POLISI mkoani Mwanza inashikilia risasi 277 zilizookotwa
vichakani na raia wema katika eneo la Lumala, wilayani Ilemela mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu (Pichani) alisema juzi walipokea taarifa kutoka eneo hilo
kuwa zimeokotwa risasi 277 za silaha ya kivita aina ya SMG.
Kwa mujibu wa Kamanda, risasi hizo zilitupwa katika eneo
hilo na zilikutwa kwenye galoni ya lita tano baada ya kuokotwa na raia wema.
Inasadikiwa zilitupwa na wahalifu ambao jeshi hilo bado
linaendelea kuwasaka katika
operesheni yake inayoendelea kwenye wilaya za Sengerema,
Kwimba na Magu.
Kamanda Mangu amezihusisha risasi hizo na majambazi
mawili waliouawa wiki iliyopita wakati wakirushiana risasi na polisi walipotaka
kufanya uporaji katika duka la wakala wa Kampuni ya Bia (TBL) katika eneo la
Igoma.
“Itakumbukwa kuwa Mei 18, Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na wananchi waliwaua majambazi wawili waliojaribu kufanya uporaji
eneo la Igoma ambao walikuwa na silaha aina ya SMG,” alisema Kamanda Mangu.
Alisema baadaye ilifahamika kuwa majambazi hao walikuwa
ni wahalifu sugu ambapo waliwahi kukamatwa wakiwa na risasi 597 za SMG kisha
kufungwa jela.
CHANZO: HABARILEO
Post a Comment