* ATANGAZA KUANCHANA NA UBUNGE IFIKAPO MWAKA 2015.
WAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta (pichani), amewatuhumu
viongozi wenzake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa walishiriki
kwenye njama ovu za kumnyang’anya uspika kwa sababu waliogopa spidi na
viwango vyake.
Sitta alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (SAUT), Mwanza.
Ingawa Sitta hakuwa tayari kutaja majina ya viongozi hao waliomhujumu,
ni wazi kuwa tuhuma hizo zinamwelekea moja kwa moja Rais Jakaya
Kikwete, amb
Inafahamika pia kuwa Rais Kikwete ndiye aliyeleta wazo la kuwa na spika mwanamke, kigezo ambacho Sitta asingeweza kukitimiza.
Awali kabla ya kufanyika kwa vikao hivyo mwaka 2010 kulikuwa na tetesi
kuwa Sitta hatakiwi kurejea kwenye kiti hicho kwa sababu alichangia
kushamiri kwa upinzani na migogoro ndani ya CCM.
Baadhi ya wagombea wa CCM waliojitokeza kuchuana na Sitta katika
kuwania nafasi hiyo ni Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, na Anna
Makinda. Itakumbukwa kuwa wakati anagombea uspika, Sitta alikuwa ndiye
Spika kwa miaka mitano iliyotangulia (2005-2010).
Alisema hujuma hiyo ililenga kumstaafisha kwa lazima kabla ya muda
wake, kwa kisingizio cha wakubwa zake hao kutaka Bunge liongozwe na
mwanamke, jambo ambalo alionekana kutoridhishwa nalo.
“Siku zote mimi ni mtu wa viwango na ukweli. Hata wakati nilipokuwa
Spika wa Bunge, baadhi ya wakubwa zangu wa kazi hawakufurahishwa na
uwazi, viwango na spidi yangu ya kuongoza Bunge.
“Kwa sababu ya baadhi ya wakubwa wangu kutofurahishwa na viwango
vyangu, nilistaafishwa Uspika kabla ya muda wangu. Sababu na kisingizio
chao, eti huu ni wakati wa Bunge kuongozwa na mwanamke!. Hii mmh,”
alisema.
Wajuzi wa siasa ndani ya CCM wanasema kwamba hii ilikuwa mara ya pili
kwa Rais Kikwete “kumhujumu” Sitta. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2005
kwa kumnyima uwaziri mkuu ambao Kikwete alikuwa amemuahidi wakati wa
mchakato ndani ya kundi lake la wanamtandao.
Katika mtandao huo, Kikwete alikuwa na watu wawili aliokuwa amewaahidi
uwaziri mkuu – Sitta na Edward Lowassa – kila mmoja kwa muda wake. Hata
hivyo, habari za ndani zinaeleza kuwa mara baada ya kushinda, Rais
Kikwete alibadili msimamo, kwa kigezo kuwa alikuwa anapata wakati mgumu
kumpa uwaziri mkuu mtu ambaye (yeye Kikwete) angemmwamkia “shikamoo.”
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa njama za kumwondoa Spika aliyekuwapo, Pius
Msekwa, na kumhamasisha Sitta agombee uspika. Kundi la wanamtandao
lilimpiga vita Msekwa likimwita “agano la kale,” likahakikisha Sitta
anapita.
Hata hivyo, Sitta alifanya kazi ya uspika kwa msuguano mkubwa kati
yake na Waziri Mkuu wa wakati ule, Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu
mwaka 2008 kwa shinikizo la Tume ya Bunge kuhusu kashfa ya kampuni tata
ya kufua umeme, Richmond.
Kuhusu ufisadi, Sitta alisema amejipambanua kupambana nao pasi na woga
kwakuwa anaamini hiyo ndiyo nia nzuri ya kuliokoa taifa.
Aliongeza kuwa wapo baadhi ya watu hapa nchini wanafanya biashara ya unyonyaji na wanasafirisha fedha nje ya nchi.
Alisema biashara hizo za kiunyonyaji ndizo zinazosababisha mikopo ya
elimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuendelea kucheleweshwa, na aliwataka
wasomi na Watanzania wote kutokukubali nchi kushikwa na mafisadi, kwani
watu hao ni hatari na hawana huruma na uchumi wa taifa.
“Mpaka leo hii namsifu sana Baba wa Taifa, hayati mwalimu Julius
Kambarage Nyerere kwa uadilifu aliokuwa nao. Aliona mbali, alipiga vita
ukabila na unyonyaji wa rasilimali za nchi. Hivyo, tusiruhusu tabaka la
watu wanyonyaji kuongoza uchumi wa taifa hili,” alisema
Sitta.
Alisema, yeye binafsi kamwe hakubaliani na vitendo vya kifisadi
vinavyofanywa na baadhi ya watu, hivyo wasomi na Watanzania wasiunge
mkono watu walioihujumu nchi kupitia mikataba mingi mibovu ya kifisadi.
Aidha, Waziri Sitta alieleza kusikitishwa na usiri wa mambo unaofanywa
na Serikali kuhusu maendeleo ya nchi, na alitaka usiri huo usiwepo,
huku akihoji: “Utaendeshaje nchi kwa usiri? Kwa nini ufanye siri kuhusu
mambo ya kimaendeleo kwa wananchi wako ?”.
Aliponda pia kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi wa nchi unaoonekana sasa
kwa kukua kwa asilimia 6.9 kwa mwaka, badala ya kukua kwa asilimia 10
hadi 12 kwa mwaka, na aliwalaumu baadhi ya viongozi nchini kutazama
suala la kuongeza ajira badala ya kupigania ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kustaafu ubunge
Alisema hivi sasa anafikiria kustaafu ubunge, na tayari ameshawaambia wapiga kura wa Urambo Mashariki juu ya azima yake hiyo.
Alisema ni vema na viongozi wengine wakafikiria kustaafu siasa baada ya kuwatumikia wananchi kwa kipindi kirefu.
“Viongozi wenzangu msipende kung’ang’ania madaraka. Nawaombeni
mjifunze kusema yatosha …staafuni kama ninavyotaka kufanya mimi,”
alisema.
Jitihada za kupata wasaidizi wa Rais Kikwete kuzungumzia kauli ya
Sitta hazikuzaa matunda, kwani simu zao katika kitengo cha mawasiliano
Ikulu, zilikuwa zimezimwa hadi tunakwenda mitamboni.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment