufunzi wao sambamba na usafiri wanakwenda na kurudi kwenye mazoezi hasa wakati wa usiku.
Wanafunzi hao wa
Udaktari wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake
huo wa kuanzisha mafunzo hayo hapa Nchini ambao utapunguza gharama
kubwa.
Naye kwa upande
wake Mwalimu Mkuu wa Darasa hilo Dr. Maria Makdalema kutoka Nchini Cuba
ameelezea furaha yake kutokana na umahiri mkubwa walionao wanafunzi
wake.
Hata hivyo Dr.
Maria alisema `ukosefu wa vifaa vya mazoezi unawapa mazingira magumu
wanafunzi hao katika kujipatia mazoezi ya vitendo ambayo ni muhimu
katika mafunzo yao.
Mapema Mkurugenzi
Idara ya Tiba ambae ndie anayeratibu mafunzo hayo Dr. Salhia Muhsin Ali
alisema mafunzo hayo ya Udaktari yamejumuisha wanafunzi 50 ambao 38 kati
yao wapo Unguja na 12 Kisiwani Pemba.
Dr. Salhia alieleza
kwamba wanafuzi 38 wa Unguja hivi sasa wako katika hatua ya mwisho
kumaliza mafunzo yao ya miaka saba wakati wale 12 wa Pemba wanaingia
mwaka wa nne wakiwa katika mkupuo wa tatu.
Katika Mkutano huo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alichangia shilingi Laki
Tano kusaidia ununuzi wa Vifaa muhimu vidogo vidogo na kuahidi Serikali
Kuu kuyafanyia kazi yale matatizo mengine makubwa likiwemo lile la
upatikanaji wa Projector.
VIA/www.zanzinews.com
Post a Comment