Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewaonya watu wanaosababisha uvunjifu wa amani nchini humo kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Onyo hilo linafuatia ghasia ambapo ofisi kadha, maduka na nyumba
zimechomwa katika mkoa wa Mtwara ulioko kusini mashariki mwa Tanzania jana
Akihutubia kupitia televisheni ya taifa, TBC1,
Rais Kikwete amesema wale waliokamatwa na polisi wakati wa ghasia hizo
watashitakiwa.
Ghasia hizo zilianza muda mfupi baada ya Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuwasilisha bajeti ya
wizara yake bungeni. Akizungumzia madai ya waandamanaji hao, Rais
Kikwete amesisitiza kuwa raslimali za nchi ni mali ya taifa zima.
Amesema mkoa wa Mtwara haujatelekezwa na kusema
kwamba kuna mipango ya kutumia gesi hiyo kujenga viwanda vya mbolea na
kutumia gesi hiyo asilia kuzalisha nishati ya umeme kwa mikoa ya Mtwara,
Lindi, na Ruvuma ili kuunganishwa katika gridi ya taifa.
Ofisi zachomwa
Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa mkoa wa Mtwara
kamanda Linus Sinzumwa, vurugu hizo zilitokea jana asubuhi mara baada
ya Wizara ya Madini na Nishati kusoma bajeti yake ya makadirio ya mapato
na matumizi huko Bungeni mjini Dodoma na kusababisha uharibifu wa mali.
Ametaja uharibifu huo kuwa ni pamoja na kuchomwa
kwa majengo ya serikali kama mahakama, nyumba za watendaji wa serikali,
baadhi ya majengo ya chama tawala na nyumba za watu binafsi.
Hata hivyo, kamanda huyo, amekanusha taarifa za
kuuawa kwa mtu mmoja katika eneo hilo na kubomolewa kwa daraja
linalounganisha mji wa Mtwara na maeneo mengine.
Kamanda Sinzumwa amesema watu wapatao tisini na
mmoja wanashikiliwa na jeshi na polisi kuhusiana na matukio mbalimbali
ya ghasia hizo.
Ghasia hizo, zinahusishwa na madai ya muda mrefu
sasa ya wananchi wa mkoa huo kupinga ujenzi wa bomba la gesi
iliyogunduliwa mkoani humo kusafirishwa hadi Dar es Salaam, kaskazini
mwa Mkoa wa Mtwara, kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme.
Hii ni mara ya pili mkoani Mtwara kutokea kwa
ghasia zinazohusisha maafa kwa binadamu na uharibifu wa mali kama
ilivyotokea mapema mwaka huu.
BBC
BBC
Post a Comment