DODOMA, Tanzania
Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano
wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, akizungumza na waandishi wa habari
leo, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma. Amezungumzia kuhusu yaliyojiri
kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kilichofanyika jana, pia mjini
Dodoma. (TAARIFA NA PICHA
TAARIFA KAMILI KAMA ILIVYOTOLEWA NA DK. ASHA-ROSE
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya
Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilifanya kikao chake cha kawaida
mjini Dodoma Mei 21, 2013 chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho
Kikwete. Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu ilijadili na kutafakari
masuala mbali mbali yanayohusu Uchumi, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya
Taifa.
MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI
Migogoro ya wakulima na wafugaji
imekuwa mingi na imeenea sana katika taifa letu. Migogoro hii inatokana
na sababu nyingi: mabadiliko ya tabia nchi; ongezeko la idadi ya watu
na mifugo. Kamati Kuu inasikitishwa na kuendelea kwa migogoro hii ambayo
imekuwa tishio la amani na usalama katika jamii, na pia kusababisha
wakulima kupata hasara baada ya mazao yao kuliwa na mifugo.
Tumeishuhudia migogoro hii mkoani Morogoro hivi karibuni, katika ziara
ya Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana na imeripotiwa katika maeneo
mengine ya nchi yetu.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali
kuishughulikia na kuitafutia ufumbuzi wa kudumu migogoro hii. Kamati Kuu
inaiagiza Serikali kuharakisha zoezi la kutenga maeneo kwa ajili ya
wakulima na wafugaji na kujenga miundombinu ya malisho, maji, na majosho
ili kuwezesha wafugaji kutohamahama na mifugo yao.
KULINDA HIFADHI
Kamati Kuu imezungumzia suala la
mahusiano kati ya Hifadhi za taifa, wafugaji na wananchi waishio katika
vijiji vinavyozunguka Hifadhi hizo. Kamati Kuu inatambua umuhimu wa
Hifadhi kwa manufaa ya taifa letu na vizazi vijavyo. Inasisitiza msimamo
wake wa kuzilinda Hifadhi za taifa sanjari na kuanzisha na kuendeleza
mahusiano hayo.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali
kuwashirikisha wananchi katika kutenga maeneo ya Hifadhi, kulinda maeneo
ya wanyama pori na kutenga maeneo ya malisho ili kuondosha migogoro
isiyo ya lazima katika maeneo yanayozunguka Hifadhi.
ZAO LA KOROSHO
Kamati Kuu ilijadili matatizo
yanayolikabili zao la korosho ambayo ni: kuyumba kwa bei ya korosho,
malipo ya wakulima kuchelewa, tozo nyingi wanazolipishwa wakulima na
udhaifu wa baadhi ya vyama vya ushirika.
Tatizo hili limedumu kwa muda mrefu na linastahili kushughulikiwa kwa njia ya kipekee.
Kwa kutambua kwamba wapo baadhi
ya viongozi na watendaji wa Serikali, viongozi wa vyama vya ushirika
na wafanyabiashara binafsi wanaochangia katika kuendeleza matatizo
yanayowakabili wakulima wa korosho:
Kamati Kuu inatamka kwamba hali
hii haivumiliki. Kamati Kuu inaitaka Serikali kukaa na wadau wote na
kuchukua hatua zitakazotoa ufumbuzi wa kudumu wa matatizo haya kwa zao
la korosho. Kamati Kuu pia inaitaka Serikali kuwachukulia hatua za
kisheria hao wote wanaochangia kuendelea kwa matatizo haya kwa
wakulima wa korosho.
MIGOGORO YA KIDINI
Kamati Kuu imepokea taarifa ya namna migogoro ya kidini inavyoshughulikiwa na hatua zinazochukuliwa. Kamati Kuu inaipongeza Serikali na vyombo vya dola kwa namna inavyoendelea kukabiliana na wahalifu wanaotumia mgongo wa dini kuanzisha vurugu na uvunjifu wa amani katika nchi yetu. Kamati Kuu inatoa mwito kwa Watanzania kukataa vitendo vyote vinavyochochea migogoro ya kidini; wananchi wajihadhari na watu waovu wenye nia mbaya ya kuligawa taifa letu.
Kamati Kuu imepokea taarifa ya namna migogoro ya kidini inavyoshughulikiwa na hatua zinazochukuliwa. Kamati Kuu inaipongeza Serikali na vyombo vya dola kwa namna inavyoendelea kukabiliana na wahalifu wanaotumia mgongo wa dini kuanzisha vurugu na uvunjifu wa amani katika nchi yetu. Kamati Kuu inatoa mwito kwa Watanzania kukataa vitendo vyote vinavyochochea migogoro ya kidini; wananchi wajihadhari na watu waovu wenye nia mbaya ya kuligawa taifa letu.
Pamoja na jitihada za vyombo vya
dola hadi sasa, Kamati Kuu inaitaka Serikali iandae mkakati wa kuzuia
migogoro ya kidini kabla haijajitokeza.
MAKAMPUNI NA VIWANDA VILIVYOBINAFSISHWA
Kamati Kuu imetafakari hali ya
viwanda hivi. Ni muongo mmoja umepita tangu ubinafsishaji ulipokamilika.
Kuuzwa kwa mashirika na viwanda vya umma kwa watu na makampuni binafsi
kumekuwa na matokeo ya aina mbili: yako yale yaliyobinafsishwa na
yakawa na maendeleo mazuri na kuchangia uchumi wa Taifa. Na
yako ambayo yanaendeshwa kwa kiwango cha chini au yamefungwa.
Kamati Kuu inasikitishwa na hali hii, kwani viwanda vilivyofungwa ni vile vilivyokuwa vikifanya kazi muhimu ya uzalishaji.
Viwanda hivi ni vya korosho,
usindikaji wa pamba, mafuta ya kula, viwanda vya mazao ya ngozi, na
vinginevyo. Hali hii inalikosesha Taifa fursa za ajira, kukua kwa
mapato, kuimarika kwa uzalishaji na kuongezeka kwa uuzaji wa bidhaa
zilizosindikwa na kuzalishwa nchini.
Imedhihirika kuwa wafanyabiashara
waliochukua viwanda hivyo ndiyo hao hao wanaofanya biashara ya kununua
mazao ya kilimo na mifugo na kuuza nje kama bidhaa ghafi, wakati huo huo
wakiwa wamevifunga viwanda hivi.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali
kufanya tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuvitambua vile
vilivyofungwa, na kuwataka waliouziwa wavifungue na iwapo watashindwa
kutimiza masharti yaliyowekwa, Serikali iandae utaratibu wa kuwapa watu
wenye uwezo wa kuviendesha.
WAKULIMA WADOGO WA MIWA -
Kumekuwapo na migogoro ya muda
mrefu kati ya wakulima wadogo wa miwa na Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa
mkoani Morogoro. Matatizo haya yameshughulikiwa na watendaji mbalimbali
bila ya kupatikana kwa ufumbuzi wa kudumu.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali
kuushughulikia mgogoro huu na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu matatizo ya
wakulima wadogo wa miwa haraka iwezekanavyo.
PEMBEJEO ZA KILIMO
Chama kimejiridhisha kuwa suala
la utoaji wa pembejeo za kilimo ni zuri na lenye mafanikio. Hata hivyo
Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu matatizo yanayohusiana na usambazaji
wa mbolea ya ruzuku.
Kwa baadhi ya maeneo mbolea ya
ruzuku imekuwa ikitolewa kwa watu wasiohusika na wakati mwingine
walanguzi wamekuwa wakiingilia kati ili kujinufaisha nayo.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali
kusimamia kwa umakini na kutafuta utaratibu bora zaidi na wenye tija wa
kuwafikishia wakulima mbolea, kwa wakati na kwa uhakika.
MRADI WA UJENZI WA NYUMBA ZA WATUMISHI
Kamati Kuu imepokea taarifa na
kuipongeza Serikali kwa kutayarisha mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba
za watumishi wake. Mpango huu utatoa fursa kwa wafanyakazi ya kupata
mikopo yenye masharti nafuu na hivyo kuwawezesha kuwa na makaazi yenye
uhakika.
MWISHO:
Kamati Kuu imeitaka Serikali kuwasilisha utekelezaji wa maagizo haya mara kwa mara.
IMETOLEWA NA:
Asha-Rose Migiro,
Katibu WA NEC – Siasa Na Uhusiano wa Kimataifa,
Mei 22, Dodoma.
Post a Comment